Sunday, 13 March 2011

Watanzania waliotekwa na maharamia waokolewa


Serikali imetuma ndege maalum kwa ajili ya kuwachukua Watanzania 16 waliokuwa miongoni mwa watu 26 waliotekwa na maharamia wa somali wakiwa ndani ya meli.
Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernald Membe alisema jijini Dar es Salaam jana, kwamba Watanzania hao watawasili leo katika Uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Nyerere wakitokea nchini Madagasca.
Waziri Membe alisema meli hiyo iliyokuwa ikitokea nchini kwenda Comoro ilitekwa na maharamia wa somali Oktoba 30, mwaka jana, wakati huo ilikuwa na watu 26 wakiwemo raia wa Tanzania 16, Wacomoro (tisa) na Wamadagasca (wanne).
Alisema mara baada ya kuiteka meli hiyo, maharamia hao wapatao 14 pamoja na mateka walishindwa kuelekea nchini Somalia kutokana na meli kuishiwa mafuta, kitu ambacho kilipelekea kukaa baharini kwa muda wa mwezi mmoja.
Alisema Kutokana na kukaa muda mrefu baharini, mikate na maji walioyokuwa wakitumia ilimalizika na kusababisha maharamia hao kuamuru meli hiyo ipelekwe pwani ya kisiwa cha Madasca ambapo huko walikamatwa mara moja. "Ndani ya meli walimaliza chakula chote pamoja na maji, hawakuwa na njia ya kuishi tena na hivyo waliamua kwenda katika fukwe ya nchi ya Madagasca huko walikamatwa na kufunguliwa kesi," alisema. Watanzania waliokuwa ndani ya meli hiyo wametajwa kuwa wanaume ni 14 na wanawake wawili, ambapo kati ya hao Wazazibari ni wawili.
Membe alisema serikali kupitia Wizara yake iliwasiliana na Serikali ya Madagasca kwa ajili ya kuchukuliwa hatua za kuwarejesha nchini Watanzania hao.
Aidha, waziri Membe alisema mpaka sasa afya za watu hao zimeripotiwa kuwa nzuri na watakapowasili nchini wataruhusiwa kwenda kuungana na familia zao mara moja.

No comments:

Post a Comment