HAKUNA UFUKWE ULIOUZWA
Hakuna ufukwe uliouzwa - SMZ
Na Mwandishi wetu
Na Mwandishi wetu
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema hakuna ufukwe uliouzwa kwa Wawekezaji Visiwani Zanzibar.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mji Mkongwe wa Zanzibar, Issa Sarboko Makarani, alisema kimsingi sheria ya ardhi inaeleza bayana kuwa ardhi yote ni mali ya Serikali ikiwemo fukwe.
“Nimeshangazwa sana na hawa watu wanaoeneza uzushi kuwa SMZ imeuza ufukwe …huu ni uongo usiokuwa na chembe ya ukweli” alisema Mkurugenzi Mkuu huyo.
Alisema sheria nambari 12 ya ardhi ya mwaka 1992, inatamka bayana kuwa Mwekezaji haruhusiwi kuuziwa ardhi bali anakodishwa tu.
Kauli ya Serikali imekuja siku chache baada ya kuwepo kwa taarifa kuwa Kampuni ya Kempinski kuuziwa ufukwe katika eneo la Ras Shangani Mjini Unguja kwa ajili ya ujenzi wa hoteli ya kitalii.
“Serikali haijauza, kilichopo ni kuwa mwekezaji Kempinski amepewa Lease (amekodishwa) tena baada ya kufuata taratibu zote na wala hakuna mizengwe yoyote” alisema Makarani.
Makarani amesisitiza kwamba Zanzibar haijauza ufukwe, bali imetoa ruhusa ya ujenzi wa hoteli ya kisasa yenye hadhi ya juu katika eneo baina ya nyumba ya kihistoria ya Mambo Msiige na Starehe Club.
Akizungumzia ujenzi unaokusudiwa kufanywa na Mwekezaji Kampuni ya Kempinski, Makarani alisema ujenzi huo kwa mujibu wa mkataba wa ukodishwaji wa eneo hilo ni wenye kuzingatia sheria na masharti ya uhifadhi na uendelezaji wa Mji Mkongwe wa Zanzibar ambao unatambuliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi Elimu na Utamaduni(UNESCO) kuwa ni urithi wa ulimwengu.
“Taratibu zinaendelea za matayarisho ya ramani itakayokidhi haja ya SMZ na matakwa ya urithi wa ulimwengu…Mamlaka itathibitisha ramani ya ujenzi baada ya kufikiwa viwango vinavyokubalika vya uhifadhi wa Mji Mkongwe, sasa nashangaa hao wanaosema maneno ya ajabu ajabu kawaambie ufukwe haujauzwa” alisisitiza Mkurugenzi Mkuu huyo.
Makarani alisema kwa sasa Mamlaka ya Uhifadhi na Uendelezaji wa Mji Mkongwe wa Zanzibar ipo katika mchakato wa kupitia ramani ya Kempinski kwa ajili ya kutazama vigezo vya Kitaifa na Kimataifa.
Aidha, amewahakikishia wananchi kwamba Zanzibar haimo katika orodha ya hatari ya kufutwa katika urithi wa Ulimwengu kwa kuwa tangu ilipotambuliwa rasmi mwaka 2000, Mji Mkongwe umeendelea kuhifadhiwa kwa mujibu wa sheria.
Vyanzo vya kuaminika kutoka ndani ya Serikali vinaeleza kuwa Kampuni ya Kempinski imelipa bilioni 2 milioni 880 kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na fedha hizo kuwekwa katika hazina ya Serikali.
Kwa mujibu wa utaratibu, ukodishwaji wa ardhi kwa mgeni hekta moja ikiwa sawa na eka 2.4 inakodishwa kwa Dola za marekani 5000 kwa mwaka ambapo Kempinski eneo alilokodishwa halijafikia hata eka moja wamekodishwa kwa Dola 10,000 kwa mwaka.
Habari kutoka Mamlaka zinazohusika zinasema kikawaida kodi ya ardhi huongezeka kati ya asilimia 10 hadi 15 ikiwa ni kodi ardhi ya ukodishwaji kwa mwaka ikiwa ni ongezeko la thamani,lakini kampuni ya Kempinski italazimika kulipa asilimia 25 kila mwaka.
Chini ya mradi huo, Kampuni ya Kempinski inatarajia kuwekeza kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 30 ambazo zitahusisha ukarabati wa jengo la kihistoria la Mambo Msiige, ujenzi wa bustani ya kisasa na hoteli yenye hadhi ya nyota tano itakayojengwa ilipokuwa starehe klabu.
Nchini Tanzania kampuni ya Kempinski imewekeza katika miradi mikubwa ya hoteli za kitalii zenye hadhi ya nyota tano ikiwemo Zamani Zanzibar Kempinksi,Bilila Lodge Kempinski Serengeti,Hotel Ngorongoro Kempinski na Kilimanjaro Hotel Kempinski Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uendelezaji wa Mji Mkongwe alisema Mwekezaji Kempinski ametakiwa kulifanyia ukarabati jengo la Mambo Msiige kuliweka katika haiba yake kulingana na maelekezo ya UNESCO ambayo tayari Mwekezaji huyo ameyazingatia.
Katika michango yao mbalimbali Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi katika vikao tofauti waliitaka Serikali kuchukua hatua ya kulihifadhi eneo la kuanzia jengo la Mambo Msiige hadi starehe klabu kwa kuwa lilikuwa ni maficho ya magenge ya kihuni.
Kuhusu kukodishwa kwa majengo ya Serikali, Sarboko amesema suala hilo limeelezwa kwa kina katika sera ya Taifa ya nyumba kama tamko la sera namba 6 linavyoeleza kuhusu azma ya Serikali kujiondoa katika umiliki na ukodishaji wa nyumba zake.
“Serikali itajiondoa kwenye umiliki na ukodishaji wa baadhi ya nyumba za Maendeleo za mjini na vijijini, baadhi ya nyumba za Mji Mkongwe,nyumba za vijijini na nyumba kongwe kwa awamu kwa kuziuza baadhi yake.
Hadi sasa jumla ya nyumba 938 za Serikali zimeuzwa kwa wananchi waliokuwa wakiishi ndani ya nyumba hizo ikiwa ni utekelezaji wa Sera ya nyumba ya mwaka 2009 iliyopitishwa Baraza la Wawakilishi.
Mwekezaji mwingine S.S. Bakhressa kwa ushauri wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, amekodishwa jengo lililokuwa likitumiwa na wizara hiyo, kwa ajili ya mradi wa hoteli ya kitalii ambapo ameshalipa dola milioni 1.5.
No comments:
Post a Comment