Monday, 14 March 2011

Loliondo sasa hali shwari


Mchungaji mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ambikile Mwaisapile.

Msongamano wa watu na magari nyumbani kwa Mchungaji mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ambikile Mwaisapile, anayetoa dawa ya magonjwa sugu huko Loliondo wilayani Ngorongoro, Mkoa wa Arusha, umeanza kupungua na kusababisha nauli za magari yanayokwenda huko kupungua.
Aidha, hali hiyo imesababisha gharama za baadhi ya mahitaji muhimu ya binadamu, vikiwemo vyakula kuanza kupungua.
Wakizungumza na NIPASHE, baadhi ya viongozi wa serikali, wasafirishaji na abiria wanaokwenda na kutoka katika eneo hilo, wamesema nauli za mabasi zimepungua kutoka kati ya Sh. 75,000 na 100,000 iliyokuwa inatozwa awali hadi kufikia kati ya Sh. 40,000 na 60,000.
Waliongeza kuwa kwa upande wa magari aina ya Toyota Land-Cruiser yanayoaminika kwa safari za huko pia imepungua kutoka kati ya Sh. 120,000 hadi Sh. 150,000 na kufikia kati ya Sh. 70,000 hadi Sh. 100,000.
Wakizungumzia hali hiyo, baadhi ya wasafirishaji pamoja na kuipongeza serikali kwa kuona umuhimu wa kumsaidia Mchungaji Mwaisapile wamesema kuwa kupungua kwa gharama hizo kumetokana na kupungua kwa muda wa kusubiri matibabu ambapo kwa sasa wagonjwa wana uwezo wa kufika na kupata huduma na kuondoka tofauti na ilivyokuwa awali.
Awali, wagonjwa walikuwa wanalazimika kusubiri kwa zaidi ya wiki moja.
Hata hivyo, wasafisihaji hao akiwemo Idrisa Daudi, Ali Abdallah na Gordian Mwakipesile, wameiomba serikali kuiboresha barabara inayokwenda Loliondo ili iweze kupitika wakati wote na kwa urahisi zaidi.
Walisema kuboreshwa kwa barabara hiyo kutasaidia wananchi wasitozwe gharama kubwa.
Kuhusu kupungua bei ya vyakula, Mwakipesile alisema kuwa bei ya vyakula imeshuka kwa kiwango kikubwa ambapo mguu wa mbuzi uliokuwa ukiuzwa kati ya Sh. 20,000 na 25,000 hivi sasa unauzwa kati ya Sh. 15,000 hadi 18,000 wakati mkono wa mbuzi unauzwa kwa Sh. 10,000 badala ya Sh. 15,000 za awali.
Kwa upande wa maji chupa ya Kilimanjaro iliyokuwa inauzwa kati ya Sh. 2,500 na 3,000 hivi sasa inauzwa kwa bei ya kawaida ya Sh. 1,000.
Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Elias Wawalali, amethibitisha kuanza kupungua kwa msongamano wa watu nyumbani kwa Mchungaji Mwaisapila.
Wawalali alisema msongamano huo umepungua kutokana na jitihada za serikali kuweka utaratibu mzuri wa kumwezesha Mchungaji Mwaisapile kutoa huduma bila kubughudhiwa.
Hata hivyo, Wawalali alisema kuwa bado wananchi wanaendelea kumiminika kwa mchungaji huyo hata nyakati za usiku.
Aliwataka wananchi wanaokwenda kupata tiba hiyo wazingatie taratibu zilizowekwa ili wapate matibabu kwa urahisi.
WAGENI KUTOKA NJE
Katika hatua nyingine, wasafirishaji hao wameiomba serikali kufuatilia watu wanaotoka nje ya nchi kwenda kwa mchungaji huyo kwa kuwa huenda baadhi yao hawafuati sheria na taratibu za kuingia nchini.
Wasafirishaji hao walisema kuwa wanaposafirisha abiria kwenda eneo hilo, wameshuhudia makundi ya watu kutoka nchi jirani ambao sio rahisi kujua kama wanatoka nje ya nchi.
Wakati wananchi wakianza kufurahia kupungua kwa nauli, baadhi ya watu wengine wakiwemo wapigadebe na madalali wa tiketi za magari yanayokwenda Loliondo, wamesema hali hiyo imeanza kuwaathiri kimapato kwa kuwa kipato chao kimeanza kupungua.
Baada ya kugundulika kwa dawa inayodaiwa kutibu magonjwa sugu huko Loliondo, maelfu ya watu kutoka nje na ndani yalianza kumiminika kwenda Loliondo kupata tiba.
Hali hiyo iliwafanya wasafirishaji kupandisha nauli zaidi ya mara mbili ya nauli ya kawaida ambapo ilimlazimu mtu kulipa Sh. 150,000 kutoka Arusha kwenda Loliondo na kurudi.

No comments:

Post a Comment