Sunday, 6 March 2011

Muungano hauna sura nzuri-DPP

Na Mwinyi Sadallah
6th March 2011
Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar (DPP), Othman Masoud Othman amesema muundo wa Muungano ulivyo hivi sasa hauleti sura nzuri baada ya Rais wa Zanzibar kuondolewa nafasi ya kuwa makamo wa Rais wa Muungano wa Tanzania kufuatia mabadiliko ya 11 ya katiba.
Hayo ameyaeleza alipokuwa akiwasilisha mada kuhusu mada ya “Mgongano kati ya mapatano ya Muungano na Katiba ya Tanzania,” katika mjadala wa Katiba mpya uliyofanyika jana katika ukumbi wa EACROTANAL mjini hapa.
Alisema marekebisho hayo ya Katiba yalimaliza muungano kwa kuwa Zanzibar ilipoteza mamlaka ya Rais wa Zanzibar katika muundo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati Muungano huo uliotokana na Jamhuri ya watu wa Zanzibar na Tanganyika.
Mkurugenzi huyo alisema kwamba kabla ya mabadiliko hayo, Rais wa Zanzibar alikuwa sehemu ya Muungano na kushiriki katika vikao mbalimbali tofauti na hali ilivyo hivi sasa jambo ambalo halileti sura mzuri katika kuimarisha Muungano.
Alisema pamoja na kuanzisha nafasi ya Makamo wa Rais wa Muungano bado mamlaka aliyopewa kwa mujibu wa Katiba hana mamlaka ya kiutendaji kwa Zanzibar kwa vile si mjumbe wa Baraza la Mawaziri Zanzibar wala sio mtendaji katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).
“Tujiulize Makamo wa Rais wa Muungano ana uhusiano gani na Zanzibar wakati si mjumbe wa Baraza la Mawaziri, hana uhusiano wa kimamlaka ya utendaji na Zanzibar, wala hana uwezo wa kumpa amri hata sheha,” alihoji Mkurugenzi huyo.
Alisema kimsingi, kiungo kilichobaki katika Muungano hakina mamlaka yoyote kwa Zanzibar na kushauri kuna haja ya kufanya mabadiliko ikiwemo kuangalia upya orodha ya mambo ya muungano.
Alisema kwamba hivi sasa mambo ya muungano yakifanyiwa uchambuzi wa kina ni zaidi ya 31 kutoka 11 jambo ambalo alisema linahitaji kuangaliwa wakati wa kuandika Katiba mpya.
Aidha, alisema kumekuwepo na mgongano wa Katiba ya Muungano na Zanzibar katika utungaji wa sheria, akitoa mfano wa Ibara ya 64 ya Katiba ya Muungano ambayo inaruhusu sheria zinazopitishwa na Bunge kutumika Zanzibar wakati Ibara ya 132 (1) ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 inasema sheria zote zinazotungwa na bunge ambazo hazihusiani na mambo ya Muungano ni lazima ziridhiwe na Baraza la Wawakilsihi kabla ya kutumika Zanzibar.
Alisema kwamba pamoja na Bunge kuwa na wabunge 324 bado uwakilishi wa Zanzibar katika chombo hicho bado ni mdogo kwa kuwa bunge lililopita Zanzibar ilikuwa na wabunge 64 tu, na kutahadharisha kuwa idadi isiangaliwe kwa wingi wa watu au ukubwa wa kijiografia Zanzibar, iangaliwe kama ni mataifa mawili yaliyoungana.
Hata hivyo, alisema kwamba pamoja na kasoro hizo Katiba ya Muungano imeweka sharti kuwa huwezi kubadilisha orodha ya mambo ya muungano au kuongeza hadi ipatikane theluthi-mbili ya wabunge kutoka pande mbili za muungano, jambo ambalo alisema linahitaji kuzingatiwa katika mabadiliko yoyote ya Katiba ya Muungano.
Akichambuwa mada ya mkurugenzi wa mashitaka, mwanasheria wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Yahya Hamad Khamis, alisema amefuatilia sana nyaraka za muungano lakini nyingi zimesainiwa na Rais wa kwanza Mwalimu Julius Nyerere bila saini ya Rais wa kwanza wa Zanzibar, Marehemu sheikh Abeid Amani Karume, jambo ambalo linazua maswali mengi juu ya uhalali wa muungano.
“Nimetafuta sana sehemu aliyosaini Rais Karume, sioni saini yake, kama yupo mtu aliyeona atusaidie kwa hilo ili kuondosha utata,” alisema mwanasheria huyo huku akipigiwa makofi na washiriki wa kongamano hilo.
Hata hivyo, alisema muungano upo kinadharia lakini kwa mujibu wa sheria haupo kwa vile ni lazima iangaliwe umekuja vipi na nyaraka zenyewe kutokana na kiongozi mmoja kutoka upande mmoja wa muungano kutoonekana saini yake.
Yahya ambaye ni mwanasheria mkongwe Zanzibar, alisema kwamba upo mgongano wa kikatiba kwa sheria zinazotungwa na Bunge na baadaye kutumika Zanzibar kwa vile ibara ya 64 ya Katiba ya Muungano imeipa uwezo wa kutumika Zanzibar, huku akiunga mkono mtoa mada kuwa mgongano huo ni lazima uangaliwe upya katika kuandika katiba mpya.
Alisema kwamba masuala ya muungano yamekuwa yakiongezeka kinyemela jambo ambalo alisema linahitaji kuangaliwa kwa wakati hasa maeneo yenye kasoro ili yaweze kuangaliwa katika mjadala wa katiba unaotarajiwa kuanza nchini.
Akichangia mada hiyo, Mhandisi kutoka kampuni ya ZANTEL, Ali Khamis alishangaa kwa kusema kuwa matatizo ya muungano yamekuwepo muda mrefu lakini wanasheria Zanzibar wameshindwa kuyachambua na kuyatafutia ufumbuzi kwa mujibu wa sheria.
Naye Mwandishi wa habari Mkongwe Zanzibar, Salim Said Salim, alisema kwamba muungano wa Tanganyika na Zanzibar haukufanyika kwa uwazi, na ndio chanzo cha mkanganyiko katika muungano.
Alisema kuwa aliyekuwa Waziri mkuu wa Zanzibar wakati muungano unaundwa Marehemu Kassim Hanga na mwanasheria mkuu wa Zanzibar wakati huo Jaji Wolfang Dourado hawakushirikishwa ipasavyo katika kuunda muungano.
Hata hivyo, Salim alisema kwamba viongozi na wananchi wengi Tanzania Bara na Zanzibar hawafahamu mambo ya msingi yaliyokuwemo ndani ya Muungano na yasiokuwa ya muungano na kazi hiyo ya kuwaelimisha inahitaji kufanywa na serikali yenyewe ili wananchi waweze kuamua mfumo wa muungano wanaotaka.
Naye Miraji Khamis Kiongwe, alisema wakati umefika mtu anayechaguliwa kuwa kiongozi Zanzibar lazima ajulikane kama Mzanzibari halisi mwenye babu na bibi ili aweze kutetea vizuri maslahi ya Zanzibar.

No comments:

Post a Comment