“Uhusiano baina ya Tanzania na Sychelles ni wa kihistoria”
Na Salma Said
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Balozi Seif Ali Iddi ameeleza nia ya Tanzania ya kuendeleza uhusiano wa muda mrefu baina ya Seychelles na Tanzania. Mheshimiwa Makamu wa Pili wa Rais aliyaeleza hayo katika mazungumzo yake na Makamu wa Rais wa Seychelles, Mhe. Danny Faure, huko mjini Victoria.
Alisema uhusiano huo wa nchi mbili hizo ulioanzishwa na viongozi waasisi Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na Mhe. Albert Rene umeweka msingi mzuri wenye faida kubwa kwa nchi hizi.
Mheshimiwa Balozi Iddi alisema mwaliko wake nchini Seychelles, zaidi ya kuhudhuria Tamasha la Kimataifa la Utalii pia unalenga kutafuta mbinu mpya za kuimarisha uhusiano huo yakiwemo masuala ya utalii, biashara na uchumi kwa ujumla.
Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Seychelles Mheshimiwa Danny Faure alisema Seychelles na Tanzania zina agenda moja, hivyo zinapaswa kushirikiana zaidi na kuwa mfano katika kanda hii ya Mashariki ya Afrika.
Alieleza haja ya kushirikiana katika nyanja za uchumi na vita dhidi ya maharamia, wanaoteka nyara meli katika Bahari ya Hindi.
Mapema Mhe. Balozi Iddi alitembelea Kiwanda cha Samaki cha Oceana Fisheries cha Victoria na kuzungumza na uongozi wake juu ya uwezekano wa kuanzisha kiwanda chao Zanzibar.
Naye Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Mama Asha Seif Iddi alikuwa na mazungumzo na mke wa Rais Mstaafu wa Seychlles Mama Sarah Rene.
Katika mazungumzo yao Mama hao walijikita katika masuala ya matatizo ya madawa ya kulevya yanayowakabili watoto wa nchi mbili hizi. Mhe. Mama Asha Seif alisema ni kazi ngumu kuyazuia madawa kwa mara moja kwa kuwa wanao mtandao mkubwa, fedha nyingi na mara nyingi hushirikiana na wakubwa.
Kwa upande wake Mama Rene ambae anaongoza NGO ya kupambana na janga hilo kwa kuelimisha watoto, alimshauri Mhe. Mama Asha kuelimisha watoto wa Zanzibar kwa NGO kama hizo.
Abdulla A. Abdulla
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
No comments:
Post a Comment