Friday, 16 August 2013

Labda Scotland Yard, ninashida na Polisi ya Tanzania


Katie Gee (kushoto) na Kirstie Trup. Mabinti raia wa Uingereza waliopatwa na mkasa wa kumwagiwa tindikali eneo la Shangani, Zanzibar.
Katie Gee (kushoto) na Kirstie Trup. Mabinti raia wa Uingereza waliopatwa na mkasa wa kumwagiwa tindikali eneo la Shangani, Zanzibar.
KABLA ya kubaini wamekuja makachero wa Scotland Yard kuchunguza kumwagiwa tindikali kwa wasichana wa Kiingereza ndani ya Mji Mkongwe wa Zanzibar, nilihofia sana ukweli wa tukio hautapatikana.
Ukweli wa tukio hilo nilihofia hautaelezwa kirahisi kwa kuwategemea askari polisi wetu kwa sababu zilizo wazi.
Mojawapo ni ukweli kwamba hawa wetu hawana rekodi nzuri katika jukumu muhimu la kuchunguza matukio ya kigaidi kama hili la kumwagia watu tindikali.
Katika eneo hili la kufanya uchunguzi baada ya kutokea tukio la namna hii – na hapa nazungumzia matukio kadhaa ya kujeruhi viongozi wa dini na serikali, pamoja na kuwaua baadhi yao kwa risasi za moto, polisi yetu ni dhaifu.
Ila udhaifu huu pengine unatokana na mazingira mazima ya utendaji kazi wa taasisi za kidola kwa jinsi unavyogubikwa na mihemuko ya nje ya utashi wao.
Mara kadhaa Polisi ya Tanzania imethibitisha kuwa haiko tayari, labda kwa utashi wao wenyewe au kwa kutokana na kugubikwa na misukumo au niseme shinikizo za kisiasa, kuthubutu kusema ukweli inapotokea imechunguza matukio kama haya.
Nakumbusha matukio yaliyotokea Zanzibar, miaka ya 1990, hasa baada ya kurudishwa mfumo wa vyama vingi nchini. Kulikuwa kumeshamiri matukio ya watu kutupa na au kupaka kinyesi kwenye visima vya maji ya kunywa na kusiliba kinyesi kwenye madarasa ya skuli.
Yalikuwepo pia matukio ya kupigwa wananchi kwa kutumia bakora/mijeledi pamoja na kujeruhiwa kwa kupigwa mapande ya nondo; na matukio la kuchomwa na kulipuliwa kwa moto na au mabomu ya petroli (TNT) maskani za Chama Cha mapinduzi (CCM) na ofisi za serikali.
Pamoja na matukio hayo, kikundi cha watu mahsusi kilizoea kuchapisha na kusambaza vipeperushi vyenye ujumbe wa aina wenye matusi ya nguoni dhidi ya viongozi wa upinzani hasa Chama cha Wananchi (CUF) na vingine vyenye ujumbe unaolenga kuchonganisha serikali na wananchi.
Katika matukio hayo hakuna hata mara moja Polisi walitoa taarifa ya uchunguzi walioufanya. Na matukio yaliendelea mpaka pale wananchi wema kisiwani Pemba walipowanasa wahusika wakuu wa ushenzi ule.
Vijana wa Micheweni walifanikiwa kuwanasa wanausalama wa serikali wakiwa kwenye gari lenye namba za kikosi kimojawapo cha ulinzi na usalama, wakiwa na majerikeni na ndoo zilizojaa vinyesi, mafuta ya petroli, chupa na tambi za kulipulia mabomu ya petroli.
Ilikuwa ni usiku mkubwa gari lilipoingia kijijini na kujikuta limezungukwa ambapo walipopekuliwa walikutwa wamesheheni vifaa hivyo, huku wakiwa na bunduki.
Walipoulizwa, na kwa sababu wanajulikana kwa majina na sura kuwa ni askari wa serikali, walidai walikuwa wakisaka wahalifu na kwamba “mizigo” hiyo waliikuta imefichwa.
Wanausalama hao walipigwa kisawasawa na tangu siku hiyo, mtindo wa watu kumwaga vinyesi ulikoma. Katika kujaribu kutafuta huruma ya wananchi na ulimwengu, vikosi vilitangaza kuwa watu wasiojulikana wamevamia askari na kuwapora bunduki aina ya Sub Machine Gun (SMG).
Tuhuma hizo moja kwa moja zilishushiwa aliyekuwa mbunge wa Micheweni wakati ule.
Zile zilikuwa ni enzi za giza. Enzi ambazo watawala waliamini kuwa wanaweza kuendesha siasa za kijambazi dhidi ya vyama vya upinzani na wafuasi wa vyama hivyo, na isiwe lolote.
Matukio ya kulipuliwa kwa mabomu ya petroli yalifurtu ada/ yalishamiri kiasi cha kunisukuma kuyatafutia jina mahsusi ili yafahamike kwa urahisi kwa wananchi. Niliita milipuko ile kama “milipuko ya kishetani.”
