Tume ya Warioba yatishia kujiuzulu..
Tume ya Warioba yatishia kujiuzulu..
Mwandishi WetuToleo la 317 25 Sep 2013..
Profesa Baregu, Kabudi, Butiku wawasha moto
TUME ya Mabadiliko ya Katiba inayoongozwa na Waziri Mkuu wa zamani, Jaji Joseph Warioba, sasa inasuburi uamuzi wa mwisho wa serikali kuhusu Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba uliopitishwa hivi karibuni bungeni, ili hatimaye kwa pamoja wajumbe wa tume hiyo waamue kujiuzulu ama waendelee na majukumu yao, Raia Mwema limeelezwa.
Kwa mujibu wa vyanzo vyetu mbalimbali vya habari ndani ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, katika kikao chake cha mwanzoni mwa wiki iliyopita jijini Dar es Salaam, sehemu kubwa ya wajumbe walikuja juu wakionyesha kukerwa na namna mabaraza ya katiba yalivyoingiliwa na Chama cha Mapinduzi.
Mbali na kukerwa huko, vyanzo vyetu vya habari vinaeleza kwamba wajumbe hao pia hawakubaliani na baadhi ya vifungu vya Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, ambao uliungwa mkono na wabunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM) pamoja na Mbunge wa Vunjo (TLP) Augustine Mrema na kwa upande mwingine, muswada huo ukipingwa na wabunge wengine wa Kambi ya Upinzani Bungeni, ambao walifikia hatua ya kupambana na askari wa Bunge ndani ya ukumbi wa vikao vya Bunge.
Tayari Profesa Mwesiga Baregu amemweleza mwandishi wetu kwamba wajumbe wa tume hiyo wanayo matumaini kwamba serikali itaruhusu marekebisho ya baadhi ya vifungu vya muswada huo, ili hatimaye Tume ya Mabadiliko ya Katiba iendelee na shughuli zake hadi katika hatua ya mwisho ya awamu ya pili ya kura ya maoni, kama itakuwapo.
Kwa mujibu wa sheria ya awali ya mabadiliko ya Katiba, Tume ya Mabadiliko ya Katiba inapaswa kuendelea ‘kuishi’ hata baada ya Bunge la Katiba ambalo linaweza kuhitaji ufafanuzi kuhusu kilichomo ndani ya rasimu ya Katiba itakayowasilishwa katika tume hiyo.
Katika muswada wa sasa, inaelezwa kwamba uongozi wa Bunge la Katiba unaweza kumwita Mwenyekiti wa Tume ya Katiba au mjumbe yeyote kutoa ufafanuzi huku Tume hiyo ikiwa tayari imevunjwa, mara baada ya rasimu ya Katiba itakayowasilishwa bungeni kukamilika.
Lakini kinyume cha mapendekezo ya sasa, inashauriwa kama ilivyokuwa katika sheria ya awali, Tume iendelee kuwapo wakati wote wa Bunge la Katiba na wakati wa upigaji kura ya maoni wa awamu ya kwanza na hata awamu ya pili kama utakuwapo na wakati huo huo, Tume iendelee kuwa na jukumu la kutoa elimu kuhusu rasimu ya Katiba husika.
Mvutano ndani ya Tume
Kwa mujibu wa vyanzo vyetu vya habari, katika kikao cha mwanzoni mwa wiki iliyopita kilichoongozwa na Jaji Warioba, Kamishna wa Tume hiyo, Mzee Joseph Butiku aliendeleza msimamo wake wa kujuta akisema kama angejua kutakuwa na uchakachuaji katika mchakato wa Katiba Mpya asiyengekubali uteuzi wa kuwa kamishna.
Butiku anaelezwa kwenda mbali zaidi akisema amekubali uteuzi wa kuwa kamishna wa Tume hiyo si kwa sababu ya shida ya kupata pesa kwani amekwishazoea kuishi maisha ya bila kuwa na pesa, isipokuwa amekubali kuwamo kwenye Tume hiyo ili kujenga, kutetea na kulinda mustakabali bora wa nchi na vizazi vijavyo.
“Ndugu Mwenyekiti, sisi wengine tumeingia humo katika hii Tume si kwa sababu ya kupata pesa kama baadhi ya watu wanavyodhani.
Kwanza tumekwishazoea kwa miaka mingi kuishi bila pesa,” kinaeleza chanzo chetu cha habari kikimnukuu Butiku, ambaye naye anatajwa kuwa tayari kuachia ngazi endapo kusudio la ‘kuchakachua’ mchakato wa Katiba Mpya litaendelezwa kupitia jaribio la muswada wa sasa kuhusu Katiba Mpya.
Lakini pia chanzo chetu hicho kinamnukuu Profesa Mwesiga Baregu naye akitishia kujiuzulu akiamini kwamba kazi nzuri iliyokwishafanywa na Tume inalenga kuchakachuliwa, kwa kuivunja kwanza Tume kabla ya kuanza kwa Bunge la Katiba na kazi ya Tume iwasilishwe na kusimamiwa kwa kutumia chombo kingine ambacho pengine kinaweza kuwa na utiifu wenye lengo la kuvuruga kazi ya kiungwana iliyofanywa na Tume ya Jaji Warioba.
“Mimi niko tayari kujiuzulu endapo hali hii itakuwapo,” Profesa Baregu anatajwa kutamka maneno hayo kwa Jaji Warioba huku Profesa Palamagamba Kabudi akitajwa kupingana wazi wazi na uamuzi wa serikali kupitisha muswada ambao anaamini umejaa udhaifu mkubwa unaoruhusu mchakato wa Katiba Mpya kuingiliwa na kisha kuharibiwa.
