VISHOKA WA ARDHI WAMUUMIZA KICHWA SHAMUHUNA.
Sasa wauza kiwanja cha Ikulu
Na Mwanajuma Abdi
WAZIRI wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati, Ali Juma Shamuhuna amesema lipo tatizo la baadhi ya watu kujibebesha mamlaka ya kuuza ardhi hata ikiwa serikali imeyatenga kwa kazi maalum.
Shamuhuna alieleza hayo mbele ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, alipokuwa akitoa ufafanuzi kufuatia wajumbe wa Baraza hilo kujadili hotuba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi aliyoitoa wakati alipolizindua Baraza hilo mwishoni mwa mwaka jana.
Alisema tatizo la kuuza ardhi Zanzibar limekuwepo ambapo baadhi ya watu kwa makusudi wamekuwa wakiyauza maeneo ya ardhi yaliyotengwa kwa shughuli mbali mbali bila ya kuogopa.
Alikitoa mfano alisema hivi karibuni wapo watu wameuza ardhi ya kujengewa Ikulu, katika eneo la Chuini na kujichukulia fedha za uuzaji huo.
Waziri Shamuhuna alifahamisha kuwa, alipata 'vinoti' vya kumchokoza kwamba suala la ardhi haliwezi, jambo ambalo usiku wake watu wameuza eneo la Chuini lililotengwa na Serikali kwa kujengea Ikulu siku zijazo na tayari wamegawana fedha.
Waziri huyo alivipongeza vyombo vya habari kwa kufuatilia na kuandika matatizo ya ardhi, jambo ambalo linamsaidia katika ufuatiliaji wa tatizo hilo.
Akizungumzia suala la maji safi na salama, alikiri kuwepo kwa tatizo katika huduma hiyo na kueleza kuwa hakuna Jimbo lolote lililokamilika kwa wananchi wake kupata maji ya uhakika.
Waziri Shamuhuna alisema mradi wa Japan umekamilika, lakini bado tatizo la maji lipo hivyo jitihada zinaendelea kuchukuliwa ili wananchi wapate huduma hiyo.
Aidha alisema serikali inaendelea na mchakato wa kufanyika kwa utafiti wa uwezekano wa kuchimbwa mafuta Zanzibar, ili yaweze kukuza uchumi wa nchi.
Alisisitiza kwamba, mafuta yakipatikana yatabakia ya Zanzibar na sio ya Muungano katika kuendeleza uchumi na ustawi wa jamii, sambamba na kudumishwa kwa utulivu na amani nchini, ambayo ndio shabaha kubwa ya kupatikana kwa maendeleo ya haraka.
Nae Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Omar Yussuf Mzee alisema Zanzibar ni nchi ya visiwa, hivyo uchumi wake unategemea kukuzwa kwa huduma katika bandari, utalii na uwanja wa ndege ili iondokane na utegemezi wa wahisani kutoka nje.
Alieleza katika bajeti ya serikali shilingi bilioni 171 ni mapato ya ndani ukilinganisha na bajeti yenyewe ni shilingi bilioni 424, ambapo asilimia 60 ya bajeti ni utegemezi kutoka kwa wahisani.
Waziri huyo, aliongeza kusema kwamba, ili kuondokana na masuala hayo Zanzibar inahitaji kujiimarisha ili iweze kuuza mafuta ya ndege na meli katika kutimiza malengo ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Januari 12 mwaka 1964.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Abdilahi Jihad Hassan alisema kuingizwa sekta ya utalii katika wizara hiyo itaendelea kuimarika kwa vile vyombo vya habari vina msukumo tosha wa kuelimisha jamii hususani vijijini ili nao waweze kufaidika na mapato ya nchi.
Akifanya majumuisho ya hotuba hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Mwinyihaji Makame alisema Serikali itaendelea kuimarisha rasilimali muhimu ikiwemo uvuvi, kilimo na kukuza elimu nchini.
Sambamba na kushughulikiwa upya muundo wa utumishi wa Serikali, ambapo Wizara maalum imeundwa kwa lengo la kuimarisha maslahi ya wafanyakazi.
No comments:
Post a Comment