Hatuwezi kuorodhesha majanga yote yaliyotokea katika nchi yetu katika kipindi hicho cha miaka miwili kwa sababu majanga hayo yalikuwa mengi na wananchi wote walikuwa mashahidi wa majanga hayo. Hapa tunazungumzia pia majanga yaliyotokana na ajali za barabarani, moto, ajali za majini, reli, anga na nyinginezo. Ni ajali zilizotuachia majonzi kama taifa. Kama tulivyoshuhudia katika janga la mabomu ya Gongo la Mboto wiki iliyopita, majanga hayo yalituachia watoto yatima, wajane, walemavu wa viungo, vipofu na familia zilizosambaratika. Lakini somo kubwa tulilojifunza ni kuwa majanga mengi yalitokana na serikali yetu kutowajibika kwa kushindwa kusimamia vizuri sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa katika uendeshaji wa mambo mbalimbali. Ni bahati mbaya kuwa badala ya kuendesha shughuli za kiserikali, kibiashara na kijamii kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa na mamlaka zinazotambuliwa kisheria na kikatiba, siasa ndio imekuwa dira ya kuongoza kila sekta na wanasiasa ndio wamekuwa vinara wa kuhubiri yale wasiyoyatekeleza na kuwa chimbuko la kuporomoka kwa maadili katika serikali na sekta mbalimbali. Ndio maana tunadiriki kusema kuwa viongozi ni chanzo kikubwa cha majanga yanayotokea katika nchi yetu. Kwa kutanguliza siasa, kwa mfano, angalia jinsi watendaji serikalini wanavyoangalia sheria za barabarani zikikiukwa mchana kweupe pasipo kuchukua hatua. Angalia jinsi nyumba zinavyoota kama uyoga katika miji yetu licha ya kuwapo mipango miji na watendaji lukuki wenye dhima ya kusimamia mipango na ramani za miji hiyo. Angalia jinsi watu wanavyovamia na kujenga katika hifadhi za barabara na serikali inavyowaonea muhali ili wasiinyime kura wakati wa chaguzi mbalimbali. Ni kwa sababu hiyo Tanzania limekuwa taifa la majanga. Na Watanzania tutegemee majanga zaidi katika siku sio nyingi kuanzia sasa. Angalia jinsi majanga lukuki yanavyosubiri kutokea katika sehemu nyingi za nchi yetu, hasa mijini. Ebu tuangalie Jiji la Dar es Salaam, kwa mfano, ambalo kwa miaka nyingi limekuwa mtaji mkubwa wa wanasiasa katika kutawala nchi yetu. Serikali imeacha kila mtu afanye atakavyo na hali hiyo ndio itakuwa chimbuko la majanga mengi tunayodhani yatatokea muda sio mrefu kuanzia sasa. Katika Daraja la Ubungo, kwa mfano, tujitayarishe sasa kushuhudia janga kubwa zaidi ya majanga ya mabomu ya Mbagala na Gongo la Mboto likitokea. Uvamizi wa kutisha wa maelfu ya Machinga wanaofanya biashara katika daraja hilo, bila kujali msongamano wa watu na magari yanayosafirisha abiria wa jijini na mikoani, matrela ya kusafirisha mafuta ya kulipuka, nyaya za umeme mkubwa zinazopita juu ya vichwa vyao, mitambo ya Kampuni ya Umeme ya Songas na kituo cha mafuta vilivyo karibu sana na eneo hilo, ni vyanzo vya majanga yanayosubiri wakati tu. Angalia biashara zinazofanyika kandokando ya barabara sehemu za Manzese, Tegeta, Tandika Sokoni, Buguruni, Banana, Soko la Ilala, Mbezi Mwisho, Mzunguko wa Mtaa wa Msimbazi, Mahakama ya Ndizi Mabibo, na kadhalika. Huko mikoani miji mingi inayo maeneo ambayo wafanyabiashara wamevamia barabara kama vile hakuna halmashauri za miji au mamlaka za Serikali Kuu. Sisi tunadhani kuwa kwa vile mamlaka husika zimetanguliza siasa badala ya kusimamia kanuni, sheria na taratibu zilizowekwa ili kuepusha majanga yanayowaangamiza Watanzania kila kukicha, pengine Kamati ya Bunge inayosimamia masuala ya ulinzi na usalama, chini ya Mwenyekiti wake, Edward Lowassa iingilie kati ili itunusuru na majanga hayo yanayosubiri kutokea. |
Kheri yote inapatikana pale Mwenyezi Mungu anaporidhika na mja wake, na funguo za kheri zimo katika Dua pamoja na unyenyekevu kwa Mwenyezi Mungu na kuonesha kumpenda kwa kutenda yale yanayomridhisha na pia kumuogopa kwa kuepukana na makatazo yake. Mja anapokabidhiwa na Mola wake funguo hizi basi ajue kuwa Mola wake anamtakia kheri, na anaponyimwa basi ajue kuwa amefungiwa milango ya kheri
Tuesday, 22 February 2011
Serikali sasa ichukue hadhari kuepusha majanga
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment