Tuesday, 21 June 2011


Tuchimbeni mafuta yetu

Mwakilishi wa Jimbo la Chonga (CUF), Abdallah Juma Abdallah
SMZ ICHIMBE MAFUTA YAKE HAKUNA KUCHELEWESHA
BAADHI ya wajumbe wa baraza la wawakilishi wamesema wakati umefika kwa wazanzibari kutumia rasilimali zake za asili zilizopo nchini ikiwemo uchimbaji wa mafuta na gesi asilia kwa lengo la kujikomboa kiuchumi.
Wawakilishi hao wameyasema hayo jana wakati wakichangia bajeti ya serikali ya mapato na matumizi ya mwaka wa fedha wa 2011/2012 katika kikao cha baraza la wawakilishi kinachoendelea huko Chukwani Mkoa wa mjini wa magharibi.
Mwakilishi wa Jimbo la Chonga (CUF), Abdallah Juma Abdallah alisema lazima waziri anayehusika na fedha akae na wataalamu wake watafute namna ya kujinasua na kutafuta ulazima wa kutumia rasilimali za nchi na ili wajikomboe.
‘Zanzibar imefika pahala viongozi waone kwamba inahaja ya kutumia rasilimaliz ake mfano hii rasilimali yetu ya gesi na mafuta tulionayo, sasa tuyataumie kwa ajili ya kuwanufaisha wananchi wetu ili tujikomboe kiuchumi’ alisema Abdallah Juma.
Alisema imani yake kwamba kukiwepo uchumbaji wa mafuta basi matatizo mengi yaliopo ya kuondosha umasikini na mambo megine yatakuwa yametatuliwa kwa kuwa mafuta yatakapochimbwa tayasaidia sana wazanzibari kujitatua katika matatizo madogo madogo yote ambayo hivi sasa nchi inashindwa kujiendesha kutokana na ukosefu wa fedha.
‘Mimi naamini asilimia 90 ya matatizo yetu ya ndani yatakuwa tumeshayatatia ufumbuzi kwa ikiwa tutachimba mafuta yetu lakini suala la kuondokana na umasikini kwa wananchi wetu litaondoka kwa kiasi kikubwa’ alisema mwakilishi huyo.
Alisema Tanzania bara ambazo wamechimba gesi kipindi kikubwa bila ya kuomba ruhusa ya mtu ambapo suala hilo halikuwa kwenye kero za mungano imekuwaje lingizwe kwenye kero hivi sasa wakati wote hakukuwa na kero baada ya kusikia Zanzibar wanataka kuchimba mafuta imekuwa ni kero za muungano.
Mwakilishi wa jimbo la Kitope [CCM] Makame Msimba amesema suala la uchimbaji wa mafuta Zanzibar lisiwe na mjadala wowote kwa sasa zaidi ya kuchimbwa kwa kuwa hakuna kitu cha kukisubiri.
‘Suala hili halina mjadala nashangaa kusikia tusubiri taratibu mpaka zitoke kwenye bunge tunasema hatutaki kusikia mambo ya kusubiri tutatuliwe kwanza kwenye kero za muungano …hatutaki….’ alisema huku akishangiriwa na wajumbe wote wa baraza hilo.
Alisema suala hilo la uchimaji wa mafuta na gesi asilia Zanzibar tayari limeshalipitisha ndani ya baraza la wawakilishi na kinachosubiriwa na wawakilishi hao na wananchi wote ni waziri ataeleza katika bajeti hii ametenga fungu gani katika kuliendeleza hilo la uchimbaji wa mafuta na sio vyenginevyo.
Mshimba alisema watu wanaosoma kwa ajili ya suala hili waendelee kusoma lakini bajeti ni lazima iwe na msisimko wa kuliendeleza suala la mafuta lilivyoelezwa katika bajeti.
Akizungumzia suala la mamlaka ya mapato Tanzania [TRA] alisema hakuna sababu ya kubaki hapa Zanzibar kwa kuwa kuna bodi ya ukusanyaji wa fedha hapa Zanzibar ambayo ni ZRB.
‘Tunataka tra iondoke haraka na ibaki ZRB ichukue kila kitu na ule utaratibu wa kudai kwa mkoba pia undoke hii ni dalili ya rushwa’ alisema mwakilishi huyo.
Aidha aliwataka mawaziri wapunguze matumizi yasiyo ya lazima safari zisizo na tija tunataka kila waziri anaekwenda nje aoneshe kile alichokipata ili wazanzibari wote wanufaidike nacho.
‘Hichi kidogo tulichonacho inabidi kiende vizuri fedha nyingi lakini hazifiki kunakokusudiwa, mimi nashauri mawaziri kutumia wigo wa kudhibiti mapato na sio kutumia fedha nyingi tu bila ya kuwanufaisha wananchi’ alisema .
Abdallah naye akizungumzia suala la ushuru mwakilishi huyo ameonesha kusikitishwa kwake na jambo la kutozwa ushuru mara mbili nalo linakera na ni udhalilishaji wa makusudi unaofanywa na mamlaka ya mapato Tanzania {TRA} kwa wazanzibari.
‘Sasa wazanzibar tuliopo hapa tunasema kwa udhalilishaji huu tunoafanyiwa na TRA hatuitaki tena hapa’ alisema mwakilishi huyo ambaye anatoka kisiwani Pemba.
Mussa Ali Hassan alilalamikia wawekezaji wenye kuwadhalilisha wananchi ambao huja kuwekeza na baadae kuwakopa wananchi amabo ni masikini na baadae kukimbia bila ya kulipa fedha za wanachi hao.
Alisema ni vyema kukaribisha wawekezaji wanaoweza kukuza uchumi sio wawekezaji wanaowakopa wananchi na baadae kuondoka na kuwacha wananchi bila ya kuwalipa .
‘Tulitegeemea wao ni watu wa kwanza kuwekeza na kuimarisha uchumi wa nchi yetu utasikia mara nyingi wawekezaji wa hoteli ameshakopa na ameshaondoka na kuwacha wananchi na umaskini..suala hilo lishughulikiwe na hatuhitaji wawekezaji wa aina hiyo’alisema .
Upande wa nafasi za ajira JKU tulitegemea ndio nguvu kazi ya Taifa vijana hawa walitegemea watajifunza mengi na kupata ajira lakini vijana wameanza kuvunjika moyo wa kukosa kuajiriwa mpaka waende JKT na wanakwenda na wakirudi hawana ajira kipindi cha nyuma vijana wakipewa ajira ya jeshini hivi sasa nafasi hiyo imeondoshwa tunaomba nafasi hii irejeshwe JKU .ili waweze kupata ajira.
Vijana wanaomaliza kidatu cha sita wanakosa ajira ni vyema ajira zianze kulingana na elimu mwaka 78 wanajeshi waliokwenda Uganda na walifanikiwa wakiwa na elimu ya darasa la 11 tu hivyo ajira irejeshwe kama hatutoi ajira tutakuwa tunafuga wezi mitaani.
HATUEZI KUJIBU MASWALI YA HAPO KWA HAPO
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imesema bado haijaweza kujibu maswali ya hapo kwa hapoa kupitia baraza la wawakilishi kama inavyofanyika katika vikao vya bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania.
Waziri wa nchi ofisi ya makamu wa pili wa rais Mohammed Aboud Mohammed hayo jana wakati akijibu maswali katika kikao cha baraza kinachoendelea baada ya baadhi ya wajumbe kumtaka makamu pili wa rais kujibu maswali ya papo kwa papo kama ilivyo kwa waziri mkuu Mizengo Pinda katika bunge la jamhuri ya muungano.
Aboud alisema hayo wakati alipokuwa akijibu swali aliloulizwa na mwakilishi wa jimbo la Mpendae (CCM) Mohammed Said Mohammed aliyetaka kujuwa lini utaratibu wa mtendaji mkuu wa shunguli za baraza kujibu maswali ya papo kwa papo utaanzishwa katika baraza la wawakilishi.
Alisema utaratibu huo unahitaji mazingatia makubwa kabla ya kufikia uamuzi wake ili uwe na tija kwa wananchi.
Hata hivyo alisema licha ya kwamba hakuna utaratibu huo wa mkuu wa shunguli za baraza kujibu maswali ya papo kwa papo lakini ni wajibu wa kikatiba kwa wawakilishi kuiuliza maswali serikali.
Aboud alifafanua zaidi na kusema kanuni za baraza la wawakilishi zinatoa fursa kwa wajumbe wa baraza la wawakilishi kuuliza maswali serikali ambapo umetengwa muda wa saa moja na nusu.
Alisema bunge la jamhuri ya muungano limeweka utaratibu huo wa kumuuliza waziri mkuu maswali ya papo kwa papo ambao hutowa ufafanuzi wa masuala mbali mbali.
