Friday, 24 June 2011

 HALI YA HEWA YACHAFUKA BARAZANI


Wawakilishi wataka ripoti ya Manispaa
TRA yatwishwa lawama kuhujumu biashara Zanzibar

Na Mwantanga Ame

WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar wamecharuka wakiitaka serikali iiwasilishe ripoti ya uchunguzi ya Baraza la Manispaa pamoja na Mamlaka Mapato Tanzania (TRA) kwani upo uwezekano Mamlaka hiyo inahujumu biashara Zanzibar.

Wajumbe hao walieleza hayo jana walipokuwa wakichangia hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa mwaka wa fedha 2011/2012, iliyowasilishwa jana na Balozi Seif Ali Iddi katika kikao kinachoendelea huko Mbweni nje kidogo ya mji wa Zanzibar.

Wakichangia bajeti ya Ofisi hiyo, baadhi ya Wawakilishi walisema ingawa wameipokea bajeti ya wizara hiyo, lakini wameshangazwa sana kuiona haikugusia ripoti iliyotayarishwa na Madiwani kulichunguza Baraza la Manispaa wakati tayari serikali imeshaipokea.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Jimbo la Kitope, Makame Mshimba Mbarouk alisema wanapaswa kuisikia serikali inasema nini juu ya ripoti ya Manispaa ikiwa ni miongoni mwa hatua za utekelezaji wa utawala bora nchini.

“Tulitarajia Mheshimiwa Makamu katika bajeti yako tungeisikia ripoti, lakini hakuna hata sehemu moja tunaomba waziri akija atueleze maana sisi tulisema hapa tukafikia kukwaruzana na viongozi wetu tusameheane, lakini tunaiomba ripoti ije”, alisema Mshimba.

Aidha, Mwakilishi huyo, pia alieleza ipo haja ya serikali kuifanyia uchunguzi Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kutokana na kuendelea kuwatoza kodi mara mbili wafanyabiashara wa Zanzibar, ambapo huenda ikawa kuna hujuma za kuuwa biashara Zanzibar.

Mwakilishi huyo alifahamisha kuwa serikali inalazimika kuanzisha uchunguzi huo kutokana na kuwepo ukiukwaji wa makubaliano yaliofikiwa katika vikao vya Muungano kwa wafanyakazi wa Mamlaka hiyo kuendelea kuwatoza kodi mara mbili wafanyabiashara wa Zanzibar.

Alisema makubaliano yaliyofikiwa bado utekelezaji wake umo kwenye makaratasi kutokana na kuongezeka vitendo vya kutozwa ushuru mara mbili.

Mshimba alifahamisha kuwa ni vyema kwa serikali ikafikiria kukutana tena na viongozi wa TRA na kuwaelezea juu ya kuendelea vitendo hivyo kwani kinachoonekana bado hawataki kufuata yaliyokubaliwa.

Kutokana na hali hiyo Mwakilishi huyo alipendekeza kwa serikali kama itashindikana kupatikana suluhu ni vyema Mamlaka hiyo ikaondolewa Zanzibar kwani huenda ikawa inahujumu kwa makusudi sekta ya biashara ili kukuza upande wa pili wa Muungano.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe Ismail Jussa Ladhu, alisema serikali inapaswa kuiwasilisha ripoti ya Baraza la Manispaa, ili wajumbe wa Baraza waweze kuitambua kutokana na baadhi yao kutofahamu na kuisoma gazetini.

Aidha, Mwakilishi huyo, alisema ripoti hiyo itapowasilishwa kwao wataweza kuona vipi waisaidie serikali katika kuepusha kutokea matumizi mabaya ya fedha za serikali.

Akizungumzia juu ya hoja ya migogoro ya ardhi, Mwakilishi huyo alisema serikali inapaswa kuona inawawajibisha viongozi wote wanaojitumbukiza katika migogoro ya aina hiyo.

Aidha kuhusu, Kamati ya Fedha ya Pamoja (JFC), alisema ipo haja kwa serikali kuhakikisha ripoti iliyotolewa inafanyiwa kazi kwa haraka kwani hawaoni sababu ya kuwepo ucheleweshaji wakati ikiwa tayari imekamilika.

Mapema Mwenyekiti wa Kamati Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa Hamza Hassan Juma alisema suala la kudumisha Muungano, wao wanaliunga mkono, lakini hawatakuwa tayari kuona mambo ya msingi ya maslahi ya Zanzibar yanakwamishwa kwa makusudi na baadhi ya watendaji wasiotaka kutekeleza matakwa ya Muungano.

“Kwa hili hatuna mzaha hata kidogo kwani wananchi wetu ni maskini sana hali ya maisha kila siku inazidi kuwa ngumu wakati nchi yetu inazo raslimali za kutosha kuwakomboa kwenye umasikini huo, na wametuteuwa sisi kuja kuwatetea maslahi yao”, alisema Hamza.

Mwenyekiti huyo alikosoa hali ya jengo jipya la Baraza la Wawakilishi kutokana na kuanza kuvuja katika baadhi ya maeneo na kuomba iwepo kamati ya wataalamu itayoweza kulishughulikia jengo hilo ili kudumisha hadhi ya jengo hilo.

No comments:

Post a Comment