Sunday 2 January 2011

Waislam wataka Katiba mpya izingatie usawa


Baraza la Vijana Waislam Tanzania, limeungana na wadau mbalimbali wakiwemo wanaharakati kudai katiba mpya nchini, ila wamesema uundwaji wa katiba hiyo ulenge kutoa haki na usawa kwa raia wote bila ubaguzi au upendeleo.
Pia, baraza hilo limewataka waumini wa Kiislam nchini wasijiweke nyuma katika kushinikiza mabadiliko ya katiba, kwa madai suala hilo lina masilahi kwao na taifa kwa ujumla.
Akiwahutubia waumini wa Kiislam kabla ya swala ya Ijumaa ndani ya Msikiti wa Mwenge, Amir wa Baraza hilo, Sheikh Shaaban Mapeyo, ambaye pia ni Imamu wa msikiti huo, alisema dai la katiba linagusa watu wote na hivyo hata itakavyoandikwa ilenge haki na usawa kwa wote.
Sheikh huyo alisema kama wanajamii Waislam nao wanahitaji mabadiliko ya katiba mpya, ila iwe yenye kutoa haki na usawa kwa raia wote bila ubaguzi au upendeleo kama ambavyo katiba ya sasa ilivyo.
"Waislam tunaungana na wengine wanaodai katiba mpya, pia kama itafanyiwa marekebisho ikiwa ni mara ya 15, basi ilenge kutoa usawa na haki kwa wote badala ya kunufaisha makundi fulani na mengine kukandamizwa," alisema.
Aliongeza, dai la katiba mpya halikuanza sasa, ila safari hii limepata msukumo mkubwa, akisema kama wanaoguswa na mapungufu ya katiba ya sasa anawahimiza waumini wenzao kuamka na kuidai katiba mpya badala ya kulala.
"Waislam amkeni kudai katiba mpya au marekebisho yake, kukaa kwenu kimya ni kuonyesha kutojali au kutoguswa na mapungufu yaliyopo sasa hususani ibara ya 19 ya badiliko la 14 ya katiba iliyopo," alisema Sheikh Mapeyo.
Alisema, pamoja na kuonekana dai la katiba mpya linapata vikwazo, toka kwa baadhi ya viongozi wa serikalini, bado wananchi na wanaharakati hawapaswi kurudi nyuma na kuliacha jambo lizimike hivi hivi.
Baadhi ya watu waliibuka kupinga suala la katiba mpya ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema, aliyedai hakuna haja ya katiba mpya, kitu kilichotofautiana na kauli ya Rais Jakaya Kikwete aliyeridhia suala hilo alipokuwa akitoa salamu zake za Mwaka Mpya juzi, jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment