Sunday, 1 September 2013

WANANCHI KOMBENI NA FUONI WAIOMBA SERIKALI KUWAPATIA ENEO LINGINE LA MAKAZI



551
 
Na Ali Issa –Maelezo Zanzibar 
Wananchi wa Shehia za Maungani, Kombeni na Fuoni katika wilaya ya Magharibi Unguja  wameiomba Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kuwapatia eneo jengine la makazi badala ya Eneo la awali wanaloishi watu hao hivi sasa kudai  kuchukuliwa   na Jeshi la wananchi wa Tanzania kwa lengo la utanuzi wa kambi ya kisakasaka.
Hayo yamesemwa leo huko skuli ya msingi  Fuoni kitongani na Mwenyekiti wa kamati ya Umoja wenye mashamba  Khamis Vuai Makame alipokuwa na mazungumzo na wana Vijiji hivyo katika mkutano maalumu ulio ambatanisha waandishi wa habari kufuatilia ujio na maamuzi ya viongozi walio toa juu ya   mgogoro huo walipo watembelea.
Amesema mpaka sasa hakuna utekelezaji juu ya  ufumbuzi ulio tolewa wa tatizo hilo, licha ya viongozi kujaribu  kutoa maamuzi ambayo yengelifuatwa tatizo hilo lingekua limeshamaliza.
 Aidha Mwenyekiti huyo amesema hali hiyo kwakweli ina athiri harakati za kimaendeleo kwa mtu mmoja mmoja au jamii yote  kwa kukosa fursa kuya tumia maeneo yao katika harakati za kiuchumi na uzalishaji wakiwa raia wema, huru na wanaofuata sheria na taratibu za Nchi.
“Kwakweli hatutendewi haki kwani viongozi wanapo toa agizo wajibuwake kutekelezwa lakini hapa sisi hadi leo ya tolewe maamuzi na maelekezo hakuna utekelezaji wowote na sisi tuna athirika na familia zetu”, alifahamisha Mwenyekiti kwa masikitiko.
Alifahamisha  katika hatua walizo zichukua awali walikutana na Makamo wa Pili wa Rais  Balozi Seif Ali Iddi, na Waziri wa Ulizi wa Serikali
ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Shamsi Vuai Nahodha kuwaelezea tatizo hilo ili kupata njia muafaka za mgogora huo na viongozi hao kutoa maamuzi lakini bado hakuna hatua yoyote iliyofikiwa, huku wakiendelea kuathirika.
Sambamba na hilo  alisema pamoja na kuwepo taratibu za kufatilia matatizo hayo lakini bado Serikali haijatoa ufumbuzi wa aina yeyote
licha ya kuahidiwa kulipatia ufumbuzi ndani ya miezi mitatu lakini la kushangaza ni mwaka mmoja hivi sasa.
Pia alisema katika dira ya maendeleo ya Vijiji kuna mpango wa uanzishwaji wa ujenzi wa barabara kutoka kombeni hadi Fuoni jambo ambalo halitoweza kufanyika kutokana na tatizo hilo.
Mapema katibu wa kamati hiyo Omar Khatibu Omar akimkaribisha mwenyekiti wa kamati hiyo alisema kua mnamo mwaka 1978 chombo hicho cha ulinzi kilifika katika eneo hilo na kuonana na wakaazi kwa ajili ya kupata eneo la kuanzisha kambi ya kijeshi Kisakasa kwa kushirikiana na familia 10 zilizokuwa zikishi kwa wakati huo kwa makubaliano ya kutaka kupewa eneo kwa masharti ya  kulipwa fidia wananchi lakini  kutoka mwaka huo hadi leo hakuna mwana nchi alio pewa fidia hiyo.
Alisema pamoja na hayo wananchi bado  wana imani na jeshi hilo kwani ni lao wenyewe,  jambo la msingi kufuatwa taratibu na kuthamini haki za binaadamu kwani nao ni raia wa Tanzania ambao  hupaswa kuwa na makaazi bora ambayo hayatowaletea athari yoyote wananchi wao.
Nae mwananchi Mzee Hamis Mwinyi akielezea kwa uchungu alisema, yeye ni miongoni mwa watu kumi waliokubaliana kutoa eneo kwa jeshi kuweka kambi kwa masharti ya malipo lakini hadi hivi leo bado hawaja lipwa na maeneo yao yanaendekea kuchukuliwa na Jeshi kinyume na makubaliano yao na kuekewa mabango kuwa eneo hilo ni sehemu ya  kambi.
 Mzee huyo alisema jambo jengine linalo washangaza kuona jeshi wamezidisha eneo kwa kuweka mabango katika makaazi ya waananchi ambapo awali hayakuwemo jambo ambalo limekuwa likitutia mashaka hasa ikizingatiwa hakuna elimu ya usalama kwa wananchi.
Kutokana na hali hiyo wananchi wamerudi nyuma katika hatua za kimaendeleo ikiwemo kuanzisha Ujenzi wa vituo vya afya, elimu na hata
mambo ya kilimo na ufugaji.
Kutokana na hali hiyo ilielezwa  zaidi ya koo 224 zimeathirika kufutia utanuzi wa kambi hiyo, ikidaiwa kwa makisio ya likomita saba kwa upana na urefu.

No comments:

Post a Comment