Raia wa India ahukumiwa kunyongwa Dar |
James Magai MAHAKAMA Kuu ya Tanzania katika Kanda ya Dar es Salaam, imemhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa, raia wa India, Vinoth Plavin Nadhesan, baada ya kupatikana na kosa la kuua na baadaye kuuweka ndani ya begi mwili wa marehemu. Hukumu hiyo ilitolewa jana na Jaji Dk Fauz Twaib, baada ya kuridhishwa na ushahidi upande wa mashtaka kuwa, mshtakiwa alitenda kosa hilo kwa kukusudia.Vinoth alikuwa akikabiliwa na shtaka la kumuua kwa makusudi, Abdulbassit Abdallah wa jijini Dar es Salaam na baadaye mwili wake, kuuficha ndani ya begi kabla ya kuutelekeza katika eneo la maegesho ya magari katika jengo la JM Mall. Ilidaiwa kuwa mshtakiwa alimuua marehemu kwa kutumia visu na mishale na kwamba mauaji hayo yalifanyika Februari 6 mwaka 2009, baada ya kumuita nyumbani kwake, katika eneo la Kariakoo, Mtaa wa Kipata. Akisoma hukumu hiyo Jaji Dk. Twaib alitupilia mbali utetezi wa mshtakiwa ulioungwa mkono na hoja za mwisho za wakili wake Majura Magafu aliyekuwa akisaidiana na wakili Irene Maira, kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo wakati akijitetea. Katika utetezi wake, Vinoth alikiri kumuua marehemu, lakini alidai kuwa alilazimika kufanya hivyo, baada ya marehemu kuanza kumshambulia kwa kumpiga fimbo na kwamba hatua hiyo ilikuja baada ya kushindwa kuelewana wakati wakidaiana fedha. Katika majumuisho ya hoja, wakili wake Magafu alidai kuwa ushahidi katika kesi hiyo ulikuwa wa mazingira tu hasa ikizingatiwa kuwa hakuna shahidi aliyemshuhudia mshtakiwa akitenda kosa hilo. Alidai kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo bila kukusudia.Hata hivyo Jaji Dk.Twaib alitupilia mbali utetezi huo na badala yake akakubaliana na hoja za upande wa mashtaka ulioongowa na Wakili wa Serikali, Shadrack Kimaro, akisaidia na Ceciliy Mkonongo kuwa kulingana na mazingira, mshtakiwa alifanya mauaji hayo kwa kudhamiria. Wakili Kimaro alidai kuwa mshtakiwa aliidanganya mahakama kwa kutoa maelezo yalioonyesha kuwa alitenda kosa hilo wakati akijitetea tofauti na maelezo yake ya ungamo . Alidai kuwa katika maelezo yake ya uongo, mbele ya Inspekta wa Polisi Mapunda na maelezo ya ungamo mbele ya mlinzi wa Amani, Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Kariakoo, Judas Kayombo, mshtakiwa alikiri kufanya mauaji hayo. Katika hukumu yake, Jaji Dk Twaib alisema ushahidi wa shahidi mshtakiwa ni ushahidi ulio bora zaidi. Alisema kulingana na ushahidi wa upande wa mashtaka na maelezo hayo ya onyo na ungamo ya mshtakiwa, ameridhika kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo kwa kukusudia. Alisema utetezi wa mshtakiwa kuwa alikuwa akijitetea hauna nguvu.Alisema hata kama alikuwa anajitetea kwa madai kuwa marehemu ndiye aliyeanza kumshambulia, lakini nguvu aliyoitumia katika kujitetea ilizidi kiwango kinachotakiwa kisheria. Katika maelezo yake ya onyo mshtakiwa aliyedai mbele ya Inspekta Mapunda kuwa aliamua kutumia visu viwili kwa sababu havikuwa imara na kwamba alitumia na mishale kwa sababu alitaka kumuua marehemu kwa madai kuwa kama angepona yeye mshtakiwa angekuwa katika wakati mgumu. Akirejea maelezo hayo na maelezo ya mshtakiwa wakati wa akijitetea, Jaji Dk Twaib alisema mazingira yanaonyesha kuwa mshtakiwa alikuwa na nia kutenda kosa la mauaji. "Hivyo ninakubaliana na waungwana wazee mahakama wote watatu kuwa mshtakiwa aliua kwa kukusudia na kwa kuwa adhabu ya kosa la mauaji ya kukusudia kwa mujibu wa sheria ni kifo, basi ninamhukumu mshtakiwa kunyongwa hadi kufa,"alisema Jaji. Katika kujaribu kumnasua mshatakiwa katika kitanzi, wakili Magafu alidai kuwa ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka si wa moja kwa moja bali ni wa kimazingira na kwamba hakuna hata sahahidi mmoja aliyeshuhudia mauaji yakitekelezwa. Mshtakiwa alikamatwa na Polisi Februari 17 mwaka 2008 katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam, akijiandaa kutoroka kwenda kwao India |
No comments:
Post a Comment