Thursday, 26 September 2013

Mjane mweupe’ na uvamizi wa Al Shabaab Nairobi

Mtuhumiwa anayesadikika kuwasaidia washambulizi wa Westgate Mall, Bi. Samantha Lewthawaite "Mjane Mweupe"
Mtuhumiwa anayesadikika kuwasaidia washambulizi wa Westgate Mall, Bi. Samantha Lewthawaite “Mjane Mweupe”

JENGO la kibiashara la Westgate jijini Nairobi ni jengo ninalolifahamu vizuri sana. Ndani ya jengo hilo mlikuwa maduka mbalimbali yakiuza vitu vya kila aina — vyakula, sahani, nguo, zana za kielektroniki, madawa, simu za kisasa za mkono na viatu.  Pia mna benki pamoja na mikahawa. 
Binafsi tangu nilipohamia Nairobi mwishoni mwa 2009 nimekuwa na mazoea ya angalau mara moja kwa wiki kwenda kwenye mkahawa maarufu uitwao Artcaffé ulio ndani ya jengo hilo.
Nikipendelea kwenda huko Jumatano usiku ambapo chakula huteremka uzuri zaidi kikisaidiwa na muziki wa jazz ya kisasa. Artcaffé palikuwa mahala pa mtu kuonekana.
Palikuwa hapakosi wafanyabiashara walioinamisha vichwa wakijadili biashara, wanabalozi, mawaziri na wakuu wengine wa serikali ya Kenya, waandishi wa habari wakijipumbaza pamoja na watumishi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na wa asasi zisizo za kiserikali.
Kulikuwa hapakosi warembo wa kila aina waliovaa mavazi ya mitindo ya kisasa.  Mara mojamoja wakishangaza kwa mitindo ya nywele zao.
Mtu wa kwanza kunichukua kwenye mkahawa huyo alikuwa Yusuf Hassan, Mbunge wa jimbo la uchaguzi la Kamukunji. Desemba 7, 2012 Yusuf alijeruhiwa vibaya sana aliporushiwa gruneti na watu wasiojulikana ingawa wengi wanaamini walikuwa magaidi wa Al Shabaab.  Yusuf alishambuliwa usiku baada ya swala ya isha nje ya msikiti uitwao Masjid Hidaya.
Juzi Jumamosi saa za mchana ilikuwa ni zamu ya jengo la Westgate kuvamiwa na magaidi. Miongoni mwa wa mwanzo kushambuliwa walikuwa wateja waliokuwa Artcaffé.
Nilipoziona picha za televisheni za athari ya shambulio la Artcaffé malaika yalinisimama na mwili ulinisisimka. Malaika yalizidi kunisimama na nikaingiwa na uchungu niliposikia kwamba mtu mmoja niliyekuwa nikimjuwa Profesa Kofi Awonoor, mshairi mashuhuri wa Kiafrika aliyewahi kuwa balozi wa Ghana nchini Brazil na katika Umoja wa Mataifa, ni miongoni mwa watu zaidi ya 60 waliouawa mkahawani humo akiwa na mwanawe aliyejeruhiwa.
Siku chache tu kabla ya mwezi wa Ramadhani nilikuwako Artcaffé na mmoja wa wanangu Tahar Rajab aliyekuwa akinitembelea na aliyekuwa pia mwandishi kwenye gazeti la Star la huko Kenya. Tulikuwa tukila chakula cha mchana.
Nakumbuka siku hiyo nilimwambia Tahar kwamba tulikuwa mahala pa hatari, kwamba siku moja magaidi wa Al Shabaab wataushambulia mkahawa huyo, hasa baada ya magaidi hao kuionya Kenya zaidi ya mara moja kwamba iko siku watayashambulia maghorofa ya Nairobi.
Dereva wangu alinikumbusha juzi kwamba niliwahi kumuonya asiwe anaegesha gari kwenye eneo la kuegeshea magari lililo chini ya jengo la Westgate.
Huo ulikuwa ni wimbo niliozoea kumwimbia kila aliyekuwa tayari kuusikia.
Wimbo huo sikuwa nikiuimba peke yangu. Kuna siku mama mmoja wa Kiingereza kwenye hafla nyumbani kwa Balozi wa Uingereza nchini Kenya, alininongoneza kwamba yeye kamwe hendi wala hatokwenda hata dakika moja kwenye mkahawa wa Artcaffé.
Nilipomuuliza kwa nini alinijibu kwamba ni wazi mkahawa huo ni shabaha ya magaidi wa Al Shabaab kwani kila wanachokichukia kilikuwapo hapo: pombe, wanabalozi na watalii kutoka Marekani na Ulaya na watumishi wa Umoja wa Mataifa.
Alichosahau kuongeza au labda alichokuwa hakijui ni kwamba mmiliki wa Artcaffé ni raia wa Israel, aliyewahi kushtumiwa kuwa ni mkabila. Inasemekana kwamba raia wengine wa Israel wanamiliki maduka kadhaa yaliyo katika jengo hilo.
Kwa ufupi, kwa muda mrefu nimekuwa nikihofia kwamba kuna siku mkahawa wa Artcaffé utashambuliwa na magaidi.  Nikiamini kwamba magaidi, hasa wa Al Shabaab, watarusha gruneti kwenye mkahawa huo na kutoroka.
