Wednesday, 10 July 2013

Wende warudi, mamlaka kamili ndiyo jibu Zanzibar 


HaramaCHAMA Cha Mapinduzi (CCM) hakika kimo ndani ya mahangaiko makubwa yanayotosha kufanana na hali halisi inayomkabili mwanadamu anapokuwa anatapia roho baada ya kujikuta katika hatari inayomgharimu maisha.Mwenendo wa chama hichi ulioshuhudiwa siku chache za wiki iliyokwisha, unaonesha dhahiri jinsi viongozi wake wakuu wanavyojitahidi kupambana na wakati, kazi ngumu isiyomfalia mwanadamu hata kuijaribu.
Desturi ya mwanadamu ni kwenda na wakati na wala siyo kupambana au kupigana na wakati kwa sababu wakati ni jambo nyeti lisilomtizama mtu yeyote. Wakati ni tunu ya enzi isiyotetereka. Wakati unaelezea na kubainisha maisha halisi yanayojiri katika zama iliyopo.
Kwa namna wakati unavyojistawisha na kusawiri, mwanadamu hana namna ya kukabiliana nao. Na anapoamua kuingia katika mapambano na wakati inakuwa ni sawasawa na kibarua kinachomkabili mpanda farasi wawili kwa wakati mmoja. Hatimaye atapasuka msamba!
Mpanda farasi hata awe mahiri, stadi au fundi kiasi gani, ajuwe ataadhirika tu iwapo atashikilia kuwapanda farasi wawili kwa wakati. Huyu ngurumbili hakujaaliwa nguvu za kuwaongoza farasi wawili na kwa hivyo hata iweje, hatamudu kuwaongoza mbele.
Nina hakika mpanda farasi wawili hamudu leo na hatamudu siku yoyote ile kazi ya kuwaongoza mbele. Badala yake, nina imani kubwa kabisa, ataishia kuadhirika tu. Ima ataanguka kwa kushindwa kuwadhibiti, au ataangushwa na farasi mmojawapo.
Mpanda farasi huyu amekosea pamoja tu: ameamua kupambana na ukweli wa mambo au hali halisi. Amekataa kuamini kile anachokiona kinatokea. Amekataa ukweli na matokeo yake yatakuwa kuadhirika. Atapasuka msamba. Atakufa kihoro kwa sababu atapata matokeo ambayo hakujitayarisha kuyakabili.
Mwanadamu anaposhindwa kuusoma wakati, bila ya shaka utampita na atapitwa hasa na mazingira mapya yanayojengeka. Kwa asili, yeye ndiye anayeshika kamba ya kubadilisha mambo, lakini pale anapokuwa mgumu wa kwenda na wakati, kuikubali hali halisi iliyopo, basi wakati wenyewe utambadilisha.
Amekataa kuufuata wakati, utamlazimisha utakako. Hii ni akitaka asitake, ndivyo itakavyokuwa hatima yake.
Mara tu baada ya kuzinduliwa kwa rasimu ya katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Juni 3, mwaka huu, CCM iliharakia kuitisha kikao cha juu kinachojumuisha viongozi wake wachache – Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (CC-NEC).
Majadiliano yaliyojiri ni rasimu iliyotolewa hadharani chini ya ugeni wa heshima wa Makamu wa Rais wa Jamhuri, Dk. Mohamed Gharib Bilal. Viongozi wasaidizi wakuu wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi (BLM), yaani makamu wawili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi (VPII) na Maalim Seif Shariff Hamad (VPI) walikuwepo.
Kikubwa kilicholetwa ndani ya rasimu ya katiba ni pendekezo la mabadiliko ya mfumo wa kuendesha nchi kimuungano. Kwamba inapendekezwa kuwe na mfumo wa serikali tatu, kinyume kabisa na utashi wa CCM wanaoshikilia mfumo wa serikali mbili.
Haya ni mabadiliko makubwa. Ni mabadiliko yanayolenga kufuta mfumo ulioota mizizi kwa miaka 49 ya uhai wa Muungano wa Tanzania – zao lililotokana na kuunganishwa kwa dola mbili zilizokuwa huru – Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika, kulikofanywa Aprili 26, 1964.
Kumbe wakubwa wa CCM kama vile wameshtukizwa na pendekezo hilo. Kama vile hawakutarajia lingeletwa mbele ya wananchi wa Tanzania. Eti tuseme kuwa kunajengeka picha kwamba kilicholetwa katika rasimu, CCM hawakukijua, au hawakukiwaza kamwe.
Sitaki kuamini. Kwa namna wengi wa wakubwa hawa wanavyojinasibu, hakuna wasichokijua. Wanajua walichokitarajia kitakuja. Wanajua Tume ingeleta nini, ndivyo ilivyo imani yangu.
Kama hawakujua hiyo ni bahati mbaya inayotokana na kuzeeka kwao wakubwa hawa. Si chama hichi ninachokijua kujikuta kimeshtukizwa na jambo kubwa linalohusu mustakabali wa nchi. Hiyo si kawaida ya chama hichi.
Watanzania wamezoea CCM kujua kila kitu hata yale yaliyo ya siri. Wanajua kila kitu kinachopikwa na kilichowiva tayari kuliwa. Wanajua. Nasema hivi wenzangu, kama hawajui na hawakujua kuwa kungekuja pendekezo katika rasimu la kubadilisha mfumo wa Muungano, basi hiyo inatosha kuwa dalili ya wazi ya kutimia kwa enzi za mwisho za chama hicho.
Kumbe hawataki mabadiliko ya mfumo. Hawataki bwana. Ingawa anayeshikilia kijiti cha uongozi wa taifa sasa, Jakaya Mrisho Kikwete, ni mmoja wa wanasiasa waliokuwa vijana na kukaa mstari wa mbele katika kudai kuwepo kwa serikali ya Tanganyika mwaka 1994, ikiwa na maana ya kutaka ziwepo serikali tatu, mbali na zile za Muungano na Zanzibar, leo wameshtukizwa. Sijuwi.
Walipokutana katika Kamati Kuu wakasema haiwezekani. Hapana. Waliosema haiwezekani serikali tatu, tunaambiwa walilalamika sana, lakini hatimaye ikatoka sauti ya kimungu kuelekeza kama chochote “tuwaachie wanachama wetu waamue.”
Wakakubaliana watoke hapo na waende kwa wanachama wao, hawa nadhani wangali milioni tano tu ndani ya taifa lenye watu milioni 45 na ushei.
Sasa wiki iliyokwisha ndio walikuwa kwenye kazi ya kujenga hoja kwa wananchi wanaoitii CCM. Kwamba chama hichi hakitaki mfumo wa serikali tatu, kinataka taifa libaki na mfumo wa serikali mbili – ya Muungano inayofanya pia kazi kwa ajili ya watu wa Tanganyika peke yao, na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inayotumikia maslahi ya Wazanzibari.
Kule Tanganyika, ofisi ya Katibu Mwenezi, Nape Nnauye, inatajwa kuwa ndiyo inayoratibu utekelezaji wa jukumu la kuwapika wana-CCM ili waamini na kuupigania mfumo uliozeeka na kuushikilia usibadilishwe. Kwa Zanzibar, kazi hiyo inaonesha imeachiwa Naibu Katibu Mkuu wa chama, Vuai Ali Vuai.
Ukatumwa ujumbe kutembelea Zanzibar ili kujenga wanachama wao kujitambua kwa hilo. Ndipo yakatokea matukio ambayo nayaona kama yanayojenga taswira ya mantiki halisi ya yale aliyoyasema Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Ijumaa iliyopita.
Alisema si kazi ya kundi au chama chochote cha siasa, si kazi ya mtu yeyote, na wala si kazi ya taasisi au asasi yoyote ya kiraia kujenga morali wananchi wafuate maoni ya aina fulani wayatakayo. Kazi hiyo iachiwe Mabaraza ya Wilaya (kwa Zanzibar) na Kata kwa Tanganyika.
Mabaraza haya yameundwa na wajumbe waliochaguliwa na wananchi kwa kura kupitia uchaguzi ambao hata hivyo kwingi ulivurugwa kwa makusudi kwa ajili ya kuisaidia CCM iwe na udhibiti na sauti ya maamuzi ndani ya vikao vya mabaraza hayo.
