Sunday 2 January 2011

Mgogoro wa ardhi moto Zanzibar



Sakata la mgogoro wa ardhi kati ya waumini wa kanisa la Anglikana na Fatma Amani Karume mtoto wa Rais mstaafu, umechukua sura mpya baada ya kubainika alianza kujenga bila ya kufuata utaratibu wa sheria ikiwemo kibali cha baraza la Manispaa ya Mji wa Zanzibar na Wilaya ya Magharibi Unguja.
Hayo yamebainika katika kikao cha pamoja kati ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, viongozi wa baraza la manispaa na wa Wilaya ya Magharibi, Idara ya ardhi na upimaji pamoja na ujumbe wa watu watano wa kanisa la Anglikana walioongozwa na Askofu mstaafu John Ramadhan.
Habari za uhakika kutoka ndani ya kikao hicho zinaeleza kwamba viongozi wa Manispaa na Wilaya ya Magharibi walijikuta wakiwa katika wakati mgumu walipotakiwa kuthibitisha kama walitoa vibali vya ujenzi katika eneo la ardhi la kanisa.
"Kwa upande wetu hatujatoa kibali, na jambo hili ni geni kwetu" alikaririwa mjumbe mmoja akiwanukuu viongozi wa baraza la manispaa na Wilaya ya Magharibi Zanzibar.
Katibu wa kanisa la Anglikana, Nuhu Salanya alithibitisha ujumbe huo wa kanisa kufanya mazungumzo na Makamu wa pili wa Rais baada ya jeshi la Polisi Zanzibar kuzuia maandamano ya waumini wa kanisa hilo yaliyokuwa yafanyike leo mjini Zanzibar kupinga kitendo cha mtoto wa Rais mstaafu kuvamia eneo lao la kanisa.
Hata hivyo, katibu huyo alikataa kuzungumza chochote kuhusiana na maazimio yaliyofikiwa katika kikao hicho lakini alisema wamepata matumaini mapya kutokana na ahadi alizozitoa makamu wa pili wa rais kushughulikia sakata hilo linalozidi kuchukua sura mpya katika siasa za Zanzibar hususan serikali mpya ya umoja wa kitaifa ambayo kwa kiasi kikubwa imejenga imani kwa wananchi kuhusiana na mizozo ya ardhi.
Hivi karibuni Waziri wa Ardhi, Ali Juma Shamhuna alifuta hati 20 za ardhi za vigogo kadhaa katika eneo la Mombasa mjini Zanzibar likiwemo eneo liliokuwa likimilikiwa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Saleh Ramadhan Feruz, kwa vile maeneo hayo yalikuwa ya wazi na yalitolewa na serikali ya awamu ya sita kinyume na sheria.
Matukio hayo ya uporaji, unyang'anyi na ufisadi wa ardhi yaliripotiwa na mtandao wa kimataifa wa wikileaks na kuwahusisha baadhi ya vigogo wanahuska na matukio ya ufisadi wa ardhi kwa kujigawia maeneo nyeti kwa maslahi binafsi kwa kutumia lugha ya 'hapa pangu' jambo ambalo ni kinyume na misingi ya utawala bora.
"Tumefarijika sana, na ahadi ya makamu wa pili wa rais amesema amepokea malalamiko yetu, atayapeleka kwa Rais Dk. Shein na baadae tutaarifiwa kila hatua itakayofikia kuhusiana na suala hili," alisema katibu wa kanisa la anglikana.
Hata hivyo, habari kutoka ndani ya kikao hicho, watendaji wa idara ya ardhi na upimaji walikuwa katika wakati mgumu pale walipotakiwa kujieleza kwamba ni kweli eneo la ardhi la kanisa hilo walimpa Fatma Karume kwa shughuli za ujenzi wa makazi.
Imeelezwa kwamba watendaji hao walijitetea kuwa eneo la kanisa walichukua mita 15 na hawajaruhusu ujenzi katika eneo lilitengwa kwa shughuli ya maziko na maendeleo ya kanisa.
"Katika eneo la kanisa tumeingia mita 15 tu, na katika makaburi hatujagusa," alikaririwa afisa wa ardhi kutoka ndani ya kikao hicho.
Hata hivyo, ujumbe wa kanisa ukiongozwa na askofu mstaafu John Ramadhan ulisimama imara katika kikao hicho na kueleza wameamua kuonana na makamu wa rais baada ya kuona juhudi za kutaka eneo lao lirejeshwe kukwama kwa muda mrefu licha ya kuwasilisha malalamiko katika maeneo yanayohiska ikiwemo Ikulu katika kipindi cha uongozi wa Rais mstaafu Amani Abeid Karume.
Kikao hicho kimekuja baada ya waumini wa kanisa la anglikana kufanya misa maalum ya kuomba mwenyezimungu kwa kutumia uwezo wake eneo la ardhi waweze kulipata na liendelee kwa matumizi yaliyokusudiwa.
Baada ya kumaliza misa mnamo alasiri, walikwenda katika eneo la mzozo Mbweni, na kubomoa sehemu ya ujenzi ulioanza kufanyika na kupitisha azimio kuanzia sasa watalinda mali hiyo ya kanisa kwa kutumia nguvu zao kwa kusaidiana na nguvu za yesu kristo.
Baadae waumini hao walitawanyika lakini habari zilizopatikana zinaeleza kwamba kiongozi mmoja ameomba msaada wa Polisi kuanza kulinda eneo hilo akisisitiza kuwa ni la kwake na tayari amekutana na kamishna wa Polisi Zanzibar Mussa Ali Mussa.
Waumini wa kanisa la Anglikana walikuwa waandamane leo mjini Zanzibar kuanzia kanisa la Mkunazini hadi Ofisi za Mkuu wa mkoa wa Mjini Magharib lakini askari polisi wa Zanzibar walizuia maandamano hayo kufanyika kwa vile Mkuu wa mkoa ambaye walitarajia kumpelekea malalamiko yao hafanyi kazi siku ya Jumapili.
Hata hivyo, walishauriwa watafute njia nyingine ya kupeleka malalamiko yao na ndipo walipoamua kuomba kukutana na Makamu wa pili wa rais wa Zanzibar.
    

No comments:

Post a Comment