Wednesday, 21 August 2013

Tutapambana na wanaoturejesha nyuma- Mansoor 


Mansoor Yussuf Himid amevuliwa gamba lakini bado hajutii chama chake kumvua gamba anasema 'tunahitaji kuwa na mapinduzi ya fikra'

Mansoor Yussuf Himid Mwakilishi wa Jimbo la Kiembe Samaki kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) anasema ‘tunahitaji kuwa na mapinduzi ya fikra’
Mansoor Yussuf Himid Mwakilishi wa Jimbo la Kiembe Samaki (CCM) amesema Zanzibar inahitaji mapinduzi ya kifikra ili wananchi waweze kusonga mbele katika kuiletea mabadiliko nchi yao.
Mansoor amesema hayo leo katika kipindi cha kinaga ubaga kinachorushwa hewani na Radio ya DW ambapo alisema ana matumaini makubwa ya wazanzibari kusonga mbele katika kuiletea maendeleo nchi yao katika mchakato wa kupatikana katika mpya nchini Tanzania ambapo alisema anafurahishwa na mijadala inavyokwenda hasa inayohusisha masuala la Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Mwakilishi huyo ambaye hivi karibuni amejinyakulia umaarufu mkubwa kutokana na misimamo yake ya kuitetea Zanzibar amesema wapo watu ambao wana fikra za kudumaza mapambano yanayoendelea ya kutaka mabadiliko katika muungano lakini alisema hawatafanikiwa kwa kuwa wazanzibari watapambana nao .
“Ni kweli wapo watu wenye fikra za kizamani wasiotaka maridhiano wasiotaka mabadiliko na wasioitakia mema Zanzibar lakini tutapambana nao wenye fikra hizo za kihafidhina wenye fikra za kukataa mabadiliko na kukataa maendeleo” alisema Mansoor.
Aidha alionesha kufurahishwa kwake na wimbi la vijana ambao kwa dhati wanaonekana kupata kuleta mabadiliko katika nchi yao huku akisifia hali ya amani iliyopo sasa baada ya kufikiwa maridhiano ya kisiasa kati ya vyama viwili vikuu vya CCM na CUF.
“ Hakuna anayebisha kama hali ya amani iliyopo tunapaswa kujivunia nayo kwa sababu huko nyuma tulikuwa hatuna amani na ilikuwa mtu hajui wakati gani atapigwa au atakutwa na nini watu wakiishi kwa wasiwasi sasa hivi tunapaswa kushukuru kwa hali tulionayo” aliongeza Mansoor.
Mansoor alisema dhamira sahihi ya maridhiano yanahitajika kukubaliwa na kila mmoja katika vyama vya siasa ambavyo vimeunda umoja wa kitaifa, ili kujenga umoja wa kitaifa wa kweli kweli.
Akitaja mafanikio ya kisiasa alisema muhimu kuliko yote ni amani na utulivu uliopo ambapo tokea kurejea kwa mfumo wa vyama vingi kumekosekana kwa amani na hivyo kuja kwa umoja wa kitaifa kumeleta matumaini makubwa kwa wananchi na wapenda amani.
Aidha suala la kushutumiana kwa viongozi wakuu akiwemo Rais wa Zanzibar Dk Ali Shein na Makamo wake wa Rais Maalim Seif Sharif Amani alisema wapo katika hali ya matumaiani na nzuri ya kuendeleza ustaarabu na uungwana lakini wapo wenye ukorofi ambao wanachochea hali ya kukosekana amani na kujiona ndio wao.
“Wapo wanasiasa wanaona kama hujatukana matusi ya nguoni kama hujawa mhafidhina bado hujawa mwanasiasa madhubuti” aliongeza.
Akizungumzia msimamo wa hali ya kisiasa iliyopo alisema anaiona Zanzibar yenye matumaini na Zanzibar yenye nuru ambapo alisema anawaona vijana madhubuti wasiofungwa na fikra potofu na fikra zisizofungamana na chochote lakini wazanzibari hivi sasa wanafikiria kusonga mbele zaidi.
Hata hivyo alisema wazanzibari wa leo hawataki kuletewa chuki wala kuletewa ubaguzi na hakuna aliye tayari kurudi nyuma walipotoka kwa kuwa wameshafahamu kwamba kwa miaka kadhaa wamekosa kuiletea nchi yao maendelea kutokana na migogoro ya kisiasa.
“Wazanzibari hatuwezi kurudi kule tulipotoka, wazanzibari hivi sasa wanataka mabadiliko wanataka kusonga mbele na kamwe hataki kurudi tunapotoka hakuna mzanzibari utayemshawishi kurudi nyuma bali kila mzanzibari anataka kusonga mbele na kuendeleza umoja na mshikamano” alisema Mansoor.
 

No comments:

Post a Comment