Haikunipitikia kwamba wataingia ndani ya Artcaffé, wakiwa na silaha nzito nzito na kuwatwanga wateja kwa risasi. Wala haikunipitikia kwamba watalishambulia jengo zima likiwa na halaiki ya watu na kuwashika baadhi yao mateka.
Majeshi ya Kenya yaliwanusuru watu wasiopungua elfu moja waliokuwamo ndani ya jengo hilo.
Ni wazi kwamba Polisi wa Kenya walitambua mara baada ya jengo la Westgate kuvamiwa kwamba wavamizi walikuwa magaidi.  Juu ya hayo, hawakukurupuka na kuanza kuwataja kuwa ndio waliohusika.
Ni Al Shabaab, ambao sasa wanaongozwa na Ahmed Abdi Godane (ambaye pia anaitwa Mukhtar Abu Zubayr), waliotoa taarifa kwenye mtandao wa Tweeter kwamba wapiganaji wao wenye umri wa baina ya miaka 20 na 27 ndio waliofanya shambulio hilo.
Orodha walioitoa ya wapiganaji hao inaonyesha kwamba wametoka nchi mbali mbali: Marekani (sita), Sweden (wawili), Urussi (mmoja), Canada (mmoja), Uingereza (mmoja), Finland (mmoja), Kenya (mmoja), Syria (wawili), Somaliland (mmoja) na Somalia (mmoja). Orodha hiyo lakini ilikanushwa na baruapepe moja iliyosema kuwa imetoka kwa Al Shabaab.
Al Shabaab pia walidai kwamba vijana hao waliongozwa na mwanamke, dai ambalo serikali ya Kenya ililikanusha.
Dai hilo lilivusha uvumi kwamba kama ni la kweli basi mwanamke huyo huenda akawa Mwingereza aliyesilimu Samantha Lewthwaite. Mwanamke huyo ambaye kwa umaarufu anajulikana kwa majina ya ‘Mjane mweupe’ na ‘dada mzungu’ alihamia Kenya na wanawe watatu mnamo 2007.
Hata baada ya Al Shabaab kujitambulisha kuwa ndio wavamizi wakuu wa Kenya waliendelea kusisitiza kwamba hawana uhakika ni nani aliyehusika.  Walifanya ndivyo kwa sababu shambulio hilo lina taashira za mtandao mkubwa zaidi kushinda wa Al Shabaab, ule wa Al Qa’eda.
Ninavyofikiri ni kwamba uvamizi huo ulipangwa, kuratibiwa na kuongozwa na Al Qa’eda, kwa niaba ya Al Shabaab. Wavamizi wa Westgate walijiandaa kwa silaha nzito nzito na wanaonyesha kwamba walipata mafunzo ya hali ya juu ya kijeshi kiasi cha kunifanya niamini kwamba walisaidiwa kwa kiwango kikubwa na tawi la Al Qai’da lilioko Yemen ya Kusini.
Hata hivyo, Inspekta-Jenerali wa Polisi ya Kenya, David Kimaiyo, hakukurupuka kama alivyokurupuka Kamishna wa Polisi wa Zanzibar, Mussa Ali Mussa, baada ya Padri Joseph Anselmo Mwang’ambwa kumwagiwa tindikali huko Unguja mjini. Mussa mbiombio aliruka na kuwatuhumu baadhi ya watu askari wake waliokamata kuwa walikuwa njiani kwenda Somalia kujiunga na Al Shabaab.
Jengine alilolifanya Kimaiyo ni kutumia majukwaa ya mawasiliano ya kijamii kama Tweeter na Facebook kuwaarifu Wakenya na ulimwengu, kwa jumla, kuhusu kadhia hiyo ya Westgate.
Huku kwetu mambo yanatokea lakini Polisi wetu wako jii, kimya kabisa. Mara mojamoja huzungumza na waandishi wa habari lakini muda mwingi hatuoni wakifanyalo ila pale wanapowatandika bakora au wanapowafyatulia risasi wale wanaowaona kuwa ni wapinzani wa Serikali.
Kadhalika Kimaiyo hakusita kuomba msaada wa nchi za kigeni ijapokuwa serikali ya Kenya imekuwa ikishikilia kwamba ni Wakenya tu walioingia Westgate kupambana na magaidi.
Ukweli ni kwamba mara tu baada ya uvamizi huo tuliwashuhudia askari wa Polisi ya London (the Metropolitan Police) na makachero wa Scotland Yard wakiwasaidia askari wa Kenya.
Si askari wa Kiingereza peke yao waliowasaidia Wakenya. Makomando kutoka Marekani na Israel nao pia walisaidia. Baadhi yao na wale askari wa Kiingereza tayari walikuwako nchini ambako wamekuwa wakishirikiana na majeshi ya huko kwa muda mrefu kupambana na ugaidi. Na kwa muda sasa jeshi la Israel limekuwa likivipa zana za kivita na ushauri vikosi vya jeshi la Kenya lenye kupigana na Al Shabaab nchini Somalia.
Ahmed Rajab
Chanzo: Raia Mwema

No comments:

Post a Comment