Tuesday, 25 January 2011

Ukimwi Upo Zanzibar Mjihadhari -Maalim



MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad ameziagiza taasisi zote visiwani humo kujipanga upya katika suala la kusimamia vita dhidi ya ukimwi.
Alisema ingawa Zanzibar ina kiwango kidogo cha maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi, juhudi mpya inahitajika kuhakikisha kiwango hicho hakiogezeki.
Maalim Seif alitoa agizo hilo wakati anazungumza na viongozi wa tume ya ukimwi Zanzibar (ZAC) kwenye makao makuu ya taasisi Shangani Mjini Unguja.
Alisema vita dhidi ya ukimwi vinahitaji ushirikiano wa jamii kwa jumla lakini viongozi kuanzia masheha wakuu wa wilaya na wa mkuu wa mikoa na viongozi wa dini na wanasiasa wanapaswa kuwa mstari wa mbele.
“Kila mmoja katika jamii, wakiwemo walimu na hata wazazi wawe na tabia ya kukaa na watoto kuwafundisha juu ya mambo mabaya” alisema Maalim Seif.
Maalim Seif ambaye ni makamu wa kwanza wa rais alisema viongozi wa dini kwa upande wao waongeze juhudi katika suala la ufundishaji maadili, hasa juu ya mavazi kwa vijana wa kike na wa kiume.
“Vijana wengi wamepotea kimaadili, wa kike wanavaa nguo za kushindana kuonyesha magoti na wa kiume wanashindana kuvaa vidani na kusuka nywele kama wanawake” alisema Maalim Seif.
Alisema katika hatua hii ya kupambana na ukimwi kila kiongozi lazima aweke suala la ukimwi katika kila mazungumzo yake na wananchi.
Maalim Seif alisema ili kufnikisha vita hiyo ZAC inatakiwa kufanya utafiti zaidi kujua kama kiwango cha asilimia 0.6 cha maambukizo kinaongezeka au kinapungua.
“Zanzibar imefanikiwa kudhibiti ukimwi na kusababisha kazi ya maambukizo kubakia asilimia 0.6 lakini utafiti utasaidia serikali kuandaa na kutekeleza mikakati ya vita dhidi ya ugonjwa huu kwa usahihi zaidi ikizingatia takwimu zilizotokana na utafiti” alisisitiza Maalim Seif.
Maalim Seif aliongeza ingawa kiwango cha asilimia 1 (one percent) cha maambukizo ni kidogo lakini ni kikubwa kulinganisha na idadi ya watu wote 1.3 millioni ya wazanzibari.
Mgonjwa wa kwanza wa ukimwi Zanzibar aligundulika mwaka 1986, miaka mitatu baada ya mgonjwa wa aina hiyo kugundulika Tanzania Bara mwaka 1983

No comments:

Post a Comment