Somalia yapata Waziri Mkuu mpya
Rais wa serikali ya mpito ya Somalia amemteuwa Abdiweli Mohamed Ali kuwa waziri mkuu mpya kuchukua nafasi ya waziri mkuu aliyejiuzulu.
Abdiweli Mohamed Ali ni mchumi aliyesomea Marekani na alikuwa waziri wa mipango na ushirikiano wa kimataifa.Mtangulizi wake Mohamed Abdullahi Mohamed alijiuzulu kufuatia makubaliano yaliyofanyika mjini Kampala Uganda yaliyolenga kumaliza mvutano baina ya Rais Sheikh Sharif Sheikh Ahmed na Spika wa bunge Sharif Hassan Sheikh Aden.
Makubaliano yaliyofanyika yaliiongezea serikali ya mpito pamoja na bunge miaka mitatu, na kumtaka Bwana Mohamed ajiuzulu wadhifa wa waziri mkuu, jambo ambalo lilipingwa na raia wengi wa Somalia waliofanya maandamano mjini Mogadishu.
Waziri mkuu mpya Abdiweli Mohamed Ali alisomea chuo kikuu cha Harvard nchini Marekani na aliwahi kuwa mhadhiri wa somo la uchumi katika chuo kikuu mjini New York.
Alijiunga na serikali ya mpito ya Somalia kama naibu waziri mkuu mwaka 2010.
Mwandishi wa BBC Daud Aweis anasema uzoefu wa waziri mkuu huyo mpya katika maswala mbali mbali ya uongozi utaisaidia serikali mpya ya Somalia.
'' Taalum yake pamoja na uzoefu wake kwenye mswala ya maridhiano na uhusiano na nchi za nje zitasaidia shughuli za serikali ya mpito ambazo zimekuwa zikilegalega tangu serikali hiyo kuundwa.''
Wadhifa wake ulimwezesha kusafiri maeneo mengi nje ya mji mkuu Mogadishu, na inatarajiwa atakuwa na ushawishi wa kuipatanisha Somalia na jimbo lililojitenga la Puntland.
Vile vile wengi wanamuelezea kuwa mtu mjasiri aliyeaminika na mwenye msimamo.
Lakini bado atakabiliwa na changamoto za mgawanyiko katika baraza la mawaziri na pia wabunge.
Mwandishi wa Idhaa ya Kisomali ya BBC Younis Nur anasema usalama na matatizo ya kiuchumi yataendelea kuwa changamoto kwa waziri mkuu huyo mpya.
'' Kilichobadilika ni chupa, kinywaji ni kile kile kwa utawala wa Somalia.''
Katika majuma machache yajayo atatarajiwa kuunda baraza jipya la mawaziri na kutoa mpango wake wa kuinusuru Somalia katika kipindi cha miezi 12 ijayo, ambao ndio muda uliobakia wa serikali ya mpito.
Ali anatazamiwa kushauriana na wabunge na viongozi wa koo mbali mbali kabla ya kufanya uteuzi wa baraza la mawaziri.
No comments:
Post a Comment