Kiongozi wa shunguli za baraza la wawakilishi ni makamo wa pili wa rais ambaye hushirikiana na mawaziri katika kujibu na kuyapatia ufafanuzi maswali mbali mbali ya wajumbe wa baraza la wawakilishi wanayouliza.
Alisema kwamba serikali inaamini kwamba utaratibu uliowekwa na baraza la wawakilishi wa maswali na majibu unatosheleza na kutimiza matwakwa ya demokrasi.
Lengo la kuiuliza maswali serikali na takriban katika nchi zote za jumuiya ya madola ni kutaka wajumbe wapatiwe taarifa au kuhimiza serikali kutekeleza jambo Fulani kwa faida ya wananchi.
ZAWA YAPEWA MWAKA MMOJA KUTOA HUDUMA
MAMLAKA ya Maji Zanzibar (ZAWA) imepewa mwaka kuhakikisha suala la upatikajaji wa maji unapatikana na ikishindwa kufanya hivyo basi kazi hiyo wapewe jeshi la kujenga uchumi Tanzania [JWTZ]
Ushauri huo umetolewa na Kamati ya Wenyeviti ya Baraza la Wawakilishi wakati wakitoa maoni yao katika kikao cha baraza la wawakilishi na kutakiwa ZAWA kuimarisha miundo mbinu yake.
Mwenyekiti wa Kamati ya Wenyeviti ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Hamza Hassan Juma, aliyasema hayo jana wakati akiwasilisha maelezo ya Kamati hiyo kwa ajili ya kuchangia hotuba ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2011/2012 kwenye kikao cha Baraza la wawakilishi Zanzibar.
Mamlaka ya maji ipo haja kuikabidhi kazi hiyo kwa vyombo hivyo vya ulinzi, ni moja ya jambo kubwa litaloweza kusaidia kupatikana ufumbuzi wa upatikanaji wa huduma hiyo kutokana na kuonekana Mamlaka husika kushindwa kulipatia ufumbuzi tatizo hilo.
Alisema kupewa kazi hizo kwa vikosi vya ulinzi ni kutokana na watendaji hao kuwa na uwezo mkubwa wa kufanya kazi hizo pamoja na zana za kufanyia kazi.
Mwenyekiti huyo alisema jeshi la kujenga uchumi lina vifaa vya kufanyia kazi na wataalamu wa kumaliza tatizo la maji iwapo watapewa hiyo kazi ya kutengeneza miundombinu ya maji.
Alisema hivi sasa serikali inajiandaa kupandishia wafanyakazi wake mshahara lakini upo uwezekano mkubwa wa nyongeza hiyo isiwanufaishe kutokana na kuishia kununulia madumu ya maji.
Ingawa serikali imeahidi kuchimba visima 52 kwa ajili ya kutatua tatizo hilo lakini kinachojionesha watendaji wa Mamlaka hiyo hawana uwezo wa kulifanyia kazi suala hilo ama wamekuwa wakifanya kwa makusudi kuwakosesha maji wananchi jambo ambalo halitoi sura nzuri kwa wananchi.
Mwenyekiti huyo aliitaka serikali kupitia kwa Makamu wa Pili wa Rais, kuliingilia kati suala hilo kwa kufanya jitihada za ziada ili tatizo la maji limalizike na wananchi wapate huduma ya maji.
Aidha kamati hiyo wameiomba Mamlaka ya maji kufikiria kuigawa mji katika mambloki ili kutatua tatizo la kujaa kwa bloki moja kutokana na hivi sasa kuonekana kulifaidisha eneo moja la Mji mkongwe ambalo limeonekana halikosi kupata maji.
Alisema ipo haja kwa serikali ya Zanzibar kuona haja ya kuandaa sheria ambayo itawawezesha viongozi kutangaza mali zao ikiwa ni hatua ya kuimarisha utawala bora.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa suala la utawala bora ili liweze kuimarika ni vyema serikali ikaandaa sheria na kuipeleka katika Baraza la Wawakilishi itayokuwa inawataka viongozi kutaja mali zao.
Alisema ikiwa viongozi wataweza kutangaza mali zao itakuwa ni jambo la busara kwani wao ndio wanaotakiwa kuwa mfano bora wa kuonesha jinsi walivyopata mali hizo.
Alisema ingawa utekelezaji wa suala hilo linaweza kuwa gumu utekelezaji wake lakini wanalazimika kuufuata utaratibu huo kwani ndio njia pekee itayoweza kujenga utawala bora.
Mwakilishi huyo akiendelea kusoma hotuba yake hiyo alieleza kuwa ipo haja wakati serikali ya Muungano ikiwa inasubiri kulipatia ufumbuzi taizo la mafuta na gesi asilia ni vyema serikali ikafikiria kuanza kazi za kufanya utafiti.