Jaji Warioba ahangaika kusaka suluhu
Vyanzo vyetu vya habari serikalini, katika vyama vya siasa na hata Ikulu ya Dar es Salaam vinapasha kwamba Jaji Warioba, amelazimika kuingia katika ‘kibarua’ cha ziada kwa kutafuta suluhu kuhusu suala hilo, na hasa baada ya kuona kile kinachoitwa ‘moto’ wa makamishna katika tume yake. Lengo la jitihada hizo za Warioba zinatajwa kusaka suluhu ili hatimaye mchakato wa Katiba Mpya uendelee kutekelezwa kwa kutanguliza maridhiano na si ubabe.
Taarifa zaidi zinabainisha kwamba kwa kiasi cha kuridhisha, Jaji Warioba, anaweza kufanikisha kuwapo kwa suluhu hiyo, huku Rais Jakaya Kikwete akitajwa kumuunga mkono ‘kimya kimya’ katika juhudi zake hizo za chini kwa chini.
Profesa Baregu avunja ukimya
Katika mazungumzo yake na mwandishi wetu Jumanne wiki hii, Profesa Baregu alisema wajumbe wa Tume ya Katiba wako tayari kujiuzulu mapema zaidi ili kujiondoa katika lawama ambazo zinaweza kujitokeza mbele ya safari, kwamba Tume hiyo haikufanya kazi zake vizuri na kwa weledi.
“Kimsingi, wajumbe wanaamini kasoro hizi zitafanyiwa kazi kwa busara na weledi zaidi ili hatimaye mambo yaweze kwenda vizuri kwa maslahi ya nchi yetu, sote tunaamini Tanzania ni muhimu kuliko mambo mengine. Hata hivyo, kama matarajio hayo ya wajumbe hayatakwenda kama wanavyoamini, basi ni kama tumekwisha kubaliana wote tujiondoe (kujiuzulu),” anasema Profesa Baregu.
Alitaja baadhi ya kasoro zilizomo katika muswada wa sasa wa mchakato wa Katiba kuwa ni pamoja na kuivunja Tume ya Mabadiliko ya Katiba katika wakati mgumu wa kuwapo kwa Bunge la Katiba na pia kuelekea kuwa na kura ya maoni.
Kwa mujibu wa Profesa Baregu, huo ni wakati mgumu ambao Tume inapaswa kuwapo ‘hai’ ili kuweza kufafanua kazi waliyoifanya katika kipindi chote cha kuanza na kuendelea kwa mchakato wa Katiba Mpya.
“Inatia shaka kuweka vifungu vya kutaka Tume ya Katiba ivunje, ‘isiwe hai’ wakati wa Bunge la Katiba halafu unasema tu eti mwenyekiti au mmoja wa wajumbe wa Tume (iliyokwishavunjwa) anaweza kuitwa bungeni kutoa ufafanuzi wa kazi iliyofanywa na Tume nzima,”!
Lakini pia wakati huo huo, unaitaka Tume kutoa elimu ya uraia huku ukiwa na mchakato wa kura ya maoni ambayo inaweza kuwa katika awamu mbili kwa mujibu wa sheria.
Kama awamu ya kwanza ya kura ya maoni itashindwa kuzaa uamuzi, awamu ya pili ya kura ya maoni itaitishwa, wakati huo huo unasema Tume iwe imekwishavunjwa, na kama awamu ya pili itashindikana basi tutarejea katika Katiba ya zamani,”
Vyama vya upinzani vyaongoza upinzani
Wakati hayo yakiendelea ndani ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambako inaelezwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Waziri wa Katiba na Sheria wamekuwa na vikao na Jaji Joseph Warioba, vyama vikuu vya upinzani, CHADEMA chini ya Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, NCCR-Mageuzi chini ya Mwenyekiti wake James Mbatia na CUF-chini ya Mwenyekiti wake Profesa Ibrahim Lipumba, wameanza mikutano ya kumshinikiza Rais Jakaya Kikwete kutosaini Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, uliopitishwa na Bunge mjini Dodoma hivi karibuni.
Viongozi hao wamepanga kuendelea na mikutano ya hadhara katika maeneo mbalimbali ya nchi, ikiwa ni pamoja na kuhamasisha makundi mengine ya kijamii kuungana kuupinga muswada huo.
Hata hivyo, viongozi hao wamekuwa wakitilia mkazo zaidi kipengele cha muswada huo kinachompa nguvu Rais kuteua majina ya watu wanaoweza kuwa wabunge wa Bunge la Katiba, mbali na wabunge wanaotokana na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Baraza la Wawakilishi Zanzibar.
Katika shinikizo lao, viongozi hao wakuu wa upinzani wanataka Rais asipewe uhuru wa kuchagua majina kutoka kwenye orodha ya majina yanayowasilishwa na taasisi mbalimbali kwake na zaidi ya hapo, aondolewe uhuru wa kupuuza majina hayo na kuamua kuchagua majina nje ya orodha hiyo.
Wanataka Rais apelekewe majina yanayojitosheleza kwa mujibu wa idadi inayopaswa na kazi yake iwe ni kutangaza tu majina husika.
Kauli za Mawaziri
Tayari Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe amekaririwa akisema atamshangaa Rais Jakaya Kikwete asipotia saini muswada huo na endapo hatatia saini, basi anaweza kuingia katika mgogoro na wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mbali na Waziri Chikawe, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Uhusiano na Uratibu Steven Wassira, naye ametetea muswada wa sasa na akitoa maneno ya kejeli kwamba safari hii Rais Kikwete hana muda wa kuwaita Ikulu kwa ajili ya mazungumzo ya faragha kama alivyofanya awali, mara baada ya kupitishwa kwa Muswada na hatimaye kuwapo kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba
No comments:
Post a Comment