Wanajeshi watembeza kipigo Gongo la Mboto
Baadhi ya wananchi wanaodai kupigwa na askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) eneo la Gongo la Mboto, wakiwa katika kambi ya kupokelea misaada kituo cha Mombasa Ukonga, jijini Dar es Salaam. (Picha: Mpigapicha Wetu)
Wakati simanzi zikiwa bado zimetanda miongoni mwa wakazi wa Gongo la Mboto ambao wengi wao wamefiwa, kujeruhiwa na wengine kupotelewa na mali kutokana na milipuko ya mabomu, baadhi ya wakazi waishio eneo hilo hilo, wamepigwa na kujeruhiwa vibaya na baadhi ya kikundi kinachodhaniwa kuwa ni cha wanajeshi.
Wakizungumza na waandishi wa habari jana, huku wakiwa na majeraha makubwa sehemu mbalimbali ya miili yao, baadhi ya wananchi waliopigwa, walisema tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia jana eneo la Gongo la Mboto Msikitini baada ya kuvamiwa na kikundi kinachokadiriwa kuwa na watu 30 wakiwa wamevalia sare za jeshi.
Walisema juzi majira ya saa 6:00 usiku walishangaa kuona kundi kubwa la watu wakiwa wamevalia sare za jeshi na walianza kuwapiga wakitumia mikanda ya sare zao na fimbo zilizofanana na nyaya za umeme.
“Juzi majira ya saa sita usiku tulishangaa kuvamiwa na kundi kubwa la watu waliokuwa wamevalia sare za jeshi, na kuanza kutupiga na mikanda ya sare zao, mateke pamoja na fimbo zilizofanana na kamba za umeme huku wakiwa hawaongei chochote,” alisema Rashid Abdallah, mmoja wa waliopigwa.
Alisema mbali na kupigwa, kikundi hicho pia kiendelea kuvunjavunja vibanda vya chips mbalimbali vya wakazi hao pamoja na kunyang’anya vitu mbalimbali zikiwemo fedha.
“Mimi walipokuja kwangu wakawa wanaambizana wenyewe kwa wenyewe, piga huyu nikawaambia wasinipige mimi ni mlinzi, lakini wakasema hawana habari na mlinzi wala mtu yeyote wenyewe wanapiga tu,” alisema Kasimu Mwangosa, mlinzi wa soko la Gongo la Mboto.
Mada Maugo, Bondia wa ngumi ambaye pia alikuwemo katika mkasa huo, alisema japo kuwa hakuwafahamu kwa majina wanajeshi hao, lakini alisema sura zao sio ngeni na kwamba baadhi yao wanaoishi katika kambi ya Gongo la Mboto.
Aidha, Maugo alisema baada ya kupigwa, walilipoti kituo cha polisi, na kuelezwa na polisi kuwa watalifanyia kazi.
Mkuu wa Wilaya wa Ilala, Leomidas Gama, alipoulizwa, alisema yeye sio mzungumzaji.
Mwandishi wetu alifika katika kambi ya JWTZ Gongo la Mboto kuonana na Mkuu wa kikosi, lakini alizuiliwa kuingia ndani.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, Sada Juma, alisema jana kuwa wakazi hao walishambuliwa na kupigwa na kujeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili.
Alisema baada ya watu hao kuwajeruhi, walikimbia na kwenda kusikojulikana na kwamba hadi sasa wanaendelea kuwatafuta.
Hata hivyo, alipoulizwa kama watu hao ni askari au la, Sada alisema bado hawajafahamu hilo kwa sababu kwa mujibu wa wananchi hao, watu hao walikuwa wamevaa nguo za kiraia.
“Tunaendelea na uchunguzi, hatuwezi kusema kama watu hawa ni askari kama baadhi yao wanavyodai, tunaomba mvute subira wakati upelelezi ukiendelea,” alisema.
Kamanda Sara alisema tayari watu hao wameshafungua kesi katika kituo cha Stakishari na kufunguliwa jalada namba 3030/25/2011 ambalo kwa sasa limehamishiwa kituo cha Gongo la Mboto.
Alisema katika tukio hilo jumla ya watu wanane wamejeruhiwa sehemu mbalimbali mwilini ikiwemo kichwa na kifuani.
MISAADA ZAIDI YATOLEWA
Wakati huo huo, makundi mbalimbali, makampuni na mashirika wameendelea kutoa misaada mbalimbali kwa waathirika wa mabomu.
Wakitoa misaada hiyo mbele ya Kaimu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki, wawakilishi kutoka makundi hayo walisema wameguswa kutoa ili kuwasaidia kupunguza ugumu wa maisha kwa waathirika hao.
Misaada hiyo ni vyakula, nguo na magodoro.
Baadhi ya vyakula vilivyotolewa jana ni pamoja na mchele, unga, sukari, maharage, mafuta ya kupikia, sabuni, maji na juisi.
Kati ya watu waliojitokeza katika kutoa misaada hiyo ni pamoja na Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salam, Alhadi Mussa.
Wengine ni Benki ya Ecobank, Chama cha Waimbaji wa Nyimbo za Injili Tanzania pamoja kampuni ya Cocacola.
JWTZ YAZUNGUMZIA YA MBAGALA
Katika hatua nyingine, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) liliomba wataalamu kutoka Marekani kuja kusaidia kufanya uchunguzi wa tukio la milipuko ya mwaka 2009 huko Mbagala.
