Tuesday, 22 March 2011

Lipumba awavaa viongozi CHADEMA

 
Na Benedict Kaguo, Pangani

MWENYEKITI wa Taifa wa Chama cha Wananchi CUF Profesa Ibrahim Lipumba amesema Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) hakina nia thabiti ya
kupambana na ufisadi kutokana kuchochea mgawanyiko wa Watanzania.

Alisema chama chochote cha siasa kilichoshindwa kuthamini matakwa ya wananchi wake hakina nia ya dhati ya kuwaletea ukombozi wa kweli wanaouhitaji Watanzania kwa sasa.

Profesa Lipumba alitoa kauli hiyo wakati akihutubia mkutano wa hadhara katika mji wa Pangani katika mwendelezo wa mikutano ya chama hicho 'kuwazindua Watanzania katika kujenga demokrasia ya kweli hapa nchi'.

Alisema wafanyabiashara wa Chadema hawawezi kuongoza mapambano dhidi ya ufisadi kwa kuwa tayari wako katika mazingira ya kukumbatia rushwa, hivyo ni vigumu wao kuongoza mapambano hayo kama wanavyodai.

“Ndugu zangu wafanyabiashara na wapiga disko wa Chadema wanataka kuwang'oa mapapa ya ufisadi wa CCM ili wao manyangumi ya ufisadi waweze kuingia madarakani, hawana nia thabiti ya kupambana na rushwa,” alisema Profesa Lipumba.

Alisema aliingia kwenye siasa kwa lengo la kuwasaidia Watanzania sio kutafuta sifa kama walivyo baadhi ya wanasiasa wa Chadema.

"Sikuingia kwenye siasa kutafuta sifa, nimeingia kutumia elimu yangu kuwatafutia ukombozi Watanzania wenzangu, sasa hawa Chadema hawawezi kuiondoa CCM kwa kuwa wanachochea mgawanyiko mkubwa ndani ya nchi kwa kuwatukana Wanzanzibari waliokubali Serikali ya Umoja wa Kitaifa,” alisema Profesa Lipumba.

Awali, Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Bw. Julius Mtatiro alisema taifa linaangamia kwa kukosekana uongozi ulio madhubuti sasa ni wakati wa Watanzania kuzinduka ili uchaguzi mkuu ujao waweze kukipa ridhaa chama makini cha CUF.

“Maisha yamekuwa ya kubabaisha huduma za afya hospitalini mama zangu mnatakiwa mwende na nyembe mnapotaka kujifungua, serikali inashindwa kununua wembe lakini wakati wa uchaguzi inaweza kununua kitenge kwa kila mwanamke Tanzania nzima,” alisema Bw. Mtatiro.

Alisema wakati wa mabadiliko ndio huu na wananchi hawana budi kukiunga mkono chama hicho ili kiweze kuongoza mapambano dhidi ya rushwa, matumizi mabaya ya fedha za umma ili kuwakomboa wananchi.

No comments:

Post a Comment