Na Salma Said,
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF) Maalim Seif Sharif Hamad amesema kwamba chama chake kinaunga mkono hatua ya Rais Jakaya Kikwete kuanzisha mchakato utakaoiwezesha Tanzania kuwa na Katiba mpya.
Maalim Seif amesema kuundwa kwa Tume itakayowashirikisha wajumbe wa Zanzibar na Tanzania bara kuendesha shughuli za mchakato huo ni hatua nzuri ya kuanzia katika kufikia utekelezaji wa dhamira hiyo.
Hivi karibuni akizungumza na wananchi katika salamu za mwaka mpya Rais Kikwete alisema amekubaliana na maoni yaliokuwa ayakitolewa na wananchi na wasomi mbali mbali juu ya haja ya Tanzania kuwa na katiba mpya huku akiahidi kuunda kamati itakayosimamia mchakato huo.
Akiongea na waandishi wa habari huko Mtoni Mjini Unguja, Maalim Seif alisema hali inavyokwenda wananchi wengi wamehamasika kutaka kutoa maoni juu ya kuwa na katiba mpya hivyo ni vizuri wananchi wakapata nafasi ya kutoa maoni yao kwa kuwa katiba inayowashirikisha wananchi ndio katiba madhubuti nchini.
Maalim Seif ambaye ni makamu wa kwanza wa rais wa Zanzibar alisema wananchi ni wadau muhimu katika kutoa maoni ya katiba wanayotaka iwaongoze na kuwashauri wananchi kuunga mkono dhamira ya Rais Kikwete ya kutaka kuunda kamati ya mchakato huo.
Siku za mapumziko Maalim Seif amekuwa akiutumia katika shughuli za chama chake ambapo jana aliwakabidhi wanachama wapya 56 waliojiunga na chama hicho katika tawi la liitwalo Monduli Jimbo la Mtoni Mjini Unguja.
Maalim Seif alisema katiba upya ni muhimu na vizuri kuwekewa mazingira mazuri ya utekelezaji wake hasa kwa kuzingatia umuhimu wa suala lenyewe la uundwaji wa katiba mpya ambapo inahitajika elimu kwa wananchi na kufanyiwa kazi upya suala la mahitaji ya katiba hiyo.
Alisema suala la katiba mpya linahitaji kufanyiwa kazi na wataalamu kwa kuwa katiba ni suala ambalo linapaswa kushirikishwa wananchi na wadau mbali mbali wa nchi hii kwa kuwa katiba iliyo bora na yenye kukidhi matakwa halisi ya wananchi ni ile inayowashirikisha wananchi wote katika nchi yao ili watoe maoni na hatimae katiba mpya ikidhi matakwa yao na sio matakwa ya viongozi.
“Jamani hivi sasa mambo yanabadilika ni muhimu kuwa na Tume ya kutafuta maoni kutoka kwa wadau wa pande zote mbili za Muungano, katiba mpya tumeipigia kelele sana sisi na chama chetu na sasa Alhamdulillah mchakato huo bado unaendelea naona ni mwanzo mzuri wa rais kuunga mkono suala hilo” alisema Maalim.
Wakati huo huo Maalim Seif amewasisitiza watendaji wa Serikali kuwatumikia wananchi kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo bila kuingiza itikadi za kisiasa katika kutekeleza wajibu wa majukumu yao.
Amesema wakati umefika kwa watendaji hao kuweza kutofautisha shughuli za vyama na zile za serikali, na kwamba serikali haitomvumilia mtumishi yeyote wa umma atakayebainika kuwabagua wananchi kwa itikadi za kisiasa. “Hatumuachii kiongozi yeyote atakayebagua watu kwa itikadi za vyama”, amesema Maalim Seif huku akisisitiza kuwa viongozi wa juu wa serikali wanashirikiana vizuri katika kuwatumikia wananchi.
Amewataka watendaji wenye tabia hiyo kujirekebisha kabla ya hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi yao “Ubaguzi wowote ni haramu na hatutokubali kwa aina yoyote kuona mtu anabaguliwa katika nchi yetu kwa misingi ya kidini au kitikadi za vyama”, alisema Maalim Seif.
Amesema lengo la serikali ya mapinduzi ya Zanzibar yenye mfumo wa umoja wa kitaifa ni kuwaunganisha wazanzibari kuwa kitu kimoja kwa lengo la kurahisisha maendeleo yao na sio vyenginevyo.
Amefahamisha kuwa serikali pia ina dhamira ya kuimarisha misingi ya utawala wa sheria, ili kila mtu aweze kupata haki zake za msingi zikiwemo huduma za kijamii.
Amesema serikali inaendelea kujipanga kushughulikia kero zinazowakabili wananchi zikiwemo huduma za elimu na maji safi na salama.
Aidha amesema tayari serikali imeanza mchakato wa kushughulikia tatizo la maji Zanzibar, ili wananchi waweze kupata huduma hiyo kwa uhakika, licha ya kwamba inaweza kuchukua muda mrefu kuweza kukamilisha kazi hiyo kutokana na gharama kubwa za uendeshaji.
“Jimbo la mtoni peke yake linahitaji shilingi milioni mia nane (800), sasa angalia mara hamsini itakuwa ni kiasi gani”, alihoji Maalim Seif.
Akizungumzia kuhusu sekta ya afya amesema katika kipindi kifupi kijacho, sekta hiyo itakuwa na mabadiliko makubwa kwa kuboresha huduma zake kwa maslahi ya wananchi wote.
Kwa upande mwengine Maalim Seif ameunga mkono hatua iliyochukuliwa na Wizara ya Miundombinu ya kutoruhusu meli zenye matatizo kusafirisha abiria, pamoja na utaratibu uliowekwa wa abiria kufika bandarini kwa muda uliopangwa ili kupunguza msongomano bandarini hapo.
Amesema kitu muhimu zaidi ni usalama wa wananchi na mali zao kuliko kuangalia maslahi ya watu binafsi na biashara. “usalama wako mwananchi ndio kitu muhimu kuliko kitu chochote katika maisha” aliongeza.
Aidha amesema Wizara ya Biashara, viwanda na masoko nayo ina kazi kubwa ya kuhakikisha kuwa vyakula vibovu haviingii nchini na kutoruhusu vifaa vya kielektroniki vilivyopitwa na wakati kuingia nchini kwa lengo la kuiepusha Zanzibar kugeuzwa jaa la bidhaa chakavu. “Hatuwezi kuruhusu Zanzibar iwe jaa”. Aliongeza.