MBUNGE wa Monduli aliyewahi kuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, amesema Watanzania hawawezi kukwepa wala kupuuza mabadiliko ya Katiba kwani ndiyo uhai wa taifa.
Lowassa alisema hayo jana katika harambee ya kuchangia ujenzi wa Kanisa la KKKT, Dayosisi ya Kaskazini Kati, Usharika wa Kiutu, Mtaa wa Sekei, Arumeru, ambapo alifanikiwa kuchangisha sh milioni 100. Alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo.
Alisisitiza kuwa hata hivyo, mchakato wa mabadiliko hayo lazima uzingatie uzalendo na upendo kwa taifa.
“Utekelezaji wa mabadiliko ya Katiba utategemea namna mchakato mzima na mchango wa kila mmoja kwa lengo la kujenga taifa moja lenye misingi ya uzalendo na upendo kwa wananchi,” alisema.
Kauli hii ya Lowassa inakuja siku mbili baada ya serikali kukiri, kupitia kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kwamba iko tayari kusikia na kuwezesha kilio cha mabadiliko ya Katiba.
Kabla ya Pinda kutoa kauli hiyo mwishoni kwa wiki iliyopita, viongozi kadhaa wastaafu na waandamizi waliunga mkono hoja ya mabadiliko ya Katiba. Miongoni mwao ni Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, Jaji Mkuu Augustino Ramadhani, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Mark Bomani, Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani Robert Kisanga, na Waziri Mkuu Mstaafu Frederick Sumaye.
Hoja ya mabadiliko ya Katiba ilianzishwa miaka zaidi ya 18 iliyopita, lakini imepamba moto mwaka huu baada ya vyama vya upinzani, hasa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuibebea bango katika kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu. Ndiyo ilikuwa ajenda kuu ya mgombea urais kupitia CHADEMA, Dk. Willbrod Slaa.
Mbali na wanasiasa, wasomi, wanaharakati na wananchi wa kawaida wamekuwa wakitoa madai ya mabadiliko ya Katiba, huku wengi wakitaka Katiba mpya, na serikali ikitaka kufanya mabadiliko madogo madogo kama ambavyo imekuwa inafanya miaka yote.
Kwa mujibu wa Lowassa, kutokana na uzito wa mjadala unaoendelea, jambo muhimu ni mchakato wa kuipata Katiba hiyo; na kwamba Katiba bora itategemea kwa kiasi kikubwa mchakato mzima utakavyokuwa na mchango wa kila Mtanzania katika kujenga taifa lenye umoja na upendo.
Kutokana na umuhimu wa suala lenyewe, Lowassa alisema aliwaasa viongozi wa dini kuzingatia kuwa wana wajibu mkubwa wa kuliombea suala hilo.
Alisema katika mijadala mikubwa inayoendelea hivi sasa ya kitaifa inapaswa kutanguliza nia njema na upendo kwa wananchi.
“Leo tunazungumzia umuhimu wa kufanya mabadiliko ya Katiba yetu. Ni mjadala muhimu sana kwa uhai wa taifa. Utekelezaji wa mabadiliko hayo utategemea mchakato mzima na mchango wa kila mmoja wetu katika kujenga taifa moja, lenye uzalendo na upendo kwa wananchi.
“Tutumie kanisa hili kuombea nchi amani, na kupanda mbegu za upendo kama tunavyoagizwa na Injili. Ninaamini tukiweka mbele upendo basi mjadala huu ambao kila mmoja anayeitakia mema nchi yetu anatambua umuhimu wake, utafanikiwa na hatimaye tutapata suluhisho la pamoja na kudumu kwa njia na kwa namna iliyo bora zaidi,” alisema Lowassa.
Alisema iwapo viongozi watamtanguliza Mungu, mjadala wa Katiba, utapita kwa utulivu na amani kwa maslahi ya kila Mtanzania.
“Naamini kwamba mjadala wa Katiba unapaswa kumshirikisha kila Mtanzania mwenye mapenzi mema na nchi yake ili tuweze kufikia suluhisho la pamoja la kudumu kwa namna iliyo bora,” alisema Lowassa.
Akisisitiza umuhimu wa kumtanguliza Mungu kwa kila jambo, Lowassa alisema anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumpitisha salama katika wakati mgumu.
“Namshukuru Mungu hata katika kipindi kile ambacho nilikuwa naandamwa sana, niliyaweza magumu yote katika yeye anitiaye nguvu, tuendelee kumtegemea Mungu. Amina.”
Kwa upande wake, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayoyosisi ya Mkoa wa Arusha, Thomas Laizer, alisema umefika wakati muafaka kwa makanisa kuanza kujiendesha yenyewe.
“Kwa miaka mingi wenzetu waliotuletea neno la Mungu kutoka Ulaya na Amerika sasa wameona kuwa neno hilo tumelipokea na kanisa limekua,” alisema Askofu Laizer.
Akishiriki katika kutoa harambee yake Lowassa alikabidhi hundi ya sh milioni 10, huku Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Goodluck Ole Medeye akitoa sh milioni tatu.
Wengine waliochangia harambee hiyo ni mfanyabishara wa madini, Mathias Manga, aliyetoa sh milioni 3.7 huku mfanyabishara mwingine Justine Nyari akitoa milioni moja.
Naye Mkurugenzi wa Hoteli ya Impala, Meleu Mrema, alichangia sh. milioni mbili huku mmiliki wa shule ya Bishop Dan, Sarundere Lendisa, akitoa sh milioni 1.5.
Harambee hiyo ilifanikisha kupatikana kwa fedha taslimu sh milioni 62 na ahadi zikiwa sh milioni 37.
Katika hatua nyingine, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA), amesema anatarajia kupeleka hoja binafsi bungeni kuhusu suala la Katiba mpya kabla ya kuanza kwa kikao Februari 2011.
Kutokana na taratibu za Bunge katika vifungu vya 53 mpaka 55, mbunge anapaswa kuwasilisha hoja binafsi kwa Katibu wa Bunge siku moja kabla ya kuanza kwa kikao cha Bunge.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mnyika alisema anatarajia kuwasilisha hoja hiyo ndani ya wiki hii, kwani akiwa mwakilishi wa wananchi anajua kuwa kilio chao kikubwa ni kuhusu Katiba mpya, ambayo ndiyo inasimamia misingi ya mipango yote ya maendeleo ya taifa.
Alisema Bunge ndilo lenye maamuzi ya kutunga sheria, hivyo haoni sababu ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kupeleka ushauri kwa Rais juu ya jambo hilo kwa ajili ya kufanyia marekebisho Katiba iliyopo.
“Hapa ni kutaka kufunika hoja na kutaka kukwepa mjadala kwa kufanyia marekebisho wakati Katiba inahitaji kubadilishwa,” alisema.
Mnyika alisema Bunge linapaswa kuweka utaratibu wa kuunda kwa tume pana na kupitisha azimio kwa haraka, ili kuwa na mkutano mkuu wa Katiba utakaoshirikisha wananchi wote na kupiga kura ya maoni.
Alisema kuwa mwaka 1977 umma haukushirikishwa wakati wa kuandika Katiba hii iliyopo na kwamba Katiba ya sasa ni ya chama kimoja; hivyo inahitajika Katiba ya kwenda na mazingira ya sasa, maana hadi sasa iliyopo imeshafanyiwa marekebisho zaidi ya 14.
“Changamoto nyingine ni kwenye Muungano maana kumefanyika marekebisho ya Katiba ya Zanzibar ambayo inasema Zanzibar ni nchi wakati Katiba yetu inasema Tanzania ni nchi moja; bado tunahitaji kuwa na Katiba mpya katika hili,” alisema.
Alisema kwamba ni busara Bunge kuwa chombo na wawakilishi wa wananchi kuchukua hoja hiyo na serikali kufuata yale yatakayojadiliwa na kutolewa mapendekezo kuhusu suala hilo la Katiba na Bunge.
“Ni busara kwa Bunge kuchukua nafasi yake, Ibara ya 8 ya Katiba kifungu cha kwanza inatamka kwamba wananchi ndiyo wenye mamlaka na serikali kupata mamlaka kutoka kwa wananchi...ibara ya 63 kifungu cha 2 kuna chombo kinachoitwa Bunge ambacho kitasimamia na kuishauri serikali kuhusu Katiba,” alisema.
Mnyika alisema hivyo Bunge ndilo linalopaswa kuifanyika kazi hoja ya kuwa na Katiba mpya na si serikali, kwani yenyewe itapokea ushauri unaotolewa na Bunge kwa ajili ya kuanzisha haraka mjadala wa Katiba.
Alisema Katiba ni sawa na mkataba ambao unaongoza dira ya taifa na anayepaswa kuandika mkataba huo ni mwenye mali hivyo badala ya serikali kuanza kuandika mkataba huo inabidi Bunge lianze mapema.
Alieleza Kamati ya Rais haiwezi kulifanyia kazi vema suala la Katiba na hata kamati zilizopita zilishindwa kushirikisha wananchi kwa ukaribu hivyo hakuna haja ya kuunda tume nyingine na kuingia gharama. |
No comments:
Post a Comment