Tuesday, 8 March 2011

Ziara ya Maalim Seif Ughaibuni: Dunia yaifungulia tena milango Zanzibar
{Habari hii ileletwa kwenu kwa hisani ya Salma Said  na Zanzibar yetu}
  • Asema afya yake sasa ni poa kabisa
  • Kurejea Zanzibar kwa kishindo
Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad (kulia), akifuatilia mkutano wa UNPO, mjini The Hague, Uholanzi, 11 Februari 2011
Ziara ya Makamu wa Kwanza wa Raisi wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, katika mataifa ya Ulaya na Uarabuni, imeelezwa kuwa ya mafanikio makubwa na ya matumaini mema kwa maendeleo ya taifa zima. Hayo yameelezwa na Maalim Seif mwenyewe alipoongea na vyombo mbalimbali vya habari kwa njia ya simu mapema jana, akiwa nchini India, anakoendelea na matibabu.

Makamo huyo wa Kwanza wa Raisa ameelezea kuwa miongoni mwa mafanikio hayo ya ziara yake iliyodumu kwa takriban mwezi mmoja hadi sasa, ni mataifa kama vile Falme za Kiarabu (UAE), Oman na  Ulaya, ikiwamo nchi ya Uholanzi, kuahidi kukuza sio tu uhusiano mwema, bali pia kiwango cha misaada yao kwa Zanzibar.
“Ziara imekuwa ya faraja kubwa na ya matumaini ambayo bila shaka itakuwa ni hatua muhimu kwa maendeleo ya nchi na watu wote,” alisema Maalim Seif.
Ziara hiyo iliyoanzia mwanzoni mwa mwezi uliopita nchini Uholanzi, ilimkutanisha Maalim Seif na viongozi mbalimbali wa dunia, ambapo mjini The Hague alikutana na wajumbe wa Jumuiya ya Watu na Mataifa Wasiowakilishwa katika Umoja wa Mataifa (UNPO), akiwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya miaka 20 ya Jumuiya hiyo.
Zanzibar, kupitia Chama cha Wananchi (CUF), imekuwa mwanachama wa UNPO kwa kipindi cha miaka 20, na Maalim Seif amewahi kuwa raisi wa Jumuiya hiyo kwa vipindi viwili mfululizo.
Hata hivyo, kutokana na sasa chama chake kuwa miongoni mwa vyama vinavyoongoza serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar, CUF, kimsingi, haiwezi tena kuwa mwanachama wa Jumuiya hiyo.
Akiwa nchini Uholanzi, Makamo huyo wa Kwanza wa Rais alikutana pia na watendaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Uholanzi, kuzungumzia haja ya kuendeleza misaada katika sekta mbali mbali, ikiwamo ile ya afya visiwani Zanzibar, ambayo inafadhiliwa sasa na Uholanzi.
Kabla ya kuondoka nchini Uholanzi, ujumbe wa Makamo wa Kwanza wa Rais ulioshirikisha pia watendaji kutoka wizara za Uwezeshaji na Ushirika, Fedha na watendaji wakuu wa sekta mbali mbali nchini, ulitembelea maonyesho maalumu ya kibiashara nchini humo.
Wakiwa katika Falme za Kiarabu, Makamo wa Kwanza wa Rais na ujumbe wake walifanya mazungumzo na wajumbe wa Baraza la Wafanyabiashara na Wazalishaji wa Falme hiyo, ambapo Baraza hilo lilieleza imani kubwa ya kushikamana na Jumuiya ya Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Wazalishaji ya Zanzibar (ZNCCIA) ili kuleta msukumo wa kiuchumi kati ya pande Zanzibar na UAE.
Nchi hizi mbili zina mahusiano ya asili baina yao, ingawa kwa kipindi cha katikati mshikamano wao ulitetereka kutokana na suitafahamu ya kisiasa katika visiwa vya Unguja na Pemba.
Walichoahidi ni kurejea tena kuitambua Zanzibar kama awali kwani kipindi kilichopita cha mizozo wanasema walihofia kuambiwa wanaingia mambo ya nchi za watu”, alifafanua Maalim Seif juu ya msimamo huo wa sasa wa Mataifa ya Falme za Kiarabu, kwa Zanzibar.
Ujumbe wa Zanzibar ulitembelea Mji wa Vyuo Vikuu vya UAE, ambako walipokelewa na kuifungua milango muhimu ya uhusiano wa kitaaluma katika ngazi za elimu ya juu, ambapo fursa imetolewa ya mshikamano baina ya vyuo vikuu nchini na vile vya Uarabuni, zikiwamo ahadi za nafasi za masomo.
Mazungumzo kama haya yalifanyika pia nchini Oman, ambapo milango ya mashirikiano ya siku nyingi baina ya nchi hizi mbili ilifunguliwa tena upya.
Kwa sasa, Makamo wa Kwanza wa Rais yuko nchini kwa ajili ya matibabu, ambako  anaendelea vyema baada ya kufanyiwa upasuaji wa magoti yake mawili.
Walinifanyia uchunguzi na wakasema nifanyiwe upasuaji wa magoti wakaniweka ICU siku moja. Siku ya pili wakataka nifanye mazoezi. Nikatembea kwa miguu yangu na sasa niko vizuri. Alhamdulillahi. Nalazimika kuzidi kufanya mazoezi,” amebainisha Maalim Seif katika mazungumzo yake kwa njia ya simu na Idhaa ya Kiswahili ya Deutsche Welle, Ujerumani.
Maalim Seif ameeleza shukurani zake za dhati kwa wananchi wote waliomuombea dua katika matibabu hayo na safari ya ujumbe wake kwa ujumla.
Alipoulizwa ni lini anatarajia kurejea nchini, Maalim Seif alisema ni
“siku yoyote kuanzia sasa nasubiri na sitaki nije kufikia kitandani bali kuendelea na kazi kama kawaida.”
Wananchi na serikali kwa ujumla, wanamsubiri kwa hamu kubwa kiongozi huyo ambaye amekuwa akileta hamasa kubwa ya utendaji na utekelezaji wa majukumu tangu kuja kwa mfumo wa sasa wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar.

No comments:

Post a Comment