Maalim Seif hakukurupuka eneo la Darajani
Na mwandishi wetu Salim Said Salim
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akihoji bei ya mboga mboga katika soko la Darajani, wakati wa ziara yake ya kutembelea soko hilo hivi karibuni
UZOEFU katika maisha umethibitisha kwamba wahenga waliona mbali waliposema “Chombo hakiendi ikiwa kila mtu anapiga makasia yake.” Vilevile hawa wazee hawakuchoka kutuusia na kutuambia: Daraja ukilibomoa ujue kuogolea.
Nimezitoa methali hizi mbili ili kuwatahadharisha Wazanzibari juu ya hatari ya hali ya kisiasa ninayoiona huenda ikaibuka mbele ya safari na kuwarudisha kule walikotoka kwenye siasa za chuki, uhasama, matusi, kupigana na hata kuuwana.
Tuendelee kuomba Mungu aepushe mbali tusirejee kule ambako siasa ilikuwa ndio sababu ya mauti ya watu wengi, kuzalisha vizuka na mayatima wengi na wengi kukimbia nchi yao.
Hata hivyo, kila panapochomoza vidudu mtu vinavyoshabikia maovu kama haya, upo wajibu wa kukumbushana na kupeana wasia, kama walivyofanya wazee wetu siku za nyuma na methali zile kuwa na maana mpaka hii leo.
Kwa jinsi hali ninayoina Zanzibar hivi sasa naona kama walivyosema wazee juu ya kutokuwepo usalama katika safari ya visiwa hivi kwa vile kila mmoja anapiga makasia yake.
Safari ninayoizungumzia hapa ni ya kisiasa. Kinachoonekana viongozi wetu wanatuonesha waziwazi kuwa kila mmoja anapiga makasia yake na tayari chombo kinaanza kwenda mrama ishara ya hatari ya kuzama.
Mmoja wa mifano mingi ya kuthibitisha haya ni viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na hasa Jeshi la Polisi kuridhia, kama vile ni sahihi, kwa baadhi ya hao wanaoitwa viongozi wa kisiasa (mimi nawaita wahuni) wanaoweza kupanda juu ya jukwaa na kutukana matusi ya nguoni viongozi wakuu wa nchi.
Kitendo cha kuwaridhia wahuni kutukana viongozi, iwe kwa kauli za mdomoni au kutumia mabao ya mtangazo, ni kielelezo kinachoonesha viongozi wetu wameamua kila mmoja kupiga makasia yake. Ndio maana tunaona safari yetu ya serikali ya umoja wa kitaifa imo shidani.
Jengine ambalo ni baya zaidi ni huu uamuzi wa baadhi ya viongozi wa SMZ (wananchi wanawataja kwa majina) wa kuamua kukejeli na kufanyia jeuri agizo la Makamo wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad alipotembelea soko kuu la Darajani, mjini Unguja wiki iliyopita.
Maalim Seif alisema, kama ilivyo sheria ya Zanzibar ya tokea siku za ukoloni, ya watu kuwa huru kufanya biashara wakati wa mwezi wa Ramadhani katika eneo hilo, basi mamia ya vijana wanaotafuta rizki hapo waachiwe kufanya hivyo mpaka utapomalizika mwezi huu.
Kauli hiyo imeonekana kuwakera baadhi ya wakubwa katika serikali, kama vile na wao hawauheshimu na kuutukuza mwezi wa Ramadhani.
Vijana wa linaloitwa Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) ambalo baadhi ya wananchi wanaliona ni Jeshi la Kutesa Umma walivamia eneo hilo siku ya pili yake kuonyesha dhihaka na jeuri kwa agizo la Makamo wa Pili wa Rais ambaye alifuatana na viongozi kadhaa katika safari yake.
Vijana hawa walionesha uhuni uliokubuhu. Kwanza kama kawaida yao, walipiga watu ovyo na hata kupora bidhaa zao. Ni aibu kwa Zanzibar kuwa na jeshi lenye wahuni wa kiwango hiki. Inasikitisha, na zaidi kuona ushenzi huu unafanyika katika mwezi ambao Waislamu wanaamini ni wa rehma, kuoneana imani na kusaidiana.
