Maalim Seif ataka Zanzibar huru
Maalim Seif ataka Zanzibar huru
NA LULU GEORGE
Makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad
Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), aliyasema hayo juzi wakati wa Kongamano la Wazanzibari waishio Tanzania Bara na kusema kuwa Muungano uliotiwa saini na waasisi wa Muungano huo umefichwa na hivyo kusema dawa yake ni kuwapo kwa Serikali tatu na Muungano wa mkataba.
Maaalim Seif alimtaka Rais Jakaya Kikwete kutosaini Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2013 kwa maelezo kuwa una kasoro.
“Wazanzibar wenzangu, mimi pia ni mmoja wa Wazanzibar ambao tunataka Muungano wa mkataba… nilipoulizwa na tume nilisema nataka Muungano wa mkataba… nadhani nanyi pia mawazo yenu ni kama mimi,” alisema.
Hata hivyo, aliisifu Serikali ya Rais Kikwete kwa kuwaachia wananchi wenyewe kuiandika Katiba yao, lakini alimtahadharisha kutokuwa na wazo la kutia saini Muswada huo.
Alisema Zanzibar ni nchi kamili yenye mamlaka kama ilivyo kwa nchi nyingine, hivyo inahitaji kurejeshewa mamlaka yake na kuwa na maamuzi ikiwa na pamoja kurejeshewa kiti chake katika Baraza la Umoja wa Kimataifa (UN).
“Zanzibar iko na haki ya kuingia mikataba na jumuiya za kimataifa kama ilivyo nchi nyengine, tunataka dola ya Zanzibar iliyo nchi kamili kama ilivyokuwa zamani… Muungano umeifuta Zanzibar katika ramani ya kimataifa,” alisema na kuongeza:
“Hivi sasa Zanzibar haina haki ya kusema inajiunga na jumuiya yoyote ya kimataifa, kikwazo hiki ni kufichika kwa makubaliano ya Muungano kutoka kwa waasisi wetu, tunasema umefichwa.”
Kwa mujibu wa Maalim Seif, ili kuondoa migogoro na manung’uniko ya pande zote mbili ni kuwapo kwa Serikali tatu na Muungano wa mkataba, jambo ambalo litaondosha kelele zote za Muungano na kupelekea ustawi wa jamii na umoja na mshikamano miongoni mwa wananchi.
Aliwataka Wazanzibar wanaoishi Tanzania Bara kwa pamoja kushikamana na kutunza umoja wao na kuhakikisha Katiba Mpya inaweka madai yao likiwamo la kutaka Muungano wa mkataba.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment