Friday, 25 February 2011


 Mchoma Qur-aan Apelekwa Chuo Cha Mafunzo



Na Salma Said Zanzibar
RAMADHANI Handa Tuma (28) Mkaazi wa Mombasa wilaya ya magharibi Unguja, aliyekuwa akituhumiwa kwa kosa la kuchoma moto msahafu pamoja na juzuu za dini ya kiislamu amehukumiwa kutumikia chuo cha mafunzo kwa muda wa miezi 24 pamoja na na adhabu hiyo mshtakiwa huyo ametakiwa kulipa faini ya fedha taslim shilingi 200,000.
Adhabu hizo zimetolewa na Hakimu Khamis Ali Simai wa mahakama ya wilaya ya Mwanakwerekwe Mjini Zanzibar, aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo, baada ya kumtia hatiani dhidi ya mashitaka ya kufanya kitendo kinachoweza kuleta uvunjifu wa amani pamoja na kukashifu dini makosa ambayo yalikuwa yakimkabili mahakamani hapo.
Akifafanua adhabu hizo, Hakimu Khamis alisema kuwa shitaka la kwanza la kufanya kitendo kinachoweza kuleta uvunjifu wa amani atalipa faini ya shilingi laki mbili (200,000) na endapo atashindwa atatumikia chuo cha mafunzo kwa muda wa miezi sita.
Kuhusu shitaka la kukashifu dini, mahakama hiyo imempa adhabu ya kutumikia chuo cha mafunzo kwa muda wa miezi 18, na kufahamisha kuwa adhabu zote hizo zitakwenda sambamba, hivyo atalazimika kutumikia chuo cha mafunzo kwa muda huo wa miezi 18.
Alisema pamoja na hilo pia mtuhumiwa huyo ambaye amepatikana na makosa hayo amepewa adhabu mbili hizo ili iwe fundisho kwa wengine kutofanya makosa kama hayo ambapo alisema haki ya kukata rufaa mahakama ya mkoa ipo wazi, iwapo kama kuna upande ambao haukuridhika na hukumu hiyo.
Kwa upande wake, upande wa mashtaka unaosimamia kesi hiyo uliongozwa na Raya Issa Mselem, umeipa indhari mahakama hiyo ya kukata rufaa kwa kutoridhika na adhabu iliyotolewa dhidi ya shitaka la pili kukashifu dini.
Indhari hiyo imeitowa chini ya kifungu cha 358 (1) cha sheria za mwenendo wa jinai (CPA) namba 7/2004 sheria za Zanzibar.
Katika hukumu yake iliyodumu kwa takriban saa moja nzima, hakimu Khamis alisema kuwa upande wa mashitaka umeweza kuthibitisha makosa hayo dhidi ya mtuhumiwa huyo pasi na kuacha chembe ya shaka ya maana. Na kumuona ni mkosaji kwa mujibu wa sheria.
Alisema kuwa ushahidi wa upande wa mashitaka, umethibitisha kosa la kwanza la kuchoma moto msahafu huo kwa mujibu wa maelezo ya shahidi namba mbili, ambae alimuona akitowa vitu katika mfuko na kuvitia kwenye moto ambavyo baadae alibaini kuwa ni msahafu pamoja na juzuu hizo.
Ushahidi huo uliungwa mkono na shahidi wa kwanza wakati alipomtaka mshitakiwa huyo ahame ndani kwake alipokuwa akiishi kijana huyo, alitoka na msahafu wake na kutoa vitu vilivyokuwemo ndani yake, na baadae kuona masahafu huo kuungua moto mara baada ya kuambiwa na wanawe.
Kwa mujibu wa Mahakama hiyo, kitendo hicho cha kutoka na msahafu na kuupekuwa ni dalili tosha ya kujitayarisha na kitendo cha uchomaji ambacho alifanya akiwa ndani ya nyumba hiyo alimokuwa akiishi.
Hivyo, mahakama hiyo imefahamisha kuwa, kitendo hicho ni kweli kingeweza kuleta uvunjifu wa amani, na hasa ukizingatia kuwa mshitakiwa huyo alishambuliwa akiwa lindoni kazini kwake, pamoja na kile kitendo cha kurushiwa kiatu akiwa mahakamani wakati kesi ikiendelea.
Alisema ukiangalia mazingira hayo, ni kweli kuwa kitendo hicho kimezua hasira miongoni mwa waislamu wengi na kingeweza kuleta uvunjifu wa amani Zanzibar ambapo idadi kubwa ya wananchi ni waumini wa dini ya kiislamu.
Kuhusu shitaka la kukashifu dini, hakimu huyo alisema kuwa upande wa mashitaka nao pia umeweza kuthibitisha kosa hilo, kutokana na kuchomwa kwa kitabu hicho kitakatifu kwa waumini wa kiislamu, ambapo hata yeye mwenyewe kwa kuwa ni muumini wa dini hiyo. hivyo ameonesha dharau dhidi ya dini yake.
Alifahamisha kuwa uhuru wa kuabudu dini aitakayo mtu upo kwa mujibu wa katiba na sheria za nchi, hivyo hauwezi kuingiliwa na yoyote na kufanya hivyo ni kosa na kunaweza kusababisha matatizo miongoni mwa waumini pamoja na nchi kwa ujumla.
Hivyo kutokana na mambo mengine mengi ya kisheria yaliyojitokeza katika kesi hiyo, hakimu Khamis Ali Simai alimtia hatiani mshitakiwa huyo chini ya kifungu cha 219 cha sheria namba 7/2004 sheria za Zanzibar.
Upande wa mashitaka pamoja na kudai kuwa hawana kumbukumbu za makosa ya zamani kwa mshitakiwa, umeomba itolewe adhabu kali dhidi yake, kutokana na kitendo alichokifanya kingeweza kusababisha madhara makubwa katika jamii.
Kwa upande wake, mshtakiwa huyo aliomba apunguziwe adhabu kwa madai kwamba ana familia inayomtegemea akiwemo mke na mtoto pamoja kusumbuliwa na maradhi ya tumbo ambayo yamekuwa yakimsumbua kwa muda mrefu sasa.
Kwa mujibu wa mahakama hiyo, Ramadhan Handa Tuma alifanya kitendo kinachoweza kuleta uvunjifu wa amani, chini ya kifungu cha 74 (1) (b) cha sheria namba 6/2004 sheria za Zanzibar.
Imefahamishwa kuwa November 16 mwaka jana mahala hadharani kwa makusudi na bila ya halali alichoma moto kitabu kitakatifu yaani msahafu pamoja na juzuu za dini ya kiislamu kitendo ambacho kingeweza kuleta uvunjifu wa amani kwa jamii ya kiislamu.
Sambamba na shitaka hilo pia alihusika kuikashifu dini hiyo ya kiislamu, kwa kitendo ambacho ni kosa kwa mujibu wa kifungu cha 117 na 27 cha sheria namba 6/2004 sheria za Zanzibar.
Matokeo yote hayo yametokea eneo la Mombasa Wilaya ya Magharibi Unguja, saa 2:30 usiku wa mnamo November 16 mwaka jana.
Kesi hiyo ilifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza November 18 mwaka jana, na kwa muda wote huo mshitakiwa huyo alikuwa rumande kwa kile kilichoelezwa kwa usalama wa maisha yake ambapo mwenyewe aliiomba mahakama imrudishe rumande baada ya kupewa dhamana wakati fulani lakini alisema hawezi kuendelea kuwepo nje kwa usalama wake.
Baadhi ya waumini wa dini ya kiislamu idadi kubwa iliyokuwa ikifuatilia kesi hiyo walionesha kutoridhishwa na uamuzi huo na kusema kwamba adhabu aliopewa mshitakiwa ni ndogo kulingana na kosa alilotenda la kudharau dini ya kiislamu na waislamu kwa ujumla.
Wakiongea nje ya mahakama waumini hao wamesema vitendo kama hivyo vitendelea kutokea iwapo sheria zitatoa adhabu ndogo dhidi ya watuhumiwa kwani kitendo alichofanya ni kikubwa na kinapaswa kilaaniwa na kupigwa na waumini wote wa dini ya kiislamu kutokana na kuwa kingeweza kuchafua hali ya nchi kuwepo katika amani iwapo waumini wangepandisha jazba.
Akiongea nje ya mahakama hiyo, Katibu wa Mufti Zanzibar Sheikh Fadhil Soraga ambaye alikuwa ni miongoni mwa waumini wanaofika kusikiliza kesi hiyo tokea awali amesema yeye binafsi hajaridhishwa na uamuzi wa mahakama kwa kutoa adhabu ndogo kulingana na kitendo kikubwa lakini kwa kuwa mahakama imeshatoa mamauzi yake basi hakuna budi wauamini hao kutulia na kutizama mustakabali wa mambo yanavyokwenda.
Hii ni kesi ya kwanza kutokea ambayo iliwavuta watu wengi kufika maakamani kusikiliza ambapo vitabu vya dini kuchomwa moto kwa makusudi na kijana huyo ambaye anaeezwa kwamba alisilimu na kupewa makaazi na ngombe wa kuazia maisha na majirani zake lakini baadae alirudi katika dini yake ya kikristo ndipo mwenye nyumba akataka arejeshe nyuma yake ndipo alipokasirika na kuchoma vitabu vya kuran moto kutokana na kutakiwa kuhama ndani ya nyumba hiyo.

No comments:

Post a Comment