Lakini kilichoonekana hapa huu uhuni wa askari wa JKU ndio aina ya rehma na msaada ambao wamepewa mafunzo ya kuutumia.
Ninaamini kwa dhati kabisa vijana hawa hawakwenda pale Darajani na kufanya uhuni ule bila ya kutumwa na wakubwa zao. Walitekeleza amri ya viongozi wanaojijua na ambao wajuwe wananchi wanawajua vilevile.
Uhuni huu unaonesha dhahiri kuwepo kundi la watu wasioitakia mema serikali ya umoja wa kitaifa pamoja na nchi. Waniona serikali ya mfumo huu inasumbua uwezo na utashi wao wa kupora mali za watu, kupiga na hata kuua.
Ama kweli washairi wa karibuni, kama walivyo wale wahenga, hawakukosea waliposema: Aliyezowea vya kunyonga vya kuchinja haviwezi.
Huu si ustaarabu, hasa ukitilia maanani kwamba Zanzibar ilianza kutulia baada ya kuwa katika kipindi kilichojaa zahma za kisiasa baada ya kupatikana maridhiano ambayo baadhi ya viongozi kwa kuwa sasa wapo madarakani wanaonesha jeuri.
Watu hawa wanasahau kuwa kama siyo maridhiano ingelikuwa vigumu kwao kufika hapo walipo na ambapo wanapatumia kuhujumu wananchi. Ni vyema watazame hali inavyokuwa mbaya na nchi kutokalika kwa utulivu wakati pakikosekana siasa za maridhiano zinazohusisha kuvumiliana sana kisiasa.
Ni vizuri wahusika wa kufitini wakaacha mara moja mtindo wa kila mmoja kupiga kasia lake na tupige makasia kwa pamoja. Njia nzuri ya kuanzia ni kuwatia adabu wale wote waliotoa amri kwa askari wa JKU kwenda Darajani kufanya uhuni ulioonesha kukejeli agizo la Makamo wa Kwanza wa Rais.
Ninaamini kwa dhati hao waliotoa amri hiyo hawatawaelekeza hata siku moja hao wanaoitwa askari wa JKU kwenda kukejeli amri ya Rais au ya Makamo wa Pili wa Rais.
Lakini wamefanya hivyo kwa sababu wanayo ajenda yao ya siri ambayo sasa ipo dhahir shahir na kwa uwezo wa Mwenyeezi Mungu hatafanikiwa kuwarejesha Wazanzibari katika siasa za kupigana na kuuwana.
Ni vyema watu hao wakajirudi. Warudi kwenye mstari. Watu hawa mahodari wa kutumia vyombo vya habari vilivyo chini ya Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC) kufanya kile ambacho kwa wengi kinaokena kama ni kutaka kuwarejesha Wazanzibari walikotoka kwa sauti za upande mmoja tu kusikika zikishutumu watu wengine.
Watendaji wahafidhina hawa wasiotaka kuona Wazanzibari wanaishi kwa raha mustarehe ndani ya nchi wanayoipenda huku wakishindana bila ya kupigana, wametuma waandishi wa gazeti la Zanzibar Leo, kituo cha redio kilichokuwa Sauti ya Tanzania Zanzibar (STZ) na televisheni ya TVZ kutafuta habari zilizolenga kujenga picha kwa umma kwamba agizo la Makamu wa Kwanza wa Rais halikuwa la busara. Waoneshe kuwa kiongozi huyu alikurupuka.
Siku ya pili tu baada ya agizo lile, ZBC Redio na televisheni zilikuja na taarifa za kuonesha utekelezaji wa agizo umeharibu taswira ya eneo la Darajani. Umewavimbisha kichwa wafanyabiashara na mbaya zaidi umewachochea wafanyabiashara walioko Saateni kugoma kulipa ushuru kwa madai kuwa wanabaguliwa kushikiliwa kubaki huko ilhali wenzao wanadekezwa kukaa Darajani na hivyo kupata wateja bila shida.
Kinachosababisha yote hayo mabaya ni mipango mibaya ya serikali tangu hata serikali ya umoja haijaingia. Serikali wakiwemo na viongozi wa Baraza la Manispaa wenyewe wameshindwa kutafutia ufumbuzi tatizo la matumizi mabaya ya eneo hilo.
