Tuesday, 4 January 2011

Vuteni subira Katiba mpya- Msekwa

Na Gladness Mboma

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Bw. Pius Msekwa amewataka mwananchi mwenye mawazo Katiba kuwa na subira hadi
pale Rais Jakaya Kikwete atakapounda tume yake ndipo wayapeleke na si vinginevyo.

Bw. Msekwa aliyasema hayo jana wakati alipozungumza na gazeti hili kwa njia ya simu kutoka mjini Arusha baada ya kuombwa kutoa maoni yake kuhusu Katiba hiyo akiwa mmoja watu walioshiriki kuandika Katiba ya sasa.

"Rais ameshazungumza yote kuhusiana na Katiba mimi siwezi kuzungumza lolote mawazo yangu na ya kwako pamoja na watu wengine yanayohusu Katiba tuyapeleke katika tume itakayoundwa na Rais na siyo kuhoji mtu mmoja mmoja,"alisema na kuongeza;

"Sasa hivi tusubiri tume na siyo kusubiri maoni ya mtu mmoja mmoja, kwani haitawezekana kusikiliza maoni ya mamilioni ya watu wote kwa kuhoji mtu mmoja mmoja. Haitawezekana, ila tume itakwenda kila wilaya na kijiji kuchukua maoni ya wananchi," alisisitiza.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Rais Kikwete alitangaza mchakato wa katiba mpya katika hotuba yake ya kufunga mwaka 2010 na kukaribisha 2011, ambapo alieleza kuunda tume maalumu itakayoratibu maoni ya wananchi ili waamue jinsi wanavyotaka katiba hiyo iwe.

Katika hotuba hiyo, Rais Kikwete aliwataka Watanzania kutokuwa na jazba katika madai mbalimbali ya katiba na kuweka wazi kuwa tume atakayounda haitabagua chama, rangi, dini na kwamba itaunganisha makundi yote ya jamii.

Rais Kikwete alisema kuwa ameamua kuunda tume hiyo itakayoongozwa na mwanasheria aliyebobea, itakayokuwa na wajumbe wanaowakilisha makundi mbalimbali katika jamii kutoka pande mbili za muungano.

Hata hivyo pamoja na Rais Kikwete kuvunja ukimya kuhusu mjadala huo wa Katiba ambao uliwakuna Watanzania, baadhi yao walimeshauri kuhusu utaratibu unaofaa kwa utekelezaji.

No comments:

Post a Comment