Friday, 4 March 2011

Gaddafi sharti ang'atuke, asema Obama

Waasi mjini Benghazi
Huku hali nchini Libya ikitajwa kuendelea kuzorota, Jamii ya kimataifa imeendelea kumtaka kiongozi wake Kanali Muammar Gaddafi kuachia ngazi.
Rais Barrack Obama wa Marekani amesema kwamba Marekani huenda ikachukua hatua ambazo bado hajazitaja kumshurutisha Rais Ghaddafi kujiuzulu.
Naye Rais Dmitriy Medvedev wa Urusi ameonya kwamba huenda Libya ikakumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe ikiwa hatua za dharura hazitachukuliwa kurekebisha hali ilivyo nchini humo.
Rais Obama alikuwa akizungumza na waandishi wa habari katika ikulu ya White House ambapo alimtaka Rais Ghaddafi kung'atuka malakani mara moja.
Rais Obama pia ameonya kwamba wale wanaotekeleza mashabulizi dhidi ya raia nchii Libya watawajibika kwa makosa hayo.
Wakati huo huo Marekani sasa inatoa msaada wa moja kwa moja kusaidia wakimbizi kutoka Libya kurejea makwao. Rais Obama amearifu kwamba ametoa idhini ya kutumika kwa ndege za kijeshi za Marekani kurejesha raia wa Misri waliotorokea Tunisia kufuatia mapigano makali ambayo yamezuka kati ya wafuasi wa Rais Ghaddafi na vikundi vinayomtaka kujiuzulu.
Shirika la kutoa misaada la Marekani USAID pia limetuma maafisa katika mipaka ya Libya ili kushirikiana na wale wa Umoja wa Mataifa na mashirika mengine yasio ya kiserekali katika kutoa msaada kwa waathiriwa wa mapigano hayo.
Huku haya yakiarifiwa, mejeshi yanayomuunga mkono Rais Ghaddafi yemetekeleza mashambulizi mapya ya anga katika mji wa Brega wenye visima vya mafuta na ambao umetekwa na wapinzani wa Rais huyo. Hakuna majeruhi yalioripotiwa kufikia sasa.

No comments:

Post a Comment