Wakiulizwa viongozi hao ni kwanini mpaka leo imeshindikana kutekeleza mpango wa kuendeleza mji (Master Plan) uliohusisha ramani ya kuvutia machoni mwa mtu iliyowahi kupachikwa pale Darajani? Mbona hakuna maelezo yoyote mpaka leo ya ulikotokomea mradi ule? Viongozi waadilifu wangetoka hadharani na kuwaambia wananchi kilichotokea kuhusu mradi ule.
Hakika tunajua Maalim Seif hakukurupuka kutoa agizo lile. Alikuwa ameamua hasa kutoa ujumbe mzito tangu mwanzo wa ziara yake ile. Alikuwa anajua vizuri hali iliyopo. Anaijua hali inayowakumba wafanyabiashara hao ya kila siku kukimbizana na askari wanaojificha nyuso zao kwa soksi zinazotoa harufu mbaya. Anayajuwa yote haya.
Makamo wa Kwanza wa Rais anajuwa mtindo huo umekuwa ukiumiza wananchi wanaohangaika kupata chejio. Anajuwa hawana kazi nyingine ya kufanya ili kumudu uwezo wa kuhudumia familia zao. Ndio, Maalim Seif anajuwa wanaohangaikia maisha Darajani wana familia zao zinazowategemea kimaisha.
Sasa wanaponyanyaswa kila kukicha, wanapopigwa na kudhalilishwa kila kukicha huku wakiporwa bidhaa zao, ndio serikali yao iliyoapa kuwatumikia wao itakuwa inajenga au inabomoa? Itakuwa inawasaidia kumudu maisha au inawakandamiza na kuwavunja moyo?
Ukweli Maalim Seif anajuwa fika kwamba serikali ambayo haijafanikiwa kuondoa tatizo kubwa la ajira linaloongezeka kila mwaka kwa maelfu ya vijana kuingia katika soko la ajira wakitafuta maisha baada ya kushindwa kuendelea na masomo, wana haki ya kufanya kazi. Wataishije bila ya kufanya kazi? Na serikali haipaswi kuvunja haki hii ya binadamu kwa visingizio visivyo mashiko.
Haya ya fikra za upande mmoja yanaonekana katika mjadala wa rasimu ya katiba na wanaopanga njama hizi wanajulikana. Ni pamoja na wale wanaoweka vizingiti na kutaka kuzuwia magazeti huru yasisajiliwe Zanzibar. Kwa kweli wamechelewa, kila wanachofanya dhahiri na siri kinajulikana. Hawana nafasi hata chembe ya kufanikiwa.
Watu hawa wanapaswa kujua sasa kuwa wanachokifanya ni sawa na simulizi ya mtu kulivunja daraja linalowaunganisha Wazanzibari lengo likiwa ni kuwaangamiza. Sasa ninawauliza, kama walivyotuasa wahenga: Jee, wameshajifunza kuogelea? Kama bado, ni kwanini basi wanafanya hima na njama za kulibomoa daraja?
Nijuavyo mimi wengi wao hawajuwi kuogelea kwa vile si wana kindakindaki wa Zanzibar nchi ambayo watu wake wengi hujuwa kuogelea. Kwa hivyo ni vizuri waelewe kuwa Wazanzibari kindakindaki si watakaozama kwani wanazijua mbinu za kujiokoa pale jahazi la kisiasa likizama, ikiwa pamoja na kuogelea.
Wenyewe Wazanzibari wana wa kindakindaki yakitokea tu hujisemea: “Poo…simo.” Jee wao wenzangu na mie waliopo mbele kuchochea fitna na idhilali watajiokoaje wasikumbwe na madhara ya idhilali hiyo?
Tumuombe Mungu aiepushe Zanzibar na hawa mahasidi wasiovitakia kheri visiwa vya Unguja na Pemba. Mungu ajaalie watu wake waendelee kuishi kwa amani, raha, furaha na maelewano yenye maridhiano ya kweli na siyo ya kinafiki.
Chanzo: Fahamu
No comments:
Post a Comment