Sunday, 13 March 2011

Shein ashauriwa kupunguza Baraza la mawaziri


Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein, ameshauriwa kupunguza Baraza lake la mawaziri katika serikali ya umoja wa kitaifa (GNU) na watendaji wakuu ili muundo wake ufanane na hali halisi ya uchumi wa Zanzibar.
Ushauri huo umetolewa na Mwenyekiti wa chama cha wakulima (AFP), Soud Said Soud, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mwelekeo wa serikali ya umoja wa kitaifa, mjini Zanzibar jana.
Alisema Baraza la Mawaziri 19 liloundwa baada ya uchaguzi mkuu limekuwa ni mzigo kwa wananchi wa Zanzibar kwa vile halilingani na hali halisi ya uchumi wake.
“Tunamshauri Rais Dk. Ali Mohamed Shein kuvunja baraza la mawaziri na kupunguza idadi haiwezekani Zanzibar kuwa na mawaziri 19 wakiwemo watatu wasiokuwa na Wizara malum,” alisema Mwenyekiti huyo.
Alisema pamoja na uchumi wa Zanzibar kukua kwa asilimia 6.5 haiwezekani serikali kuwa na mawaziri 19 ikilinganishwa na idadi ya wananchi wake wapatao milioni 1.2 Unguja na Pemba.
“Nchi yetu ni ndogo watu wake wapo milioni 1.2 haiwezekani kuongozwa na mawaziri 19 kutoka 13 katika awamu iliyopita,” alisema Mwenyekiti huyo.
Alisema Zanzibar hivi sasa inakabiliwa na tatizo kubwa la mfumuko wa bei za vyakula na ugumu wa maisha tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu Oktoba mwaka jana. Kwa msingi huo alisema kutokana na ukubwa wa muundo wa serikali sehemu kubwa ya mapato ya serikali yanalazimika kutumika kuhudumia viongozi na watendaji wakuu wa serikali ambapo alisema haikuwa mwafaka kwa rais Dk Shein kuongeza wakurugenzi na kufikia 60 katika wizara zake.
Mwenyekiti huyo alisema kutokana na kupanda kwa gharama za maisha chama hicho kinashauri serikali iangalie upya kiwango cha mshahara wa kima cha chini na kuongeza kutoka 100,000 hadi 350,000.
Alisema kiwango kinacholipwa kwa hivi sasa cha kima cha chini hakiwezi kuongeza ufanisi kwa watumishi wa umma kwa vile hakikidhi mahitaji hata ya siku kumi kutokana na mfumko wa bei unaojitokeza katika soko la ndani la Zanzibar.
Aidha, alisema pamoja na wananchi kufarijika na kupatikana kwa serikali ya umoja wa kitaifa, matarajio yao yanaendelea kuzorota kwa kasi kutokana na upatikanaji duni wa huduma za jamii ikiwemo afya na maji kwa wananchi wake.
Alitoa mfano katika kisiwa cha Pemba hivi sasa mwananchi hawezi kupata huduma ya upasuaji bila kuwa na sh. 120,000 jambo ambalo linawaumiza wananchi masikini wenye kipato cha chini.
Soud ambaye alikuwa mgombea wa Urais wa Zanzibar katika uchaguzi uliopita alisema matatizo mengi ya Zanzibar yanachangiwa na kukosekana kwa siasa safi na uongozi bora kutokana na baadhi ya viongozi kuweka mbele maslahi binafsi badala ya kulitumikia taifa na wananchi wake.Hata hivyo, alisema Zanzibar inaweza kupunguza mfumko wa ongezeko la bei kwa kuimarisha uzalishaji wa ndani wa mazao ya kilimo na kusimamia vizuri sekta ya utalii.
Alisema jambo la kusikitisha kuona wakati madereva wa taxi hawana kazi za kufanya kazi za kupokea watalii na kuwatembeza zikifanywa na wazungu waliowekeza sekta hiyo na kufungua maduka ya vinyago kazi ambazo zinapaswa kufanywa na wazawa. Alisema Zanzibar hivi sasa inazalisha asilimia 25 tu mazao ya chakula kutokana na wakulima kutojengewa mazingira mazuri ikiwemo mikopo na pembejeo jambo ambalo alisema linachangia kurejesha nyuma sekta hiyo.
Aidha alisema serikali ya umoja wa kitaifa (GNU) lazima ijenge nguvu za kiuchumi hasa katika uzalishaji wa viwanda vidogo vidogo ili kupunguza tatizo la kushuka kwa thamani ya shilingi na kupunguza mfumko wa bei ambao umeanza kujitokeza visiwani.
Mwenykiti huyo alisema bidhaa muhimu kama mchele, unga wa ngano na sukari zinakabiliwa na mfumko mkubwa wa bei nakuwaathiri wananchi walio wengi Zanzibar kutokan na soko la ndani kuendelea kutegemea bidhaa kutoka nje tangu kuanguka kwa uzalishaji wa ndani ya nchi.
Mchele aina ya mapembe ambao una matumizi makubwa kwa wananchi walio wengi Zanzibar kutoka Thailand na Pakistan unauzwa sh. 1,200 badala ya sh. 800, sukari sh. 1,800 badala ya 1,000 na unga wa ngano shilingi 1,200 badala ya 900 wakati kilo ya nyama sh. 6,000 hadi 7000 tangu kumalizika kwa uchaguzi Oktoba, mwaka jana.
Serikali ya Umoja wa kitaifa ya Zanzibar (GNU), inaundwa na vyama vya CUF na CCM baada ya vyama hivyo kupata uwakilishi katika viti vya majimbo 50 na kuunda serikali hiyo.

No comments:

Post a Comment