Monday, 20 December 2010

Lipumba amlilia Mkurugenzi TBC

na Mwandishi wetu
  
MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF) Profesa Ibrahimu Lipumba amemtaka Rais Jakaya Kikwete kutengua uamuzi wa kumuondoa aliyekuwa Mkurugenzi wa TBC Tido Mhando na kurudishwa kazini.
Akizungumza mwishoni mwa wiki katika mkutano wa hadhara uliofanyika Temeke Dar es Salaam, Lipumba alisema hata kama mkataba wake uliisha lakini kulikuwa na jambo la busara la kumrudisha Tido kazini kwa mkataba mpya.
Alisema kama TBC ni ya serikali na si ya Chama cha Mapinduzi (CCM) hakukuwa na sababu ya kuitwa chombo cha serikali kingeitwa chombo cha CCM, ili katika uchaguzi kifanye kazi za chama hicho tu.
Alisema serikali inakosea kwa kusema kuwa Tido alikuwa anapendelea wapinzani, ila kama ni chombo cha serikali hakuna jambo muhimu kama chombo hicho kikawa kinafanya kazi za wananchi wote bila kujali chama, wala rangi ya mtu.
“Tido alifanya kazi kwa niaba ya wananchi na chombo cha serikali ni lazima kiwe kinafanya kazi kwa niaba ya watu wake. Hata hivyo mkurugenzi huyo amejenga heshima kwa taaluma ya habari kwa kuwa alifanya kazi bila ya upendeleo wa chama chochote,” alisema Profesa Lipumba.
Akizungumzia Katiba alisema katika uundwaji wake ni lazima kuwashirikisha wasomi mbalimbali kama vile Profesa Issa Shivji na Jaji Robert Kisanga ambao watakuwa na mawazo ya heshima na kujenga nchi.
Naye Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Hamad, alisema chama hicho kimepiga hatua kutokana na kuwa na madiwani 139 kutoka katika idadi ya madiwani 52.
Alisema kwa upande wa wabunge Tanzania Bara idadi ya wabunge imeongezeka kutoka ziro hadi kufikia idadi ya wabunge wawili, jambo ambalo limekifanya chama hicho kupiga hatua hivyo aliwataka wanachama wa chama hicho kutokata tamaa.
Hata hivyo, alisema anawashangaa wanasiasa na watu wengine ambao wanabeza suala la maridhiano na kwamba watu hao ni wa kufukuzwa kwani hawafai kuishi nchini.
Mbali na maendeleo ya chama hicho Maalim Seif alisema chama chake kimeandaa rasimu ya katiba ambapo aliwataka viongozi wa CUF kuwasilisha kwa Rais mapendekezo hayo.


No comments:

Post a Comment