Friday, 28 January 2011

Mwandishi apigwa kikatili Zanzibar


na Mohamed Said Abdullah, Zanzibar
Mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha Channel Ten, Munir Zakaria, juzi, alikamatwa na kupigwa na askari wa Baraza la Manispaa ya Zanzibar katika eneo la Darajani na baadaye kutakiwa kusalimisha kamera na mkanda wa video.
Tukio hilo limetokea wakati mwandishi huyo akifuatilia zoezi la kuwaondoa wafanyabishara katika maduka ya makontena yaliyo eneo la Darajani na wale wanaopanga biashara katika eneo la wazi la shule ya msingi na sekondari ya Darajani.
Wakati mwandishi huyo akimulika sehemu ya mgogoro huo, askari hao wa manispaa walimvamia na kumweka chini ya ulinzi kabla ya kumpakia katika gari la manispaa huku wakitumia nguvu na kumtaka kusalimisha vitendea kazi vyake kwa sharti la kuwekwa rumande endapo atapinga kutekeleza amri hiyo.
Baadhi ya wananchi walioshuhudia tukio hilo walisema askari hao walimkamata Munir na kumueleza kuwa ni mchochezi na mhamasishaji wa vurugu zinazofanywa na wafanyabiashara wanaopinga maduka yao kufungwa kwa siku ya nne mfululizo na wengine wakilalamika maduka yao kuvunjwa usiku na kuchukuliwa bidhaa bila ya wenyewe kuwepo.
Mashuhuda hao walisema, askari hao walimdhalilisha Munir kwa kumbeba kwa staili ya ‘Tanganyika Jeki’, kumpiga kiunoni, begani na chini ya taya, kabla ya kumrusha kama gunia la mchele katika karandinga la manispaa lenye namba za usajili SMZ 4740 na kumfikisha makao makuu ya manispaa hiyo.
Baada ya kufikishwa katika ofisi za manispaa, Munir alifuatwa na askari kadhaa wa manispaa hadi ofisi ya mkurugenzi Rashid Ali Juma ambaye alikuwa akimfokea mwandishi huyo wa habari na kumshutumu kuwa ni mchochezi na mhamasishaji wa vurugu hizo za Darajani.
Mkurugenzi huyo, alimpatia Munir masharti matatu, kusalimisha vitendea kazi ikiwemo kamera na mkanda wa video au kuswekwa kizuizini kwa makosa ya kushupalia habari za mgogoro huo wa Darajani.
“Munir taarifa zetu, zinaonyesha kuwa kila unapokwenda Darajani na kuwahoji wafanyabishara, hamasa zinapanda. Wafanyabiashara wanaanza kuwashambulia askari wetu, hatutaki mpige picha eneo la Darajani, katafuteni habari maeneo mengine, kwani lazima Darajani?!” alisema Rashid Ali Juma.
Baada ya majadiliano yaliyochukua zaidi ya saa mbili, hatimaye Munir Zakaria aliachiwa huru baada ya kusalimisha mkanda wa video ambao alikabidhiwa jana saa 12.40 mchana kwa masharti ya kufuta picha zote alizopiga Darajani zilizokuwa zikiwaonyesha askari wa manispaa waliokuwa kwenye lindo la eneo la Darajani.
Naye Munir Zakaria alithibitisha kukamatwa na kupigwa na askari hao wa manispaa, na tayari amesharipoti tukio hilo katika kituo cha polisi cha Malindi na kupatiwa RB namba MAL/R/B358/2011 na kudai kuwa tukio hilo limeingilia uhuru wa vyombo vya habari katika kutekeleza wajibu wao.
“Wamenikamata. Wamenipiga, wamenidhalilisha mbele ya jamii, sifahamu kitu gani kinachofichwa wakati yanayofanyika yako mbele ya macho ya watu, haiwezekani watu wazima wanapigwa magongo bila ya kuwa na hatia yoyote,” alisema Munir.
Kwa upande wake Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko, Nassor Ahmed Mazrui, amelaani vitendo vya unyanyasaji vinavyoendelea kujitokeza katika eneo hilo la Darajani, hasa baada ya maduka kuvunjwa na mengine kufungwa kwa siku ya nne mfululizo.
Waziri Mazrui alisema wafanyabiashara hao wamekuwa wakidhalilishwa na baraza hilo kwa muda mrefu, jambo ambalo alisema si la kiungwana na liko nje ya misingi ya taratibu za utawala bora.
Alisema kabla ya operesheni hiyo kufanyika vyombo vyote vinavyohusika vilistahili kuhusishwa ikiwemo uongozi wa wafanyabishara, hasa kwa kuzingatia wafanyabishara hao ni raia na wana haki ya kutafuta riziki ndani ya nchi yao.
Alisema kama waziri mwenye dhamana na masuala ya biashara atafuatilia mgogoro huo mara baada ya kumalizika kwa vikao vya Baraza la Wawakilishi kwa kukutana na pande zote zinazohusika ili tatizo hilo litafutiwe ufumbuzi wa kudumu.
Tangu kuibuka kwa mgogoro huo watu wanne wamejeruhiwa katika operesheni ya kwanza ya kuwahamisha wafanyabiashara hao, tangu Serikali ya Umoja wa Kitaifa ilipoanza kutekeleza majukumu yake.

No comments:

Post a Comment