Tuesday, 1 October 2013

Obama amewahakikishia Wanajeshi kuendelea kupata mshahara wao licha ya Bunge kushindwa kupitisha Bajeti
Na Nurdin Selemani Ramadhani

Rais wa Marekani Barack Obama amejitokeza na kutoa hakikisho kwa Vikosi vyote vya Usalama nchini humo ya kwamba wataendelea kupata mishahara yao lkama kawaida icha ya Wabunge kukwamisha kupitisha Bajeti ya Nchi hiyo kitu ambacho kitachangia kukwama kwa shughuli nyingine za Serikali. 

Bunge la Congress ambalo limesitisha shughuli zote za Serikali baada ya kushindikana kupitishwa kwa Bajeti

Obama alilazimika kujitokeza na kuhutubia Vikosi vya Usalama nchini Marekani kupitia video maalum iliyorekodiwa baada ya kukwama kwa Bajeti kitu ambacho kimeanza kuzua hofu huenda Wanajeshi nao wakaingia kwenye mkumbo wa kukosa mishahara kama wafanyakazi wengine wa Serikali.

Kiongozi huyo wa Serikali ya Washington amesema hatua ya Baraza la Congress kushindwa kupitisha Bajeti kutakuwa na madhara kwenye utendaji wa Serikali lakini hakutakuwa na athari zozote kwa Wanajeshi wa nchi hiyo kwani wenyewe watapata mishahara yao kama ilivyopangwa.

Obama amesisitiza wanajeshi na wanausalama wote watapata mishahara yao kwa wakati lakini wafanyakazi wengine wa serikali zaidi ya Laki Saba wataendelea kuathirika kwa kukosa mishahara yao kwa wakati kwa kuwa Serikali haina fedha tena za kujiendesha kwa sasa.

Rais Obama amesema suala la usalama litaendelea kupewa kipaumbele na ndiyo maana watafanya kila linalowezekana kwa wanausalama wote nchini Marekani waendelee kupata mishahara yao ili watekeleza jukumu la kulinda taifa hilo dhidi ya kitisho kutoka kwa maadui zao.

Bajeti ya Serikali ilikwama kutokana na Wabunge wa Chama Cha Republican kupiga kura ya hapana wakati wanaipitisha wakidai ni lazima Rais Obama asitishe sheria ya Bima ya Afya ambayo imekuwa ikitoa nafasi kwa wananchi wengi wa Marekani kupata na hivyo kuigharimu Serikali fedha nyingi.

Mchuano mkali ulishuhudiwa katika Baraza la Congress ambapo Wabunge wa Republican walijiapiza kutopitisha Bajeti hiyo ambayo imekuwa ikipigiwa debe na wenzao wa Democrats ambao wanasema Bima ya Afya ndiyo mkombozi kwa wananchi wenye hali ya chini.

Kukwama kupitishwa kwa Bajeti ya Serikali ya Marekani kumeongeza tishio kwa wafanyakazi kupoteza ajira zao iwapo hali itaendelea kuwa hivyo kwani serikali itashindwa kabisa kutekeleza majukumu yake kama inavyopaswa.

Hii ni mara ya pili Marekani inashuhudia wabunge wakikwamisha kupitishwa kwa Bajeti kwani mara ya kwanza ilikuwa mwishoni mwaka uliopita na hivyo kumlazimu Rais Obama kusitisha mapumziko yake na kuwashawishi wabunge kupitisha bajeti ya dharura.

 

No comments:

Post a Comment