Friday, 28 January 2011

Mamlaka hali ya hewa yatoa tahadhari

Na Waandishi Wetu, jijini

MAMLAKA ya hali ya Hewa Nchini (TMA) imetoa tahadhari kwa wananchi kuacha kukaa ufukweni mwa bahari kutokana na tishio la kuwapo kwa kimbunga katika Bahari ya Hindi.Akizungumza na gazeti hili leo asuhuhi, Mkurugenzi wa TMA, Agnes Kijazi, amesema utabiri wa hali ya hewa umebaini kuwpao kwa kimbunga hicho hivyo ni vyema wananchi wakaanza kuchukua tahadhari mapema.

Amesema upepo huo huenda ukaleta madhara katika mwambao wa Bahari ya Hindi, Visiwa vya Unguja na Pemba Tanzania.

Kumekuwapo na upepo mkali katika mwambao wa Bahari ya Hindi Tanzania pamoja na Visiwa vya Unguja na Pemba kuanzia usiku wa Januari 25, mwaka huu, upepo unaofikia kilomita 30 hadi 40 kwa saa.

Upepo huo umekuwa mkali kutokana na kuimarika kwa mkandamizo wa hewa (air-pressure) katika maeneo ya Kaskazini-Mashariki hadi Pwani ya kaskazini mwa Tanzania sambamba na kuwapo kwa mkandamizo hafifu wa hewa katika Rasi ya Msumbiji.

Hali hiyo inatarajiwa kuendelea hadi leo Januari 27, Pwani ya Kaskazini na hadi Januari 28, mwaka huu, kwa Pwani ya Kusini.

Kijazi amesema leo upepo utatoka Kaskazini Mashariki kwa kasi ya kilomita 40 kwa saa, mita tatu na nusu ambapo Januari 28, mwaka huu utatoka Kaskazini Mashariki kwa kasi ya kilomita 30 kwa saa pia utatoka Kaskazini magharibi kwa kasi ya kilomita 40 kwa saa.

Januari 29, mwaka huu utatoka Kaskazini Mashariki kwa kasi ya kilomita 30 kwa saa na utatoka Kaskazini Magharibi kwa kasi ya kilomita 30 kwa saa na mita 2 na nusu hadi 3.

“Ninawaomba wananchi wasipende kukaa ufukweni katika kipindi hiki, juu ya miti na kukaa mbali na majengo ambayo si imara ili kuepuka madhara,” amesema.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa baadhi ya nyumba jijini Dar es Salaam zimeezuliwa paa zake kutokana na upepo mkali ulionza kuvuma tangu juzi.Habari hii imeandaliwa na Christina Gauluhanga, Khadija Idd na Stella Aron.

No comments:

Post a Comment