Alisema hilo linalazimika kuanza kufanyiwa kazi kutokana na kupanda kwa gaharma za utafiti ambapo serikali ingeanza sasa ili kutambua kama mafuta hayo yapo na baadae watakaa pamoja kuona nani amlipe mwezake.
Hoja nyengine ambayo Aliieleza Mwenyekiti huyo alisema hali ya upatikanaji wa chakula bado ni ngumu kutokana na ongezeko linalojitokeza na ni vyema Shirika la Biashara la Taifa ZSTC likafikiria kuuza mchele kwani inatabiriwa 2015 mfumko wa bei utaongezeka duniani.
Aidha Mwenyekiti huyo alishauri serikali kuona inaanzisha benki ya kilimo ambazo zitawawezesha wakulima kuzitumia kupata mikopo huku ikiyahimiza mabenki hayo kupunguza riba kwani benki zilizopo nchini zimeshindwa kuwanufaisha wananchi.
Eneo jengine ambalo alilitilia mkazi ni la kuwapatia mikopo makundi mbali mbali ya wajasilia mali ili waweze kunufaika na kupunguza tatizo la umasikini na kuwawekea mazingira bora askari wa JKU ili waweze kutekeleza majukumu yao hasa kwa kuwatumia katika kuinua sekta ya kilimo.
Hata hivyo Kamati hiyo iliipongeza serikali kwa kufanikiwa kukuza sekta mbali mbali ikiwemo ya Elimu na kuomba jitihada hizo ziendelee kuchukuliwa.
Mwakilishi wa Jimbo la Dole, Shawana Bukheit Hassan, akichangia bajeti hiyo aliiomba serikali kuona inasimamia vyema suala la mapato kutokana na kuonekana sehemu kbwa ya mapato kuingia mifukoni kwa watu binafsi.
Aidha Mwakilishi huyo alilalamika utaratibu unaooendelea kutumika katika sekta ya utalii kwa baadhi ya wawekezaji kulipa kila kitu nchini kwao jambo ambalo haliinufaishi nchi kwani hata wanaowahudumia watalii hao wakiwa nchini wanashindwa kulipwa malipo yao kwa wakati.
Nae Mwakilishi wa Jimbo la Kitope, Makame Mshimba Mbarouk, akichangia bajeti hiyo alisema, bado hadhi ya hospitali ya Mnazi mmoja kuwa ya rufaa bado haijafikiwa vizuri kwani hata nguo wanazovaa wafanyakazi wa vyumba vya upasuaji ni mbovu zilizojaa matobo.
Alisema hali ya vifaa haviko katika hali nzuri kiasi ambacho inaweza kutofikia kuiondolea hadhi hospitali hiyo huku madaktari wakiwa katika hali mbaya ya kifedha.
Nae Mwakilishi wa Wete Asaa Othman Hamad, akichangia hotuba hiyo alilalamikia juu ya suala la mafuta kuchelewa kuondolewa katika mambo ya muungano kutokana na hivi sasa bado halijafanyiwa kazi.
Alisema raslimali ya mafuta ndio njia pekee itayoiwezesha Zanzibar kuwa na hali nzuri ya kiuchumi kutokana na kuwa ni raslimali ya msingi katika kukuza pato la taifa.
Nae Mwakilishi wa Ziwani, Rashid Seif Suleiman alisema, ipo haja kwa serikali kulifanyia kazi suala la mafuta kutokana na kuchewa utekelezaji wake ingawa serikali ikiwa tayari imeshalipatia ufumbuzi.
Aidha Mwakilishi huyo alisema ipo haja ya serikali kulifungulia kesi shirika la umeme Tanzania kwa kukaidi amri ya Rais Wa Tanzania iliyowataka kutoitoza Zanzibar gharama ya asilimia 100 ya kuuziwa umeme wakati mikoa mingine imekuwa ikiuziwa chini ya hapo.
Alisema inasikitisha kuona amri ya rais inakiukwa na Shirika hilo kwa kuendelea kufanya hivyo jambo ambalo ni kinyume na sheria na kueleza kuwa serikali ya Zanzibar haipashwi kulionea aibu suala hilo.
Wajumbe wa Baraza la wawakilishi waataendelea tena kuijadili bajeti hiyo leo asubuhi ambapo mjadala huo unatarajiwa kuchukua mda wa siku tatu.

No comments:

Post a Comment