Tuesday, 22 March 2011

Watanzania 64,674 wenye VVU wana TB

na Asha Bani
MPANGO wa Tunajali unaosaidia serikali kutoa huduma na tiba katika mikoa mitano nchini umefanikiwa kuwapima kifua kikuu (TB) jumla ya Watanzania 64,674 waliogundulika pia kuathirika na virusi vya ukimwi.
Kwa mujibu wa taarifa za mpango huo kupitia mtandao wake, wanawake wanaoishi na VVU wapatao 42,303 walipimwa TB ikilinganishwa na wanaume 22,571 katika kipindi kilichoishia Desemba mwaka jana.
Mpango wa Tunajali unafadhiliwa na watu wa Marekani kupitia Shirika lake la Misaada la Kimataifa (USAID) unaotekelezwa katika mikoa ya Iringa, Morogoro, Dodoma na Singida.
Mkoani Iringa wilaya ya Njombe ina jumla ya waathirika 21,484 walipimwa TB ambapo ilionyesha kuwa hospitali za shamba la chai la Lugoda wilayani Mufindi na vituo vya wilaya ya Mafinga ndivyo vilivyoongoza kwa kupima wagonjwa wengi zaidi.
“Jumla ya watu 2,864 walipimwa katika kituo cha afya cha Lugoda ambapo 3,353 walipimwa katika hospitali ya wilaya ya Mafinga…
“Mpango wa Tunajali unasaidia hospitali za wilaya na mikoa katika upatikanaji wa huduma bora ikiwemo vifaa kama darubini, usimamizi na ushauri kwa vitendo, ukarabati wa majengo ili kuwezesha hewa safi kuingia katika kliniki za TB na zile zinazotoa huduma ya tiba (CTC),” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, asilimia 50 ya watu wanaoishi na VVU wanaweza kuwa na vijidudu vinavyosababisha TB ambayo hutibika.

No comments:

Post a Comment