Wauchokonoa Muungano, waukataa
Mmoja ataka uvunjike, mwingine kura ya maoni
Spika wa Bunge, Anne Makinda
Matamshi hayo yalitolewa na wabunge hao kwa nyakati tofauti walipokuwa wakichangia mjadala wa bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha wa 2011/2012, bungeni, mjini hapa jana. Mbunge wa Micheweni (CUF), Haji Khatib Kai, alisema Tanzania ni Jamhuri ya Muungano, ambayo iliunda mataifa mawili yakiwa na lengo la kuunda taifa litakalosimamia maendeleo ya nchi.
Hata hivyo, alisema kinyume cha matarajio hayo, kila siku Wazanzibari wamekuwa wakinanung’unika zaidi kuhusu kubanwa na kero za Muungano, ambazo kila wakati zimekuwa zikizungumzwa bungeni, lakini hadi sasa serikali haijaeleza kama zimetatuliwa au la. "Wakati mwingi Wazanzibari wananung’unika zaidi kuliko Watanzania Bara.
Wazanzibari imefika mahali hawana imani na Muungano huu kwa sababu wao ndio walio nyuma katika maendeleo, lakini ikiangalia Tanzania inasonga mbele," alisema Kai.
Aliongeza: "Kwa hivyo, tunachokisema na tunachokiomba ikiwa serikali hii imeona kwamba Zanzibar imekuwa kikwazo ama imekuwa kero ama mzigo, basi ni vema watuache…narudia tena kusema ikiwa Zanzibar imekuwa mzigo na imekuwa kero, basi hebu tuachieni huo mzigo, uteremsheni kichwani ili muwe huru. La, si hivyo vinginevyo, basi afadhali Muungano huu uvunjwe, uundwe tena iwapo itawezekana.”
Kauli hiyo ilimfanya Spika wa Bunge, Anne Makinda, kuingilia kati na kumtaka mbunge huyo kusubiri mchakato wa kuandika Katiba mpya ili watumie fursa hiyo kutoa maoni yao.
Hata hivyo, kauli hiyo ya Spika Makinda haikufua dafu, kwani Mbunge wa Mgogoni (CUF), Kombo Khamis Kombo, naye aliposimama kuchangia mjadala huo, aliendeleza hoja ya Kai kuhusu kero za Muungano.
Alisema serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina wizara 26, ambazo kati ya hizo, sita ni za Muungano na kusema hali hiyo inamaanisha kwamba, mambo yote, ambayo si ya Muungano, yanapangiwa bajeti ndani ya serikali hiyo.
"Mheshimiwa Spika, tuangalie kutakuwa na usawa gani katika Muungano wetu wa Tanganyika na Zanzibar?" alihoji.
Alisema licha ya kwamba mambo ambayo si ya Muungano yamezungumzwa kwenye Katiba, kimantiki hakuwezi kuwa na usawa katika Muungano kama wizara za Muungano ni sita na wizara zilizokuwa si za Muungano ni 20 na bajeti ni moja.
Kombo alisema kama kweli serikali ya Jamhuri ya Muungano ina nia ya dhati ya kutatua kero zilizomo ndani ya Muungano, anaamini mapendekezo ya JFC (Kamati ya Pamoja ya Fedha) yangelifuatwa kama yalivyo, lakini hayakufuatwa.
Alisema anaamini hakuna ukweli wa dhati wa kutatuliwa kero hizo na kuitaka serikali ikae ikijua kwamba, imewafikisha Wazanzibari kuona kwamba, Serikali ya Muungano wa Tanzania inawadhalilisha.
Kombo alisema kuna wanajeshi, polisi na wafanyakazi wengine Zanzibar, ambao wanatumia huduma visiwani humo, lakini hawalipi kodi kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzinbar (SMZ), badala yake kodi zao zote zinaelekezwa Serikali ya Muungano.
Alisema Serikali ya Muungano imekuwa ni ‘juja wa maajuja’ kwa Wazanzibari kwa kuifanya Zanzibar haina haki wala uwezo wa kuweza kupewa nafasi ya kuitumikia Tanzania nje ya nchi. "Tuangalie mabalozi waliopo.
Zanzibar ina mabalozi wanne tu. Na hawa wote hupangwa katika nchi za Kiarabu, nchi za Kiislamu. Isipokuwa Mheshimiwa Mapuri (Ramadhan Omar) labda kapelekwa China.
Sasa niseme kwamba, Wazanzibari nao wana haki na uwezo katika Muungano huu na wana haki ya kupewa wafanyakazi kufanya katika ofisi za kibalozi,” alisema Kombo.
Alisema kuna kamati, ambazo huundwa mara kwa mara kushughulikia kero za Muungano, ikiwamo Tume ya Jaji Francis Nyalali, ambayo alisema ilikuja na mapendekezo yake, lakini mpaka leo hawajui yalikokwenda.
