Friday, 4 October 2013

Gesi, mafuta yaivuruga Katiba


Waandishi Wetu

Utiaji saini kati ya Zanzibar na kampuni ya Shell
  • - Dk. Shein ‘amalizana’ na Shell Uholanzi
  • - Zanzibar kuanzisha shirika lao la mafuta
SASA ni dhahiri kwamba sekta ya mafuta na gesi inaivuruga Katiba ya sasa ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania baada ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), kuingia mikataba ya kimataifa nje ya Muungano kinyume cha Katiba hiyo, Raia Mwema imethibitisha.
Tayari Rais wa SMZ, Dk. Ali Mohamed Shein, ameingia makubaliano ya awali na kampuni ya kimataifa ya mafuta ya Shell wa kufanya utafutaji mafuta visiwani humo, makubaliano aliyoyafanya akiwa nchini Uholanzi Agosti, mwaka huu.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania Pamoja na mambo mengine, mambo ya Muungano yanayotajwa ni mafuta pamoja na gesi ambayo yamo katika nyongeza ya kwanza ya Katiba, kifungu cha 15 kinachosema; “Maliasili ya mafuta, pamoja na mafuta yasiyochujwa ya motokaa na mafuta ya aina ya petroli na aina nyinginezo za mafuta au bidhaa, na gesi asilia.”
Ibara ya 4 (3) inasema; “Kwa ajili ya utekelezaji bora wa shughuli za umma katika Jamhuri ya Muungano, na kwa ajili ya mgawanyo wa madaraka juu ya shughuli hizo baina ya vyombo vilivyotajwa katika ibara hii, kutakuwa na Mambo ya Muungano kama yalivyoorodheshwa katika Nyongeza ya Kwanza iliyoko mwishoni mwa Katiba hii.”
Gazeti hili linafahamu kwamba SMZ imeipa Shell vitalu vinne vilivyopo Zanzibar vilivyopewa majina ya Block 9, 10, 11 na 12 kuvifanyia utafutaji wa mafuta na baadaye kupewa umiliki endapo mafuta yatapatikana.
Makubaliano hayo yanaonyesha kwamba Zanzibar tayari imeanza kutazama maslahi yake nje ya muungano kwa vile masuala ya mafuta awali yalikuwa yakishughulikiwa kimuungano.
Ubia kati ya SMZ na Shell ulifikiwa wakati wa ziara ya kiserikali ya siku tano nchini Uholanzi iliyofanywa Agosti mwaka huu na Rais wa SMZ, Dk. Ali Mohamed Shein.
Raia Mwema limefanikiwa kuona nakala ya Makubaliano hayo ya awali (Memorandum of Understanding) baina ya pande hizo mbili ambapo kuna sehemu mbili ambazo zinaonyesha namna Zanzibar ilivyojiandaa maisha nje ya muungano.
Kifungu cha tatu cha makubaliano huo kinasema hivi; “SMZ inataraji kupata haki zote za mafuta na gesi zilizo chini ya eneo lake na ikipata haki hizo inataraji kuipa Shell haki zote za mafuta,” kinasema kifungu hicho.
Kifungu cha tano cha makubaliano hayo kinakwenda mbali zaidi kwa kusema; “Mara baada ya SMZ kupata mamlaka yote kuhusu masuala ya mafuta na gesi, itakaa na Shell na kisha kuzungumza kuhusu kuingia mkataba au kuipa leseni kampuni hiyo inayohusiana na vitalu 9, 10, 11 na 12.”
Mamlaka yanayozungumzwa na kifungu hicho ni wazi yanahusu masuala ya mafuta kuondolewa kutoka katika masuala ya muungano.
Maamuzi kuhusu “mamlaka” ya Zanzibar yanatarajiwa kufikiwa hivi karibuni kwani mkataba huo huo unaeleza kwamba ni lazima mambo yaende haraka ili “Taifa la Zanzibar” lipate faida ya shughuli hizo.
Serikali ya Muungano wa Tanzania (SMT) ilikuwa imetoa vitalu hivyo vinne vya Zanzibar kwa Shell tangu mwaka 2002 lakini hakukufanyika kitu kutokana na SMZ kugomea suala hilo la mafuta kusimamiwa na SMT.
Gazeti hili lilizungumza na mmoja wa mawaziri waandamizi wa SMZ wiki hii kuhusu suala hili na alithibitishia kwamba makubaliano hayo yamefikiwa na sasa kazi ni kwa Shell.