Taarifa ya Kurugenzi ya Habari na Uhusiano, Makao Makuu ya Jeshi katika taarifa yake jana, ilisema pamoja na uchunguzi wa mabomu ya Mbagala, wataalamu hao walifanya ukaguzi wa maghala mengine nchini ambapo walibaini milipuko ya Jeshi kuwa katika mpangilio unaokubalika kiusalama.
Ilieleza kuwa katika uchunguzi huo hawakuweza kubaini nini hasa chanzo cha milipuko hiyo na kwa hali hiyo chanzo kilibakia kuwa makosa ya watendaji waliokuwa ndani ya ghala.
Hata hivyo, taarifa hiyo ilifafanua kuwa wataalamu hao walishauri baadhi ya milipuko ihamishwe kutoka Dar es Salaam na kupelekwa katika maghala mengine mikoani, na milipuko ile iliyopitiliza muda wake iharibiwe ili isizuie nafasi au kuongeza uzito wa milipuko katika ghala.
Taarifa ilisema kuwa kazi ya kuhamisha baadhi ya milipuko hiyo ilikwisha kufanyika na milipuko iliyopitiliza muda wake iliharibiwa.
Ilisema baada ya milipuko ya Gongo la Mboto Februari 16, 2011, JWTZ iliwaomba tena Wamarekani waje nchini kusaidia uchunguzi wa tukio hilo na tayari maofisa sita kutoka Jeshi la Marekani waliobobea katika masuala ya milipuko waliwasili nchini Februari 23 na 24 kusaidia uchunguzi huo.
Ilisema uchunguzi wa wataalamu hao utakwenda sambamba na ule wa tume iliyoundwa na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi.
Aidha, JWTZ ilisema mabomu 2,094 yameokotwa hadi sasa na Kikosi Kazi kilichoundwa na vyombo vya Ulinzi na Usalama kwa ajili ya kukusanya mabomu kwenye maeneo yaliyoathiriwa na milipuko ya mabomu hayo.
Taarifa ilifafanua kwamba, kikosi kazi kinapata changamoto ikiwamo ile ya kutokuwa na mhusika maalumu wa kuonyesha yalipo mabomu.
Taarifa ilisema kuwa mara kwa mara kikosi kazi kimekuwa kikipewa taarifa ya mabomu bila watu hao kujua kama yapo au yameshachukuliwa.
“Kwa kuwa hali hii imesababisha upotevu wa muda na usumbufu kwa kikosi kazi, JWTZ linawatangazia wananchi wote waliofikiwa na mabomu, wapeleke taarifa kwa viongozi wa Kata ambao nao wataziwasilisha katika vituo vya Polisi au JWTZ.
“Viongozi wa kata ndio watakaochukua dhamana ya kukiongoza kikosi kazi kuyaokota,” ilisema.
JWTZ ilisisitiza kuyatolea taarifa mabomu wanapoyaona na kamwe wasiyaguse au kuyachukua kwa ajili ya kuyauza kama vyuma chakavu kwani ni hatari kwa maisha yao.
APHTHA WAPINGA TUHUMA
Wakati huo huo, Chama cha watoa Huduma Binafsi za Afya nchini (APHTHA), kimekanusha taarifa iliyoripotiwa kwenye vyombo vya habari kuwa hawakushiriki kutoa huduma yoyote ya matibabu kwa wajeruhi wa milipuko ya mabomu iliyotokea Gongo la Mboto.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Meneja wa Mradi wa APHTHA, Dk. Samwel Ogillo, alisema walipokea taarifa hiyo kwa masikito makubwa na kukanusha vikali taarifa hiyo na kusema kuwa kuna baadhi ya hospitali binafsi zilishiriki kutoa msaada wa matibabu kwa majeruhi walioumia na mabomu.
Alisema siku ambayo Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ulinzi na Mambo ya Nje ilipotembelea eneo la Gongo la Mboto, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk. Judith Kahama, alisoma taarifa ambayo ilizitaja hospitali mbili za binafsi ambazo ni TMJ na Hindu Mandal kuwa ndizo zilishiriki kutoa huduma ya matibabu.
Alifafanua kuwa baada ya tukio la milipuko ya mabomu la Gongo la Mboto hakuna mwanachama yoyote wa APHTHA aliyepokea taarifa rasmi ya kuomba msaada kutoka kwenye hospitali za Manispaa ya jiji la Dar es Salaam za kuwaomba kwenda kutoa msaada na kusema kuwa hospitali zisizopungua tatu za binafsi zilishiriki katika zoezi la kuwahuduma wagonjwa.
Hata hivyo, Ogillo alisema licha ya kutopata taarifa za kuombwa msaada, lakini hospitali binafsi zilizoshiriki pia kutoa msaada ni Hindu Mandal, TMJ, Marie Stopes na Hubert Kairuki walikuwa wanajiandaa kuelekea eneo la tukio, lakini baada ya muda walijulishwa kuwa hali ni shwari.
“Sisi APHTHA hatukupata taarifa rasmi ya kombwa kwenda kutoa msaada siku ya tukio, lakini wenzetu watatu walishiriki kuwahuduma wagonjwa, lakini leo hii tunaambiwa hospitali binafsi hazikushiri kutoa huduma tunaomba watu wachache wasipotoshe umma kwani tumekuwa na mahusiano mazuri na serikali tangu mwaka 1991,” alisema Ogillo.
Imeandikwa na Raphael Kibiriti, Eliwinjuka Shani, Elizabeth Zaya na Romana Mallya.
No comments:
Post a Comment