Kombo alisema pia kuna kamati ya Shellukindo, lakini ripoti yake mpaka leo haijatolewa na pia kuna ya Amina Salum Ali, ambayo hadi leo haijatolewa na kuhoji: "Hivi tuamini kuna kamati gani itaweza kukaa kutatua kero za Muungano?
Kutokana na hali hiyo, alisema haamini kwamba, Serikali ya Muungano ina nia ya dhati ya kutatua kero zilizomo kwenye Muungano, hivyo, akamtaka Waziri Mkuu kusimamia jambo hilo ili lipatiwe ufumbuzi ili Wazanzibari waweze kujenga imani ya dhati.
MWAKILISHI ATAKA KURA YA MAONI
Katika hatua nyingine, Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar jana alishauri Serikali ya Mapinduzi kuitisha kura ya maoni itakayoamua hatma ya Muungano wa Zanzibar na Tanganyika.
Saleh Nassor Juma (Wawi-CUF) alisema kura hiyo itumike kupata maoni iwapo wananchi wa Zanzibar wanataka au hawautaki Muungano.
Saleh alikuwa anachangia makadirio ya bajeti ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar katika Baraza la wawakilishi jana, alisema walio wengi Zanzibar wanatofautiana kuhusu suala la Muungano uliofikiwa baina ya pande hizo mbili mwaka 1964.
Alisema makubaliano ya Muungano yanainyima Zanzibar fursa ya kuongoza taasisi nyeti kama vile Idara za Polisi, Usalama wa Taifa, Jeshi na Bunge.
"Mheshimiwa Spika, iitishwe kura ya maoni haraka … Zanzibar haijawahi kuongoza nafasi ya juu katika vyombo vya ulinzi na usalama," alisema.
Saleh alisema kuwa marekebisho ya 10 ya Katiba ya Zanzibar yameipa Zanzibar hadhi ya kuwa nchi, hivyo pia ni lazima iruhusiwe kujiunga na Jumuiya Afrika Mashariki bila kupitia mgongo wa Serikali ya Muungano.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Katiba na Sheria, Abubakari Khamisi Bakari, alisema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni halali kwa sababu uliridhiwa na wabunge kutoka pande zote za Muungano.
Waziri Abubakari alisema hayo wakati akijibu swali la Mwakilishi, Omar Ali Sheha (CUF) wa Jimbo la Chake Chake, kisiwani Pemba.
Alisema kwamba mkataba wa Muungano uliridhiwa na wabunge wote kutoka Tanzania bara na Zanzibar jambo ambalo linaonyesha uhalali wake.
Alisema kwamba mkataba wa Muungano ulitakiwa kuridhiwa na Bunge na Baraza la Mapinduzi Zanzibar (BLM) taratibu ambazo zimezingatiwa baada ya wabunge kutoka pande mbili za Muungano kuridhia mkataba huo.
Hata hivyo, alisema kwamba jambo lolote linalotumika kwa muda mrefu bila kuhojiwa uhalali wake huwa ni halali kutokana na uwepo wake.
"Muungano ni halali kwa sababu mkataba wa Muungano ulipitishwa na wabunge wakiwemo wa pande zote kwa utaratibu uliowekwa na katiba katika kupitisha mambo ya Muungano," alisema.
Aidha, alisema kwamba mambo yaliyoorodheshwa ya Muungano hivi sasa yamefikia 22 kutoka 11 na sio zaidi ya 30 kama inavyodaiwa na baadhi ya watu.
Hata hivyo, alisema kwamba kwa mujibu wa katiba mambo ya Muungano hayawezi kuongezwa au kupunguzwa hadi ipatikane theluthi mbili ya wabunge kutoka Tanzania Zanzibar na Bara.
Awali, Sheha alitaka kujua taratibu gani za kikatiba zimezingatiwa kabla ya mambo ya Muungano kuongezwa kutoka 11 tangu kufikiwa kwa Muungano huo mwaka 1964.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa (Viti Maalum-CCM), Raya Suleiman Hamad, alisema Muungano wa Tnganyika na Zanzibar umeleta faida kubwa ikiwemo kujenga umoja wa kitaifa kwa wananchi wake "Leo Ndugu zetu wapo Tanzania Bara ukivunjika waende wapi, jambo la msingi ni kurekebisha kasoro za Muungano kwa sababu umeleta faida kubwa kwa wananchi," alisema mwakilishi huyo.
Akifunga Mjadala, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi, alisema Muungano umeleta faida kubwa na tayari kero mbalimbali zimepatiwa ufumbuzi kupitia Kamati ya pamoja ya kujadili kero za Muungano.
Kuhusu utafiti na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia Zanzibar, Balozi Iddi alisema suala hilo haliwezi kutekelezwa kabla ya kufanyika marekebisho ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano na kuwataka Wajumbe wa Baraza hilo kuwa na subira wakati serikali ikiendelea kulitafutia ufumbuzi.
No comments:
Post a Comment