Wednesday, 17 July 2013

NDUGAI AIGEUKA CCM


Na Gabriel Mushi wa MTAZANIA Dar es Salaam
*Amgeuka pia Makinda, asema ni uongo, unafiki kupinga Serikali tatu…
WAKATI Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikipinga mapendekezo ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mpya juu ya muundo wa Muungano wa Serikali tatu, Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai amekigeuka Chama hicho, akisema wanaopinga suala hilo waache unafiki, uongo na kudanganyana.
Ndugai ambaye kwa upande wake alisema anaunga mkono muundo wa Serikali tatu kama Rasimu ya Katiba mpya inavyopendekeza.
Alitoa msimamo wake huo juzi Dar es Salaam, wakati akizungumza kwenye kipindi cha ‘Dakika 45’ kinachorushwa na kituo cha televisheni cha ITV.
Alisema kulingana na maoni yaliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ameyapokea kwa mikono miwili, hivyo wananchi wanatakiwa kuisoma rasimu hiyo, na wasiisome kama gazeti:
“Lakini moja ya mjadala mkubwa ni Serikali tatu…sio siri watu wamekuwa wakilijadili sana na hasa kutoka upande wa Zanzibar,” alisema Ndugai na kuongeza:
“Ni jambo ambalo wazee wetu wameliweka uwanjani tulitazame na tunapaswa kulitazama kwa umakini kwa sababu hili ni suala la msingi sana katika uendeshaji wa nchi yetu,”.
Alifafanua: “Ninadhani tuache unafiki, uongo na kudanganyana kwa hali ilivyo…huwezi kuzungumzia serikali moja au mbili…wenzetu Zanzibar watajiona wamemezwa,” alisisitiza:
“Hili ni jambo ambalo lilishindikana tangu mwaka 1964…ni kero ambazo hata tufanye nini zitaendelea…kwa hiyo nadhani wazee hawa walifikiri sana na nadhani wako sahihi kabisa,” alisema Ndugai ambaye pia ni Mbunge wa Kongwa, kupitia CCM.
Alisema suala la kutengana kwa sasa halipaswi kuzungumziwa labda huko baadaye, kwani suala la msingi sasa ni kuwasikiliza Wazanzibari wanataka nini na sio kuendeleza kiburi.
Mchakato wa Katiba mpya ya Tanzania upo katika hatua ya uchambuzi wa rasimu na watu mbalimbali kupitia Mabaraza ya Katiba, wameanza kutoa maoni yao.
Tayari CCM kupitia Kamati Kuu yake iliyoketi mjini Dodoma mwishoni mwa mwezi uliopita, kiliweka msimamo wa kutaka kuwepo kwa mfumo wa Serikali mbili katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete amekwishatangaza kuwa chama hicho kitakuwa moja ya mabaraza ya Katiba na kupata nafasi ya kuichambua, kuijadili na kutoa maoni kuhusu rasimu iliyotolewa hivi karibuni na Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Mwenyekiti wake, Jaji Joseph Warioba.
Wakati CCM kikiweka msimamo wake huo, Chadema kwa upande wake kimeeleza bayana kuunga mkono Serikali tatu, kama anavyopendekeza Ndugai.
Vyama vingine kama CUF, msimamo wake umekuwa haueleweki kwa sababu wakati Mwenyekiti wake, Profesa Ibrahimu Lipumba akiunga mkono Serikali tatu, Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad anataka uwepo Muungano wa Mkataba..

No comments:

Post a Comment