3rd December 2010



.jpg)
Taifa linapita katika kipindi kigumu cha machungu kufuatia kuharibika kwa mitambo ya kufua umeme kwa upande mmoja huku ya kusukuma maji nayo ikiharibika hivyo kusababisha uhaba wa maji.
Majanga haya mawili sasa yamesababisha kwanza mgawo wa umeme kwa mikoa 15 sawa na asilimia 71.4 ya Tanzania Bara, huku Jiji la Dar es Salaam likiathirika zaidi kutokana na kuongezewa mzigo wa mgawo wa maji baada ya mitambo ya kusuma maji ya Ruvu Chini kuharibika.
Shirika la Umeme nchini (Tanesco) jana lilithibitisha kwamba mgawo wa umeme sasa ni kwa mikoa 15 ikielezea hali hiyo iliyosababishwa na kuharibika kwa mitambo ya kufua umeme ya Songas jijini Dar es Salaam, kuharibika kwa mtambo mwingine wa Pangani Tanga na kupungua kwa kina cha maji katika bwawa la Kihansi.
Akifafanua taarifa ya Tanesco, Meneja Mawasiliano wa shirika hilo, Badra Masoud, alisema mashine namba tatu katika mtambo wa kuzalisha umeme wa Songas jijini Dar es Salaam imeharibika, mashine mbili za mtambo wa gesi wa Ubungo, mashine namba mbili katika maporomoko ya Pangani na kupungua kwa kina cha maji eneo la Kihansi.
Badara alisema kuharibika kwa mashine hizo kumesababisha upungufu wa uzalishaji wa megawati 150 za umeme ambao unaingia katika gridi ya taifa hivyo kuathiri mikoa ambayo imeunganishwa kwenye gridi ingawa ambayo haijaunganishwa kama Kigoma bado ina umeme wa kutosha.
Alitaja mikoa itakayoathiriwa na hali hiyo kuwa ni Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Dodoma, Singida, Tabora, Mwanza, Mara, Mbeya, Iringa, Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Shinyanga na Tanga.
Alisema mafundi wanaendelea na matengenezo ya mashine hizo kuhakikisha hali ya inarudi kuwa ya kawaida ili kumaliza tatizo la mgao wa umeme.
Katika kukabiliana na tatizo la mgao katika mikoa hiyo Tanesco imewasha mashine mbili za IPTL za jijini Dar es Salaam ambapo megawati 50 zitazalishwa.
Alisema wamelazimika kuwasha mashine mbili za IPTL kutokana na gharama kubwa za mafuta ambazo zingeweza kutumika kama wangewasha zote.
Baada ya mashine za IPTL zitasaidia kupunguza tatizo na hivyo kuacha pengo la Megawati 100 kati ya 150 zilizojitokeza kutokana na kuharibika mitambo ya kuzalisha umeme.
Hali ya umeme ikiwa tete kiasi hicho na kulazimisha matumizi makubwa ya jenereta katika uzalishaji na utoaji huduma katika mikoa hiyo, athari za kiuchumi zinabashiriwa kunyemelea taifa kutokana na kuongezeka kwa gharama za uzalishaji.
Hali hii inatokea wakati kukiwa na hofu ya kutokea kwa upungufu mkubwa wa maji katika mabwawa makubwa ya kuzalisha umeme kutokana na kutokunyesha kwa mvua za vuli mwaka huu, ingawa bado bwawa kuu la Mtera linalipotiwa kuwa na maji yakiwa na kina cha mita 693.11 chini ya kiwango cha juu cha mita 698.3.
Maji hayo yanaelezwa kuwa yanatosheleza kuzalisha umeme hadi Aprili mwakani kama maji zaidi hayataongezeka kwa kuwa kina cha chini cha kuzalisha umeme ni mita 690. Kuna ziada ya mita 3.11 wakati Tanesco inahitaji sentimeta tatu kwa siku kuzalisha umeme.
Wakati umeme ukisababisha ugumu wa maisha kwa wakazi wa mikoa 15 nchini, Mamlaka ya Maji Safi mkoa wa Dar es Salaam (Dawasco), wametangaza kuharibika kwa mtambo wa kusuma maji wa Ruvu chini.
“Dawasco inawatangazia wateja wake wote na wakazi wa Jiji kwa ujumla kwamba mtambo wake wa Ruvu Chini umepunguza uzalishaji maji kutokana na kuharibika kwa pampu zake mbili zinazosukuma maji,” imesema taarifa hiyo ambayo imetolewa kama tangazo kwenye vyombo vya habari leo.
Maeneo ambayo yantaathirika na hali hiyo ni Bagamoyo, Tegeta, Boko, Bunju, Mbezi Beach, Kawe, Mikocheni, Masaki, Oysterbay, Msasani, Mlalakuwa, Kijitonyama, Sinza na Magomeni.
Maeneo mengine ni Ubungo eneo la Viwanda, Manzese, Mwenge, Mwananyamala, Kinondoni, Ilala, baadhi ya maeneo ya Chang’ombe, Keko, Upanga, Magogoni na katikati ya jiji. Dawasco imesema kuwa juhudi za kurekebisha hali hiyo zinaendelea.
SOURCE: NIPASHE
No comments:
Post a Comment