Maalim Seif afanyiwa upasuaji wa goti India
Na Salma Said
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ofisi ya makamu wa kwanza wa rais Zanzibar iliyosambazwa kwa vyombo vya habari jana imeeleza kwamba Maalim Seif amefanyiwa upasuaji huo baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kiafya na kupatikana na matatizo hayo ya goti.
Jana asubuhi kulikuwa na uvumi kwamba hali ya Maalim Seif ni mbaya huku wananchi na wafuasi wa Chama Cha Wananchi (CUF) wakiwa khofu kubwa kwamba kiongozi wao anaumwa bila ya kupewa taarifa hali ambayo imezusha minongono mingi miongoni mwa wananchi wa Unguja na Pemba.
Baadhi ya wananchi walikuwa wakipelekeana ujumbe kwa njia ya simu na kuarifiana kwamba hali ya Maalim Seif ni mbaya sana huku akiilamu serikali ya mapinduzi Zanzibar kwa kukaa kimya bila ya kutoa taarifa uhakika juu ya kiongozi huyo ambaye amekwenda India kwa uchunguzi wa afya yake.
“Maalim Seif hivi sasa ni kiongozi wa kiserikali kwa hivyo kwa vyovyote nchi ambayo inaendeshwa kwa uwazi na ukweli na inafuata misingi ya haki lazima iseme ukweli pamoja na kuwa suala la ugonjwa ni siri lakini yeye ni mtu wa watu bwana vipi tunafichwa …hlo haliwezekani” alisema Kijana mmoja ambaye hakupenda kutajwa jina lake gazetini.
Naye Naibu Katibu wa Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Issa Kheri Hussein amewaambia waandishi wa habari n kweli amekuwa akipokea simu kuulizia hali ya Maalim Seif lakini amewatoa khofu wananchi kuwa hali ya Maalim Seif inaendelea vizuri na tayari ameanza kufanyiwa mazoezi madogo madogo hospitalini hapo.
Kheri amesema kwamba Maalim Seif anaendelea kupata matibabu na yupo katika uangalizi mzuri wa madaktari hivyo hakuna sababu ya wananchi kuwa na wasiwasi juu ya ugojwa wake kwa kuwa hali yake hivi sasa inaridhisha kwa kuwa ameshaanza kufanyiwa mazoezi.
“Ni kweli tumekuwa tukipokea simu nyingi kuuliziwa juu ya hali ya Makamu wa kwanza Maalim Seif na wananchi wamekuwa na khofu kubwa lakini tumewasiliana na watu ambao wapo na Maalim huko India na wametwambia kwamba anaendelea vizuri sana na tunachoweza kukisema kwa sasa ni kwamba wananchi wote wazidi kumuombea dua apone haraka na arudi katika afya yake inshaallah”
Maalim Seif yupo nchini India pamoja na Katibu Mkuu wa ofisi ya makamu wa kwanza wa rais, Dk Omar Dadi Shajak na Katibu wake Mohammed Noor ambao walikuwa katika ziara ya kiserikali.
Maalim Seif aliondoka nchini mwezi uliopita iliyopita na kuwa katika ziara ya kiserikali katika nchi mbali mbali ambapo kwa mujibu wa barua ya ratiba ya safari ilieleza kwamba mwisho wa safari zake za kiserikali atapita nchini India kwa uchunguzi wa kiafya.
Baada ya safari hizo za kikazi makamu wa rais alikwenda nchini India kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa afya yake ambapo uchunguzi huo umefanywa katika hospitali ya Apolo Hyderabad jimbo la Andrapradesh na kugundulika kuwa ana matatizo ya goti hali iliyosababisha kufanyiwa upasuaji.
“Matokeo ya uchunguzi huo yalionesha kwamba Makamu wa kwanza wa rais ana matatizo ya kiafya katika mgoti na tatizo hilo lilihitaji kufanyiwa upasuaji mnamo machi 1 mwaka huu, alifanyiwa ubasuaji mdogo wa goti ambapo hivi sasa anaendelea kupata matibabu na akifanya mazoezi na kusubiri goti lirudi katika hali yake ya kawaida kabla ya kurudi nyumbani” ilisema taarifa ya ofisi ya makamu wa kwanza wa rais.
Awali Maalim Seif alikuwa safarini kuanzia Febuari 7 mwaka huu ambapo safari yake ilianzia Uholanzi kwa kushiriki mkutano wa kutimiza miaka ishirini wa kuanzishwa kwa jumuiya ya mataifa ya watu wasio na uwakilishi katika umoja wa mataifa (UNPO) na kuwasilisha mada juu ya maridhiano ya kisiasa ya Zanzibar ambapo yeye mwenyewe aliwahi kuwa mwenyekiti wa jumuiya hiyo.
Akiwa Uholanzi pia alifanya mazungumzo na ujumbe wa wizara ya mambo ya ndani ya nchi hiyo juu ya mashirikiano baina ya Tanzania na Uholanzi
Makamu wa kwanza wa rais katika ziara yake hiyo alitembelea nchini Dubai ambapo pamoja na mambo mengine alikutana na wazanzibari wanaoishi nchi humo pia alipata bahati ya kutembelea maeneo mbali mbali ya kiuchumi katika nchi hiyo.
Safari hiyo ilifuatiwa na safari ya kiserikali nchini Oman ambapo yeye na mawaziri alioandamana nao walionana na mawaziri kadhaa nchini humo na kuzungumza namna ya kuimarisha uhusiano baina ya Oman na Zanzibar.
Katika ziara hiyo alifuatana na waziri wa fedha,chumi na mipango ya maendeleo, Omar Yussuf Mzee, waziri wa biashara, viwanda na masoko, Nassor Mazrui, waziri wa kazi, uwekezaji wananchi kiuchumi na ushirika, Haroun Ali Suleiman pamoja na katibu mkuu wa ofisi ya makamu wa kwanza wa rais, Dk Omar Dadi Shajak.
No comments:
Post a Comment