RAIS DKT. JAKAYA KIKWETE ATEUA MAKATIBU WAKUU WAPYA
Rais
Jakaya Kikwete amefanya uteuzi wa makatibu wakuu kumi na mmoja na naibu makatibu
wakuu 14 wapya katika wizara mbalimbali.
Miongoni
mwa walioteuliwa ni Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU),
Profesa Sifuni Mchome ambaye sasa anakuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi na aliyekuwa Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Deodatus Mtasiwa
ambaye anakuwa Naibu Katibu Mkuu, Tamisemi.
Mtasiwa
na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Blandina Nyoni
walisimamishwa kazi na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda Februari, mwaka jana kupisha
uchunguzi dhidi yao, kutokana na kukithiri kwa migomo ya madaktari nchini,
pamoja na utendaji wao kulalamikiwa.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana, Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue alisema:
“Mtasiwa ameteuliwa kwa kuwa uchunguzi dhidi yake haujaonyesha kuwa ana kosa
lolote, lakini wenzake (Nyoni) na aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na
Madini, David Jairo bado wanachunguzwa.
Katika
uteuzi huo, aliyekuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Peniel Lyimo
amehamishiwa Ikulu kusimamia Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), kuwa Naibu
Mtendaji Mkuu mwenye jukumu la kuanzisha na kuongoza Idara ya Mageuzi ya
Kilimo.
Makatibu
wakuu walioachwa kwa maelezo kuwa watapangiwa kazi nyingine ni Sethi Kamuhanda
(aliyekuwa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo), Kijakazi Mtengwa
(Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto) na Omary Chambo (Uchukuzi), huku
aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Patrick
Rutabanzibwa akistaafu wa hiari.
Balozi
Sefue alisema Rais Kikwete ameanzisha kitengo kipya katika Ofisi ya Waziri Mkuu
(Tamisemi), kitakachokuwa kikishughulikia afya ambacho kitasimamiwa na Dk
Mtasiwa.
Aidha,
aliwataja makatibu wakuu waliohamishwa wizara kuwa ni Florens Turuka kutoka
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia kwenda Ofisi ya Waziri Mkuu na Joyce Mapunjo
kutoka Viwanda na Biashara kwenda Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Makatibu
wakuu wapya
Alisema
Jumanne Sagini ambaye alikuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi),
ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo.
Dk
Servacius Likwelile ambaye alikuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha ameteuliwa
kuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo. Dk Patrick Makungu ambaye alikuwa Naibu Katibu
Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Tekinolojia pia ameteuliwa kuwa Katibu
Mkuu wa wizara hiyo.

No comments:
Post a Comment