
| Monday, 13 December 2010 09:29 |
| Na Dunstan Bahai, Jijini BAADA ya kuzushiwa kifo mara kwa mara, mwanamuziki nguli wa Tanzania, Afrika Mashariki na Kati, Ramadhani Mtoro Ongala (63), hatimaye amefariki dunia alfajiri leo.Ongala ambaye kwa jina la muziki anajulikana kama Dk. Remmy, mwili wake umehifadhiwa katika Hospitali yaTaifa ya Muhimbili. Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Hospitali hiyo, Jezza Waziri, mwili wa marehemu umepokelewa katika hospitali hiyo leo saa 10 alfajiri. Habari zaidi kutoka kwa baadhi ya watu wa karibu wa Dk. Remmy ambao walikataa kutajwa majina yao kwa kuwa siyo wasemaji wa familia ya marehemu, wamesema Dk. Remmy, aliyekuwa akisumbuliwa na kisukari, hali yake ilibadilika ghafla na kuwa mbaya usiku wa kuamkia. Wamesema kutokana na mabadiliko hayo, walilazimika kumkimbiza katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, lakini madaktari walipojaribu kumpima, waligundua kuwa tayari amefariki dunia. Wengi wanasema Remmy alishatabiri kifo chake, kwani amekuwa akiimba nyimbo kadhaa zinazohusu kifo.Pia aliwahi kunukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari hivi karibuni kuwa, endapo atapona atapata nafuu na kuruhusiwa hospitali atatunga wimbo unaowahusu manesi na madaktari, lakini hata hivyo hakuweza kukamilisha ndoto yake hiyo. Moja ya nyimbo zake ni 'siku ya kufa’, ‘uzuri wote unaoza’, ‘nyumba nalijenga inabaki’, ‘watoto na njaa wanalia...' Kwa mujibu wa tovuti ya Bongo Celebrity, Remmy alipozaliwa wazazi wake walimuita Ramadhani Mtoro Ongala. Remmy alizaliwa mwaka 1947 katika mkoa wa Kivu, Belgian Congo kabla ya kuitwa Zaire, ambayo sasa inajulikana kama Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo. Baba yake alikuwa ni mwanamuziki mashuhuri pia akiwa mpiga ngoma kwa kutumia mkono. Mara tu baada ya kuzaliwa, familia yake ilihamia Kisangani. Ingawa alianza kufundishwa masuala ya muziki na baba yake, babayake huyo alifariki dunia wakati Remmy akiwa na umri wa miaka sita. Mwaka 1964 mama yake mzazi naye akafariki dunia. Maisha ya Remmy nchini Tanzania yalianza mwaka 1978 baada ya yeye kuingia jijini Dar es Salaam baada ya kuitwa na mjomba wake, Mzee Makassy, aje ajiunge na bendi Orchestra Makassy. Wimbo wa kwanza alioandika akiwa na bendi hiyo ni ‘Siku ya Kufa’. Remmy, mwanamuziki mwenye asili ya Zaire, pamoja na umashuhuri wake nchini Tanzania, amepiga muziki mara nyingi katika nchi za Ulaya na Marekani. Akiwa na umri wa miaka sita, baba yake alifariki hali iliyosababisha mama yake kushindwa kulipia ada ya shule na Remmy kulazimika kujiingiza katika muzika ambapo miaka ya 1960 alijifunza kupiga gitaa. Akiwa na umri wa miaka tisa, hali kadhalika mama yake alifariki, hivyo ikambidi achukue jukumu la kutunza wadogo zake. Akiwa na umri wa miaka 17, alikuwa muimbaji na mpiga ngoma katika bendi ya Vijana ya Bantu Success. Hii haikuwa na maana kwa familia yake, hivyo Remmy ilimbidi atoke katika bendi hiyo. Miaka miwili baadaye, alijishughulisha tena na muziki na kujiunga na vikundi mbalimbali vya bendi za muziki akiwa mpiga gitaa. Baadhi ya vikundi hivyo ni Micky Jazz ya Zaire na Grand Mike Jazz ya huko Uganda ambapo mwaka 1978 alihamia Tanzania na kujiunga na bendi Ochestre Makassy. Bendi kubwa alizowahi kujiunga nazo ni pamoja na Virunga, Dibalo, Orchestra Supper Mazembe na Orchestra Makasi. Mwaka 1981 alijiunga na bendi ya Matimila, ikiwa na wanamuziki 18 na ikimilikiwa na mfanyabiashara mmoja na baadaye alianzisha bendi yake ya Super Matimila na kuendeleza mtindo wa kutumia magitaa 3, besi, ngoma na tarumbeta aina ya saksafoni. Remmy Ongala alipiga muziki wake kwa mtindo wa Soukous, katika maumbile mapya kabisa kwa kutumia asili na jadi ya Kitanzania. Akiimba kwa kiswahili, ushairi wake mzuri una tunzi zinazohusu siasa na pia maisha ya mtu wa kawaida na hasa utetezi wa wanyonge. Kwa ajili ya uimbaji na utunzi wake wa kuliwaza, Remmy anaitwa “Doktaâ€na ni mtu anayejulikana sana katika sehemu za Sinza ambazo ni jirani na anakoishi yeye na mkewe Mwingereza ambapo walibahatika kuzaa watoto watano. Kutokana na umaarufu huo, eneo analoishi la Sinza kipo kituo cha daladala kilichopewa jina lake la Kwa Remmy. Remmy atakumbukwa sana miongoni mwa jamii ya Watanzania kwa kutunga nyimbo za kutetea watu wanyonge. |
No comments:
Post a Comment