Watanzania tuungane kudai katiba mpya-Lipumba
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba (katikati), akizungumza kwenye mkutano na waandishi habari makao makuu ya chama hicho, Buguruni, jijini Dar es Salaam jana.
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amewaomba Watanzania wapenda demokrasia na mabadiliko kuunganisha nguvu na kudai Katiba mpya.
Aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maazimio ya Baraza Kuu la Uongozi la chama hicho ambalo lilikutana kwa siku mbili jijini Dar es Salaam.
Alisema wanataka Katiba itakayokuwa na misingi ya kidemokrasia ya kweli na itakayoweka dira ya maendeleo ya taifa kwa maslahi ya kizazi cha sasa na vijavyo.
“CUF inaungana na Watanzania wote bila kujali itikadi au nafasi walizonazo katika jamii kwa kutumia njia za kidemokrasia kudai mabadiliko ya Katiba ya nchi yetu ili ikidhi matakwa ya hali ya wakati uliopo,” alisema Lipumba.
Alisema sambamba na madai ya Katiba mpya, Baraza Kuu la chama hicho linawataka wadau mbalimbali kuungana na Watanzaia wote kuendeleza madai ya mabadiliko ya Sheria za uchaguzi na haja ya kuwepo kwa Tume huru ya uchaguzi (NEC), ambayo itaheshimiwa na kila Mtanzania kwa kutekeleza wajibu wake ipasavyo.
Alisema kutokana na matokeo ya uchaguzi yaliyotangazwa na NEC, imedhihirika kuwa tume hiyo haiko huru na haina sifa za kuweza kuaminiwa mbele ya macho ya watanzania.
Profesa Lipumba alisema alisema katika uchaguzi huo kulikuwa na kasoro, udanganyifu na mfumo wa uchakachuaji wa idadi ya wapiga kura waliojitokeza kuwa 8,626,238 kati ya wapiga kura 20,137,303 waliodaiwa kujiandikisha.
“Waliopiga kura ni asilimia 42 ya waliojiandikisha, hii ni tofauti kubwa sana ukilinganisha na waliojitokeza kupiga kura mwaka 1995 asilimia (84) na asilimia 72 mwaka 2005. Watanzania wamepoteza imani na NEC kwamba inaweza kusimamia uchaguzi huru na wa haki,” alisema.
Kuhudu sakata la Dowans, Profesa Lipumba alisema serikali haikupeleka ushahidi wa kutosha katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi (ICC), kujitetea hivyo hakuna sababu ya kuwalipa.
Alisema serikali ilipaswa kuwasilisha vielelezo vinavyoonyesha kuwa Dowans ni zao la kampuni hewa ya Richmond ambayo ililiingiza taifa katika matatizo makubwa.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment