BAADA ya kutanda hofu ya kusambaa kwa noti mpya bandia na kusababisha jamii kuziogopa, watu wasio waaminifu wameanza kusambaza noti za zamani ambazo ni bandia.
Noti hizo zilikutwa juzi mkoani Rukwa. Polisi mkoani humo wamewakamata wafanyabiashara watano kwa tuhuma za kukutwa na noti hizo za Sh 10,000 zenye thamani ya Sh 370,000.
Kati ya watuhumiwa hao, wapo Masumbuko Madaha (25) na Justine Samike (30) wote wakazi wa kijiji cha Mnyamasi wilayani Mpanda, ambao walikamatwa juzi saa tisa alasiri kwa madai ya kukutwa na noti hizo katika Soko Kuu mjini Mpanda.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Isuto Mantage alithibitisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao na kudai kuwa vijana hao walikuwa katika harakati za kununua nguo za mitumba sokoni hapo.
“Walikutwa na noti 21 zenye thamani ya Sh 210,000 ambazo walitaka kuzitumia kununulia mitumba, ndipo wasamaria wakatoa taarifa kwetu na tukafanikiwa kuwakamata “ alidai Kamanda Mantage.
Watuhumiwa wengine kwa mujibu wa Kamanda Mantage, ni Katabi Lameck (30) na Lameck Michael (18) ambao ni wauzaji wa nguo za mitumba katika Soko Kuu la Mandela katika Manispaa ya Sumbawanga.
Kamanda Mantage alidai kuwa wafanyabiashara hao pia walikamatwa Ijumaa iliyopita mchana kijijini Chala wilayani Nkasi wakiwa na noti 19 za zamani za Sh 10,000 zenye thamani ya Sh 160,000.
Inadaiwa watuhumiwa hao walipohojiwa na polisi, walikiri kusambaza noti hizo kwenye vijiji vya Fyengelezya, Nkundi, Kipande na Kantawa wilayani Nkasi ambako walikuwa wakinunua vitu kwa bei ya chini na kutoa noti hizo bandia na kurudishiwa chenji kwa fedha halali.
Kamanda Mantage alidai kuwa watuhumiwa hao baada ya kufanya uovu Huo, waliondoka kijijini hapo na kurejea mjini hapa kwa kutumia pikipiki ndipo taarifa zilipowafikia polisi ambao walifanya msako na kufanikiwa kuwakamata.
Alifafanua kuwa wakati wa mahojiano kati ya polisi na watuhumiwa hao, walidai walipata noti hizo bandia kutoka kwa John Choka (39), mfanyabiashara na mkazi wa Katalamba jijini hapa ambaye naye amekamatwa na Polisi.
Kwa mujibu wa Kamanda Mantage noti nyingi kati ya hizo zina namba zinazofanana na uchunguzi zaidi unaendelea ili kubaini zinakotengenezwa.

No comments:
Post a Comment