Monday, 9 September 2013

Jussa atoa somo kwa Muhammed Seif Khatib

 
                                                                                                                                                                                                       
Na Ismail Jussa
Kwa sisi Waswahili ambao ni watu wa Mwambao wa Afrika Mashariki kuna usemi maarufu tunaoutumia kumueleza mtu aliyeamua kuuanika mwenyewe uovu wake pengine bila hata ya kukusudia. Mtu wa aina hiyo huambiwa “Imemkumba halbadiri ya Mbayana” kwa maana ya kisomo maalum cha kidini chenye kumfanya ajibainishe mwenyewe.
Kwa hali niliyoiona leo nadhani Mohamed Seif Khatib imemkumba hiyo ya Mbayana. Na sijui kama hatoanza kuokota makopo karibu kabisa.
Baada ya kupotea mitaani kwa miezi kadhaa kutokana na kushindwa kujiendesha baada ya kutonunuliwa, kigazeti cha NIPE HABARI kinachomilikiwa na Mohamed Seif Khatib leo kimetoka na toleo maalum la kujaribu kuleta chuki na fitina za kisiasa za kuonesha kuwa harakati za Wazanzibari wanaotaka Mamlaka Kamili wanataka kupeleka mamlaka hayo Ughaibuni na kwa picha zilotumika kuwekwa ukurasa wa mbele Ughaibuni kulikokusudiwa ni kurejesha Usultani.
Propaganda hii aliieleza vizuri Rais mstaafu wa Zanzibar Dr. Amani Karume katika hotuba yake ya kuwaaga wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM pale alipowaambia kuwa imepitwa na wakati na haina mvuto tena kwa vijana wa leo ambao wanataka kauli za matumaini na siyo kutishiwa mambo yasiyoingia akilini. Si ajabu kila kukicha CCM Zanzibar imekuwa ikijichimbia kaburi yenyewe. Tartiiiiiib!
Lakini kwa leo mimi nataka nikubaliane na kigazeti hichi cha propaganda dhaifu na za kitoto za Mohamed Seif Khatib na nakuombeni na nyiye wenzangu tukubaliane naye kwamba wenye kutaka mamlaka kamili wanataka kurejesha mamlaka hayo kwa Sultani. Ila tuseme tu kuwa na yeye Mohamed Seif Khatib yumo katika vibaraka hao maana na yeye pia anayataka hayo hayo japokuwa hana ujasiri wa kuyasema lakini kaamua kuyafikisha kwa Watanganyika kwa njia ya kuyaandikia shairi kwenye kitabu chake cha WASAKATONGE.
Tujikumbushe ujumbe wa kibaraka anayetaka mamlaka kamili ili ayapeleke kwa Masultani Mohamed Seif Khatib, ujumbe anaowapelekea Watanganyika kutoka kitabu chake cha Wasakatonge, Shairi Nam. 4 liliomo kwenye ukurasa wa 3 ambapo anasema:

KOSA?
1. Metufunga kamba,
Za miguuni,
Za mikononi,
Za midomoni,
Na kututosa baharini!

2. Eti mnataka,
Tuogelee,
Tujongelee,
Tujiokoe,
Hadi tufike ufukweni!

3. Kosa letu kubwa,
Kudai haki?
Yetu miliki?
Mna hamaki,
Na huku mnatukashifu!

4. Msitunyanyase,
Siyo watwana,
Watu wa maana,
Tuloungana,
Kwa heshima na taadhima!

5. Sisi tuna kwetu,
Wenye asili,
Ilo kamili,
Na serikali
Ilopatikana kwa damu!

6. Kuheshimiana,
Kwa kupendana,
Kuelewana,
Kusikizana
Hilo tutakubaliana!

Ahsante Msakatonge Mohamed Seif Khatib kwa kutujuvya leo kwamba kumbe lengo lako la kuwaambia hivi Watanganyika ni kuyadai mamlaka yako ili kisha uyapeleke Ughaibuni kwa Masultani.
Masikini Chama Cha Mapinduzi leo kinatetewa na vitimbakwiri kama hawa. Kama si Ya Mbayana tuseme nini?

No comments:

Post a Comment