Alipoulizwa kwanini SMZ imekubali Shell ianze kazi sasa wakati imekuwa ikikataliwa tangu mwaka 2002, waziri huyo alisema; “Tumekubaliana katika vikao vya kero za muungano kwamba Zanzibar iruhusiwe kuendelea na suala hili pasipo kuingiliwa na SMT.
“Kimsingi, tuko katika hatua za mwisho kuanzisha kitu kama TPDC ya Tanzania. Hii itatusaidia kujipanga na kuweka mazingira vizuri. Kwa asilimia 70, dhamira hii imetimia,” alisema waziri huyo ambaye hakutaka kutajwa jina kwa vile si msemaji wa serikali kwenye masuala ya mafuta.
Alipozungumza na Raia Mwema kuhusu suala hilo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, alisema SMZ haijakosea kitu kwenye suala hilo.
“Kimsingi, walichoingia ni MoU na si mkataba kamili. Kama wangekuwa wameingia kabisa mkataba kingekuwa kitu kingine lakini kwa hatua ambayo wameichukua hadi sasa, hakuna tatizo lolote,” alisema.
Nyaraka zilizopo zinaonyesha MoU hiyo iliingiwa kati ya Rais Shein na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Shell, Peter Voser.
Katika makubaliano hayo, Shell imeahidi kutoa kiasi cha dola milioni moja (Sh bilioni 1.6) kwa ajili ya kusaidia masuala mbalimbali ya kijamii visiwani Zanzibar.
Mkataba huo unaeleza wazi kwamba endapo yatatokea matatizo yoyote katika utekelezaji wa mkataba huo, sheria za England ndiyo zitatua matatizo hayo.
Kwa mujibu wa rekodi zilizopo, Shell ni kampuni ya pili duniani kwa mapato makubwa miongoni mwa makampuni ya mafuta duniani. Inachukuliwa kuwa miongoni mwa makampuni sita makubwa zaidi duniani kwenye sekta hiyo.
Kampuni hiyo inafahamika kwa kirefu kwa jina la Royal Dutch Shell ikiwa imeanzishwa mwezi Februari mwaka 1907 ikiwa ni muunganiko wa kampuni mbili kubwa za mafuta za Shell Transport and Trading Company ya Uingereza na Royal Dutch Petroleum Company ya Uholanzi ambayo jina lake kwa kidachi ni N.V. Koninklijke Nederlandsche Petroleum Maatschappi.
Kwa mujibu wa tovuti ya kampuni hiyo, jina la Shell limetokana na biashara ya kwanza ya baba wa waliokuwa wamiliki wa kampuni hiyo ya Kiingereza ambaye alikuwa akiuza magamba ya nje ya wanyama wa baharini (shells).
Kampuni ya Shell imewahi kukumbwa na kashfa mbalimbali kutokana na uendeshwaji wake. Imewahi kutuhumiwa kwa kuchafua mazingira ya eneo la Delta ya Nigeria kutokana na matumizi yake ya miundombinu chakavu na umwagaji wa mafuta machafu.
Pia, mwaka 1995, kampuni hiyo ilidaiwa kushiriki katika mikakati ya mauaji ya mwanaharakati na mtetezi wa haki za wananchi wa Ogoni, Nigeria, Ken Saro Wiwa, aliyeuawa hatimaye na utawala wa kijeshi wa nchi hiyo.
Kampuni inadaiwa kuwa na tabia ya kuingilia mambo ya ndani ya nchi kiasi kwamba inadaiwa kupandikiza watu wake katika serikali na Jeshi la Nigeria huku ikitoa msaada kwa Tume ya Uchaguzi ya taifa hilo lenye watu wengi zaidi barani Afrika.
Kufikia mwaka jana, Shell ilikuwa na wafanyakazi takribani 87,000 duniani kote na mapato yake yalitajwa kufikia kiasi cha dola bilioni 467 (Sh 747 trilioni).
Kwa kiwango hiki cha mapato ya mwaka mmoja ya kampuni ya Shell yanaweza kuendesha serikali ya Tanzania kwa zaidi ya miaka 40 pasipo kuomba msaada popote. Kwa maelezo zaidi kuhusu Kampuni ya Shell, soma ukurasa wa tano wa gazeti hili.
Chanzo: Raia Mwema

No comments:

Post a Comment