Jaji Warioba anasema kazi ya kutoa maoni kuhusu yaliyopendekezwa kwenye rasimu kwa hatua ya sasa, inapaswa kuachwa kwa wajumbe wa mabaraza ambao wanaanza mikutano na vikao vyao Ijumaa.
Hapana shaka amechukizwa na alichokibani kutendeka. Amebaini kuna makundi vikiwemo vyama vya siasa, vinafundisha maoni yao yaaminike. Na hili ndilo linalofanywa na CCM.
Kwa Zanzibar, ujumbe umeongozwa na makada wakubwa watatu wakisaidiana na vijana wa jumuiya. Wameonekana watu wazima wakivimba mishipa ya shingo kufundisha vijana ndani ya ukumbi wa Chuo Kikuu cha Taifa (SUZA) na mafundisho hayo kuoneshwa moja kwa moja hewani kupitia vyombo vya habari Zanzibar.
Kwa bahati mbaya sana, walichokifundisha ni uasi ambao tayari watu waliosikiliza wamekerwa mno na kitendo cha wakubwa hao kuwajaza chuki vijana. Mengi ya yaliyoelezwa siyo tu kwamba hayana maana yoyote, bali pia hayasaidii kuijenga rasimu na hivyo wamebeza dhamira ya Tume ya Jaji Warioba. Kwa hakika vijana wanajazwa chuki tupu dhidi ya wananchi wenzao.
Pale Shaka Hamdu Shaka, naibu katibu mkuu wa UVCCM, alipoongoza kundi la vijana wenzake kutembea Zanzibar na kutoa maneno ya kifedhuli dhidi ya viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF), na hususan katibu mkuu wake, Maalim Seif Shariff Hamad, kumbe ni kutekeleza mkakati wa wakubwa zao wa kuzuia mabadiliko.
Ilikuwa ni kazi maalum iliyoelekezwa na wakubwa wa CCM. Naibu Katibu Mkuu wa Zanzibar, Vuai, aliongoza kikao ofisini Kisiwandui, na kuelekeza namna ya kutekeleza mkakati wa chama chao. Isitoshe, aliwahakikishia kuwa kazi hiyo ameagizwa na Makamu Mwenyekiti Dk. Ali Mohamed Shein.
Lakini lililo la kushangaza zaidi ni kauli yake kwamba katika kufanya kazi hiyo, vijana wameahidiwa malipo kabambe. Vijana fanyeni kazi na italipwa kwa gharama za chama. Ajabu iliyoje.
Ajabu yenyewe ni kwamba CCM wanafunga banda ilhali farasi ameshatoka bandani. Muamko wa wananchi katika mabadiliko hasa Unguja na Pemba ni mkubwa isivyo kawaida na kila mtu anayefuatilia anathibitisha ukweli huu. Hakuna kulala.
Kwa wale wanaoweza kuchukia si vibaya wakachukia lakini ukweli ni kwamba kazi adhimu iliyofanywa na Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislam (JUMIKI) imezaa matunda yanayoonekana hadharani bila ya kutumia tochi.
Kwa hivyo basi, ni vizuri viongozi wa CCM wajuwe mapema kwamba kule ndani ya mabaraza ya wilaya hakutakuwa na mchezo hata kidogo. Kazi kubwa ambayo haitumwi mtoto kuifanya. Kule hakutakuwa na nafasi hata ndogo ya kupindisha matakwa ya wananchi wa Zanzibar.
Wazanzibari walishaonesha mapema ni nini na nini wanachokitaka – mabadiliko ya mfumo wa Muungano. Si mbili na hata hizo tatu zilizoletwa na rasimu, haziwaridhishi iwapo mambo kadhaa yanayoitambulisha nchi yao hayatajumuishwa katika rasimu ya mwisho kuwa ndani ya mamlaka kamili ya Zanzibar.
Hili linajulikana wazi hata na viongozi wakubwa wa CCM. Kwamba kama maslahi ya Wazanzibari yatapuuzwa na kudharauliwa, ipo hatari ya rasimu kukwama itakapopigwa kura ya maoni. Sidhani kama hili litawafurahisha wakubwa. Watakuwa wanajidanganya wakidhani kutakuwa na nafasi ya mustakbali wa Zanzibar kubakishwa chini ya Katiba iliyozeeka ya 1977.
Chanzo: Fahamu

No comments:

Post a Comment