| Maisha Dar mashakani |
| *Maji ya Bandia yafumwa madukani Na Waandishi Wetu, jijini MAISHA ya Watanzania yanazidi kuwekwa hatarini baada ya maji ya bandia yenye nembo ya Mtera Sclach kukamatwa na maofisa wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) yakiwa yamezagaa mitaani na kuuzwa kiholela. Maji hayo yanadaiwa kuwa yalikutwa yakisambazwa kwenye maduka mbalimbali ambapo yalikuwa na ujazo wa lita 12. Kwa mujibu wa mkaguzi ambaye pia ni Meneja wa TFDA, Agnes Kijo, baada ya ukaguzi walibaini kuwa maji hayo hayakidhi viwango vya ubora. Amesema mbali na kutokidhi viwango, pia msambazaji wa maji hayo alikutwa hana leseni inayomruhusu kufanya biashara hiyo wala ya bidhaa za chakula kutoka TFDA. Kutokana na kuwapo kwa hali hiyo, wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wapo hatarini kukumbwa na magonjwa mbalimbali kutokana na utumiaji wa maji ya chupa yasiyokidhi viwango. Wakizungumza na Dar Leo, baadhi ya wakazi wamedai kuwa ili kuondokana na kero hiyo umefika wakati wakaguzi kutoka TFDA kushirikiana na wananchi hata kwa kutoa zawadi kwa mwananchi yeyote atakayetoa siri za kuwapo kwa kiwanda ama mtu binafsi anayetengeneza vyakula bila ya kuwa na leseni. “Tuna imani kuwa kama wahusika wakitangaza kuwapo kwa zawadi, siri nyingi zitafuchuka na wahusika kuchukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani,” alisema Atuganile Isaya, mkazi wa Keko Magurumbasi. Mkazi wa Ukonga, Rajabu Hamisi, amesema wakaguzi hao wanapaswa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye maduka ili waweze kuwabaini wahusika. Hata hivyo, mkaguzi huyo amewashauri wananchi kuwa makini na utumiaji wa maji ya chupa ili kuepuka kukumbwa na magonjwa mbalimbali. Amesema mamlaka hiyo ipo katika operesheni ya ukaguzi wa bidhaa mbalimbali ili kuweza kuwabini wahusika na kuvifungia viwanda vitakavyokutwa vikiendeshwa bila ya kufuata sheria. |
No comments:
Post a Comment