Wednesday, 22 December 2010

Aliyelipua basi Kenya ni Mtanzania

NAIROBI, Kenya

JESHI la Polisi nchini Kenya limemtaja Albert Olando Mulanda, (35) raia wa Tanzania, kuwa ndiye aliyelipua basi la abiria lililosababisha watu 41 kujeruhiwa.Kwa mujibu wa Kamishna wa Polisi, Mathew Iteere, Mulanda ambaye ndiye mtu pekee aliyekufakatika tukio hilo, aliingia nchini humo kupitia mpaka wa Laitoktok Oktoba 23, mwaka huu kwa kutumia hati ya muda ya kusafiria iliyokuwa na namba 0903962.

Kamishna huyo wa Polisi amesema Mulanda alifanya tukio hilo peke yake na wala siyo sehemu ya kundi lililosadikiwa awali kufanya shambulizi hilo.

Awali baadhi ya mashuhuda walidai kuwa shambulizi hilo lilifanywa na watu watatu huku wengine wakidai kuwa waliohusika walikuwa ni watu zaidi ya saba.

Kamishna huyo ameeleza kuwa alama za vidole za Mulanda zimetumwa Idara ya Uhamiaji ili kuthibitishwa na mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha mjini Nairobi.

Imeelezwa kuwa vifaa vya mlipuko huo vimegundulika kutengenezwa nchini Russia na inasadikika vilipatikana nchini Tanzania na vinafanana kama vilivyolipua gari aina ya Land Rover ya Kamishna wa Wilaya ya Embakasi Desemba 3, mwaka huu.

Jeshi hilo pia linahusisha mlipuko huo ambao ulitokea mjini Nairobi katika Barabara ya River na kulilenga basi la kampuni ya Kampala Coach na milipuko mingine miwili iliyotokea mapema katika mji huo na vifaa vingine 26 vya milipuko vilivyopatikana baadaye ndani ya basi mjini Kampala.

Kutokana na hali hiyo, makachero wanajaribu kufuatilia namba za simu ndani na nje ya nchi hiyo ambazo zilipatikana kwenye kitabu cha kutunza kumbukumbu kilichokutwa mfukoni mwa mtuhumiwa.

“Tupo kwenye hatua za kufuatilia taarifa tulizozikuta kwenye kitabu chake cha kumbukumbu ila inaonekana shambulizi hilo lilikuwa limeelekezwa Uganda,” amesema Kamanda Iteere.

No comments:

Post a Comment