Karume, CUF nyuma ya Mansoor
MANSOOR Yusuf Himidi, Mwakilishi wa Jimbo la Kiembesamaki, Zanzibar, ambaye amefutwa uanachama wake ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wiki hii, anaungwa mkono kisiasa na baadhi ya waasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar na Chama Cha Wananchi (CUF), Raia Mwema limeambiwa.
Himidi alifukuzwa uanachama na Halmashauri Kuu ya CCM katika kikao chake kilichofanyika mjini Dodoma mwishoni mwa wiki iliyopita, katika tukio linalofananishwa na matukio mengine ya namna hiyo yaliyowahi kutokea katika miaka ya 1980 ndani ya chama hicho.
Kosa kubwa zaidi la kisiasa analodaiwa kulifanya Himidi ni kuunga mkono harakati za baadhi ya Wazanzibari wanaotaka muungano utakaovipa visiwa hivyo mamlaka kamili, kinyume na muundo wa sasa unaopigiwa chapuo na CCM.
Nyuma ya Himidi anatajwa kuwepo Rais wa zamani wa Zanzibar, Amani Karume, ambaye dada yake ameolewa na Mansoor katika ndoa iliyounganisha familia mbili zenye historia na serikali ya kwanza ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Wakati baba yake Amani, hayati Abeid Amani Karume, alikuwa Rais wa Kwanza wa SMZ, baba wa Mansoor, Brigadia Yusuf Himidi, alikuwa Mkuu wa Kwanza wa Vikosi vya SMZ (sawa na Mkuu wa Majeshi).
Ni mahusiano hayo ndiyo yaliyokuwa yakimfanya Mansoor aonekane anabebwa na kupewa nyadhifa muhimu wakati wa utawala wa Amani, ikiwamo uwaziri wa wizara nyeti ya Maji na Nishati na pia kuwa Mweka Hazina wa CCM visiwani humo.
Wafuatiliaji wa vikao hivyo vya CCM Dodoma, wameweka wazi kwamba wakati wa mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM uliofanyika Dodoma, Karume alikuwepo, lakini alionekana akiwa katika hali tofauti na ilivyokuwa zamani.
“Ukitazama katika picha ambayo Mwenyekiti (Rais Jakaya Kikwete) alikuwa akizindua Baraza la Wazee la Ushauri wa Chama, wenzake wote walikuwa wamevaa mashati yenye rangi ya chama chao isipokuwa yeye tu.
“Na hata lugha yake ya mwili ilikuwa tofauti. Hata kupiga makofi alikuwa kama analazimishwa. Tulijua tu kwamba amekasirishwa na uamuzi wa Kamati Maalumu ya Zanzibar kumshughulikia Mansoor,” alisema mjumbe mmoja wa NEC kutoka visiwani humo ambaye hakutaka kutajwa jina.
Mjumbe huyo wa NEC alisema ni wazi kwamba sasa kutakuwa na vita kali visiwani Zanzibar ndani ya CCM kwenyewe ambako kambi mbili zitakuwa zinapambana zenyewe. Kambi ya Karume na kambi iliyo chini ya Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein.
“Unajua wakati anawania urais wa Zanzibar mwaka 2000, Karume hakuwa na nguvu yoyote ya kisiasa pale Zanzibar. Hata Dk.Mohamed Ghalib Bilal, alikuwa na nguvu kumzidi. Alipata urais kwa sababu tu watu wa Bara walimtaka.
“Baada ya kuona kwamba hana nguvu sana Zanzibar miongoni mwa wahafidhina, Karume ameamua kuunganisha nguvu na wenzetu wa CUF, jambo linalompa nguvu kwa wananchi lakini linampa shida serikalini,” kilisema chanzo hicho.
Watafiti wa siasa za Zanzibar wanakubaliana kwamba Mansoor hana nguvu za kisiasa kama walizokuwa nazo Seif Shariff Hamad na Abood Jumbe wakati walipovuliwa nyadhifa zao za kisiasa, lakini nguvu yake kubwa iko katika maelewano aliyofanya na Karume na watu wa CUF.
Mansoor pia ana hazina miongoni mwa baadhi ya waasisi wa mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, waliofanya kazi na baba yake kwa karibu pamoja.
Ndiyo maana, yeye ni miongoni mwa wajumbe wa kamati inayofahamika kwa jina la Kamati ya Maridhiano ya Zanzibar –Inayoundwa na watu sita; wakiwamo wanachama watatu maarufu wa CCM na wengine watatu wa CUF, chini ya Hassan Nassor Moyo, mmoja wa waasisi hao.
Karume amekuwa karibu na siasa za CUF kutokana na kufanikisha kwake maridhiano ya sasa ya Zanzibar, baada ya kukutana na Maalim Seif kwa siri.
Kihistoria, kwa mujibu wa mmoja wa viongozi wa CCM aliyezungumza na Raia Mwema, mwanachama aliyefukuzwa kutoka kwenye chama tawala hicho, hawezi “kufufuka kutoka katika wafu” kama historia inavyoonyesha kwa akina Jumbe.
Hata hivyo, inaonekana kwamba kuna tofauti kubwa baina ya CCM ya miaka 1980 ambapo kulikuwa na mfumo wa chama kimoja na CCM ya sasa chini ya mfumo wa vyama vingi.
Kama alivyoandika mwanablogu mmoja katika miongoni mwa mitandao ya kijamii hapa nchini kwamba: “Hatma ya Mansoor kisiasa itatokana na namna maamuzi ya Katiba Mpya yatakavyokuwa kutokana na maoni ya wananchi.
“Kama rasimu itakidhi mahitaji ya Wazanzibari walio wengi, maisha ya kisiasa ya Mansoor na Karume yatakuwa yamefika mwisho, lakini kama Katiba mpya haitazingatia matakwa ya Wazanzibari walio wengi, huenda mwanasiasa huyo kijana mwenye umri wa miaka 46 tu, akaibuka kuwa shujaa mpya wa siasa za Zanzibar.
“Na inawezekana kabisa, Mansoor Yusuf Himidi, ameanza kujitengeneza kuwa mbadala wa siasa za akina Karume na Maalim Seif.
“Pengine, CCM imejiingiza katika mtego ambao ulikuwa umetegwa na wafuasi au watu walio nyuma ya mwanasiasa huyo. Kuna dalili kwamba kama kura ya maoni ya urais itapigwa leo kutafuta Mzanzibari atakayepigiwa kura nyingi na wafuasi wa vyama hasimu vya Zanzibar, huenda Mansoor Yusuf Himidi akawa kinara.”
Chanzo: Raia Mwema

No comments:
Post a Comment