Monday, 21 February 2011

Polisi wazicharukia benki  
Ramadhan Semtawa
BAADA ya kuongezeka kwa kasi ya kughushi noti na kuziingiza kwenye mzunguko wa fedha, ikiwamo katika baadhi ya mabenki, Jeshi la polisi nchini, limeshukia taasisi za fedha, na kuonya endapo zitashindwa kudhibiti kusambaa kwa doti bandia, wahusika watashughulikiwa bila kujali athari za kibiashara.

Onyo la polisi limekuja wakati kuna taarifa za benki moja (jina tunalo), kutajwa katika tukio la kupitisha noti bandia na kuwalinda baadhi ya watumishi wake waliobainika kufanya wizi kupitia intaneti, kwa kuwa ikiwashtaki wataharibu biashara. Akizungumza na gazeti hili, jijini Dar es Salaam jana, Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Naibu Kamishna Samson Kasala, alionya taasisi za fedha akizitaka kuwajibika na kuzuia kupitishia noti hizo.

Naibu Kamishna Kasala, alifafanua kwamba benki, zinatakiwa kuwa za kwanza kuzuia uhalifu wa mzunguko wa fedha chafu."Kosa la  kughushi noti ni uhujumu uchumi," alisema Kasala.

Kasala alisema, kosa hilo limo katika Sheria ya Kuzuia Fedha Chafu (Money Loundering ya mwaka 2007) na kusisitiza kwamba wahusika watashughulikiwa bila kujali, wanafanya kazi katika benki gani.

Naibu Kamishna Kasala, alisema hivi sasa kuna hatari kubwa kwa matapeli na watengenezaji wa fedha bandia kwenda zaidi vijijini na kufanya manunuzi kwa wakulima kwa kutumia noti bandia.

 "Hawa wanapaswa kupatiwa elimu ya kutosha vinginevyo watatapeliwa sana,"alionya Kamishna Kasala.

Kasala alisema mtandao huo, unaochapisha noti bandia unatumia udhaifu wa ufahamu wa wananchi wengi kwa kutengeneza na kusambaza fedha hizo chafu katika mzunguuko.

Alisema jeshi la polisi kwa kushirikiana na vyombo vya dola, liko makini katika kukabiliana na tatizo hilo, lakini pia akatoa changamoto kwa Benki Kuu (BoT) kuhakikisha inafanya juhudi za dhati kutoa elimu kwa wananchi kuhusu uwapo wa noti bandia katika mzunguko.

"Kama alivyosema gavana wa BoT, nadhani wao wanapaswa kufanyakazi kubwa kuhakikisha wananchi wanapata elimu ya kutosha kuhusu noti hizo..., siku zote wajanja wanatumia mwanya wa ukosefu wa elimu kufanya uhalifu," alisema.Kwa upande wa gavana wa BoT, Profesa Benno Ndulu, alisema benki zinatakaozukutwa na noti bandia zitapaswa kubeba mzigo huo, na kuwajibika kwa mujibu wa sheria.


''Benki itakayokutwa na tatizo la kupitisha noti bandia, itapaswa kuwajibika yenyewe. BoT iko makini na haitavumulia wananchi wapitishiwe fedha chafu," alionya gavana Ndulu.Tangu kuingizwa noti mpya katika soko, kumekuwa na kasi ya watu kujaribu kuziughushi huku mtandano huo, ukionekana kugusa baadhi ya benki kubwa jijini Dares Salaam.

No comments:

Post a Comment