Inspekta Jenerali wa Polisi Tanzania (IGP) wakati ule Omari Mahita, alimteua aliyekuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba kuongoza kikosi cha makachero kutoka Makao Makuu ya Upelelezi Dar es Salaam, kufanya uchunguzi wa matukio yale.
Kama nilivyotarajia na walivyotarajia wananchi wengi waliokuwa wakifuatilia mwenendo wa mambo Zanzibar, Manumba na kikosi chake hawakutoa ripoti ya matokeo ya uchunguzi walioufanya licha ya kuahadi kuiweka hadharani ripoti ya uchunguzi huo.
Katika miaka ya karibuni hapa, Jeshi la Polisi limeendeleza utamaduni uliojengeka sasa kuwa ni “mazoea” wa kuchunguza kwa kutangazia wananchi kuwa uchunguzi unafanywa, lakini kwa kuficha kutangaza ripoti ya uchunguzi walioufanya.
Si hivyo tu. Kumekuwa na kitu kinachofaa kuitwa “ulegevu” katika kuchunguza kwa umakini matukio ya kihalifu yenye sura ya ugaidi.
Kwa sababu wanazozijua wakubwa wa taasisi ya Polisi nchini, imeamua kutojishughulisha na kuchunguza matukio mazito ya kihalifu yanayotokea maeneo mbalimbali ya nchi.
Ilianzia na tukio la kutekwa, kuteswa na kutelekezwa bila ya msaada Menyekiti wa Madaktari Tanzania (MAT), Dk. Steven Ulimboka aliyeongoza wenzake katika kuibana serikali ishughulikie tatizo la uhaba wa vitendea kazi na maslahi duni ya madaktari na wafanyakazi wengine wa sekta ya tiba nchini.
Alitekwa katika mazingira yaliyoonesha wahusika ni mawakala wa dola. Alifanyiwa mbinu asifikishwe hospitali kuu kutibiwa.
Hakuna uchunguzi uliofanywa na serikali. Hata ule uliotangazwa kufanywa na Kamishna wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova, haukufika popote kwani uliuliwa kusudi kwa kumkamata na kumfikisha mahakamani haraka aliyetajwa kama raia wa Kenya akihusishwa na tukio hilo.
Kuuliwa kwa mwandishi na mtangazaji wa kituo cha televisheni cha Channel Ten wa mkoani Iringa, Daud Mwangosi, ambako kulifanywa na askari wa Jeshi la Polisi.
Uchunguzi wake ulifanywa chini ya vitisho vingi. Na hatimaye ripoti yake kuja kutolewa katika mazingira yaliyokirihisha wananchi.
Kuvamiwa, kuteswa vibaya kwa Mhariri Mtendaji wa New Habari House, Absalom Kibanda ambako serikali haikutangaza kuwa imechunguza. Hakuna mtu aliyekamatwa kufikia leo kuhusiana na tukio hilo la kigaidi.
Hakuna mtu aliyekamatwa na kufikishwa mahakamani katika tukio la kujeruhiwa kwa viongozi wa Chadema wilayani Igunga, Arumeru na Arusha wakati wa kampeni za uchaguzi, na lile la kutekwa na kupigwa vibaya kwa viongozi sita wa CUF ndani ya kambi ya JWTZ ya Naliendele, mjini Mtwara.
Na hakuna ripoti ya uchunguzi uliofanywa kuhusiana na tukio la mlipuko wa bomu kwenye mkutano wa kampeni wa Chadema jijini Arusha wala kujeruhiwa kwa mbunge wa Iringa mjini, Peter Msigwa aliyekuwa anahutubia wafuasi wa chama chake.
Sasa kama matukio yale ya zamani hakukuwa na uchunguzi wa maana uliofanywa na Polisi ya Tanzania, na kwa kuwa hakukuonekana uchunguzi wa maana kwa matukio haya ya karibuni, Polisi ya Tanzania itapewa imani gani na wananchi kwamba inaweza kuchunguza na uchunguzi wake ukaaminika?
Basi kwa sababu hiyohiyo, ndipo nikasema sitarajii kupatikana wahalifu wa matukio haya mapya ya kigaidi. Utendaji wa Polisi ya Tanzania umeingiwa na shetani mbaya wa kisiasa. Siku hizi Polisi wakishashukiwa tu kuhusika na tukio la kihalifu, tayari wananchi hawatarajii kusikia matokeo ya uchunguzi.
Ila sasa, nimeingiwa na imani kubaini wamefika makachero wa Kiingereza kuja kuchunguza tukio la kumwagiwa tindikali wasichana wawili wa Kiingereza kulikofanywa na vijana waliopanda vespa mjini Zanzibar.
Makachero hawa watafanya uchunguzi makini. Wataandaa ripoti yao, wataikabidhi kwa serikali ya Tanzania. Sema sasa, baada ya ripoti kuingia mikononi mwa Serikali yetu, usije kushangaa isisikilikane hadharani.
Hizi ndio hofu nyingi nilizonazo. Zinatokana na mazoea ambayo Polisi ya Tanzania imeyajenga – ya kuzembea kuchunguza.
Chanzo: Mawio wiki hii

No comments:

Post a Comment